HOFU ya kutekwa, kuteswa na
kupelekwa katika msitu wa Mabwepande kama ilivyokuwa kwa Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, imeanza kumtesa Rais wa
Chama cha Walimu (CWT), Gratian Mukoba.
Mukoba alisema amekuwa akipata vitisho vya
kumzuia kushiriki kwenye mgomo walioupanga kuuanza kesho, lakini amedai
vitisho hivyo havimzuii kuendelea na mkakati wa kutafuta haki za walimu.
Mukoba alisema hata kama
atapelekwa katika msitu huo uliojipatia umaarufu mkubwa kwa kutumiwa
kuendesha vitendo vya utesaji na uuaji, bado ukweli utabaki palepale kuwa
walimu wana madai ya msingi ambayo yamekuwa yakipigwa danadana na serikali.
Alibainisha kuwa watu wanaofikiri
kuwa paka anaweza kugeuka simba wanajidanganya kwa sababu haki ya mtu haiwezi
kuminywa na mtu yeyote hata kama ana madaraka makubwa.
“Unapomuona paka nyumbani kwako
huwezi kumwita simba …eeh hata kama napata vitisho havitanifanya kuacha
kutimiza majukumu yangu, hata kama mimi nitapata matatizo wapo watakaoendelea
na kupigania haki za walimu, kwakuwa huwezi kuzuia na kumnyamazisha kila mtu,
hasa katika masilahi ya taifa,” alisema.
Alisema anaamini kuwa kile
kilichomtokea Dk. Ulimboka hakitaweza kumtokea yeye kwa sababu watetezi
mbalimbali na mikataba mingi ya kimataifa ipo na inasimamiwa kikamilifu na
watu wasiopenda haki za watu zipotee.
Mukoba alisema serikali haina haja
ya kutoa vitisho kwa walimu kuwa mgomo wao ni batili bali iueleze umma ni
kesi gani na namba ngapi iliyopo mahakamani inayozuia mgomo huo.
“Serikali imezoea kupiga porojo za
kisiasa, porojo zao hazituzuii wala kutunyamazisha kuendelea na msimamo wetu
wa kuanza mgomo kesho,” alisema.
Fomu za serikali
Serikali imesambaza fomu kwa
maofisa elimu wa wilaya ikiwataka wazigawe kwa walimu na wajaze haraka ili
wabaini wanaounga au kupinga mgomo huo.
Fomu zimeandikwa maneno ya ‘Haraka
Sana’, zina sehemu mbalimbali ambazo zinamtaka mwalimu kuandika namba yake ya
hundi, kuunga mkono mgomo au kutounga mkono.
Kwa mujibu wa Mukoba, sehemu ya
namba ya hundi imewekwa mahususi kuwakata mishahara walimu watakaoshiriki
kwenye mgomo huo.
“Nawaomba walimu waendelee na
msimamo wao, maana wasiposimama imara kutetea haki zao hakuna
atakayewasaidia, mgomo huo hautaathiri utumishi wao, kwa kuwa umezingatia
sheria,” alisema na kukiri kuwa kutakuwa na vitisho na propaganda nyingi
kutoka kwa waajiri.
Kuhusu suala la serikali lililopo
mahakamani, Mukoba alisema hatua hiyo haiondoi taratibu za mgomo na kuongeza
kwamba serikali isitake kutumia kivuli cha mahakama kukandamiza haki za
walimu ambao wamezingatia taratibu na sheria zote za nchi katika mgomo huo.
Juzi CWT kilitangaza mgomo rasmi
huku kikikamilisha taratibu za mgomo kwa kupiga kura kuunga au kukataa mgomo
huo, ambapo kati ya walimu 183,000 walimu 153,848 sawa na asilimia 95 ya
walimu waliunga mkono kufanyika kwa mgomo.
Hatua hiyo imekuja baada ya
serikali na CWT kushindwa kufikia makubaliano katika siku 30 walizoipa
kuanzia Juni 25 mwaka huu.
Madai makubwa ya walimu katika
mgomo huo, mbali na malimbikizo ya madeni yao ya huko nyuma, pia wanataka
ongezeko la mishahara kwa asilimia 100, posho za kufundishia kwa walimu wa
sayansi asilimia 55 na walimu wa masomo ya sanaa asilimia 50 na posho za
mazingira magumu asilimia 30.
Mara baada ya tishio hilo la CWT,
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ofisi ya Rais (Ikulu), kupitia kwa Kaimu Katibu
Mkuu Kiongozi, Peniel Lyimo, juzi ilitoa taarifa kupinga mgomo huo kwa madai
kuwa ni batili, kwa sababu kuna kesi mahakamani inayozihusu pande hizo mbili.
“Kwa sasa shauri hili liko
Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na leo hii siku ya Ijumaa Julai 27, 2012
majira ya saa sita mchana pande zote mbili zilifika mahakamani na mahakama
ikaamuru kwamba pande zote zikamilishe maelezo yao ifikapo siku ya Jumanne
Julai 31, 2012 saa sita mchana ili kuiwezesha mahakama kuendelea kusikiliza
shauri hilo na hatimaye kutoa uamuzi. Kwa hiyo mgomo huo si halali kwa vile
shauri hilo bado liko mahakamani,” ilisema.
Maandalizi mikoani
Mkoani Mbeya, Kaimu Katibu wa CWT
Mkoa wa Mbeya, Felix Mnyanyi, alisema mazungumzo kati ya walimu na serikali
yameshindikana baada ya kuthibitishwa na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA)
na kesho walimu watagoma.
Mkoani Mara, Mwenyekiti wa CWT
wilayani Bunda, Francis Ruhumbika, amewataka walimu wote kushiriki kwenye
mgomo huo kwa kutokwenda kwenye vituo vyao vya kazi.
CHANZO GAZETI LA TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment