Friday, August 31, 2012

Peramiho imesheheni vivutio vya utalii wa kihistoria


Na Albano Midelo

Mji wa Peramiho uliopo wilayani Songea mkoani Ruvuma ni miongoni mwa miji ya zamani yenye historia ya kipekee katika kanda ya kusini.Mji wa Peramiho unafahamika zaidi nje ya nchi pengine kuliko miji mingine iliyopo kusini mwa Tanzania kutokana na mji huo kuwa na historia ya namna yake kipekee.

Historia ya mji wa Peramiho uliopo kilometa 24 tu kutoka makao makuu ya mkoa wa Ruvuma mjini Songea inaunganishwa  na wabenediktini wa kanisa katoliki kutoka St.Otilia nchini Ujerumani,ambao waliamua kuweka makao makuu yao katika Abasia ya Peramiho.
 
Wabeneditine hao waliingia kwa mara ya kwanza katika mji huo mkongwe mwaka  1898 wakiongozwa na Kasian Spiss.Tangu wakati huo wabenediktine hao wamekuwa na  wakifanya mambo mazuri na ya kipekee katika mji huo hali iliyosababisha kuutambua mji wa Peramiho kuwa ni mji unaokidhi vigezo kuwa mji wenye utalii wa kihistoria.


Mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya Taifa ya Majimaji Philipo Maligisu anasema  wabenediktine wa Abasia ya Peramiho wametengeneza historia ya kipekee na kuvutia katika nchi ya Tanzania ambapoWabenedikitine hao jambo kubwa la kwanza ambalo limeacha historia katika mji wa Peramiho na taifa kwa ujumla ni pale walipoamua kujikita katika suala zima la elimu na kuamua kuwekeza katika elimu zaidi ya miaka 100 iliyopita hadi sasa.

Historia inaonesha kuwa walipoingia kwa mara ya kwanza wabenediktine hao kwa kutambua umuhimu wa elimu  waliamua kuanzisha madarasa kwa kufundisha walimu na kufundisha wanafunzi hivyo kufundisha elimu zote mbili yaani elimu ya kiroho na elimu dunia.

Kwa msingi huo eneo la Peramiho  katika historia ya Tanzania lina historia ya kipekee kwa zaidi ya miaka 100 sasa hivyo kuna ushahidi ambao unaonyesha wabenediktine walidhamiria kufanya mambo ya msingi katika mji wa Peramiho na taifa kwa ujumla.

 Utafiti uliofanywa katika mji wa Peramiho unaonesha kuwa wabenediktine hao walizindua rasmi mji huo Julai 31,1898 na tangu hapo waliendelea na shughuli zao wakiwa na mahusiano mazuri wakati huo na utawala wa machifu katika eneo hilo.

Hata hivyo mahusiano hayo mazuri baina ya wabenedikitine hao wa kutoka nchini Ujerumani na machifu  ulikuja kuharibika wakati wa vita vya majimaji ambavyo vilianza mwaka 1905 na kumalizika mwaka 1907 na kusababisha padre Fransis Scuss kuuwawa Septemba 9 1905.

Baada ya kumalizika vita hivyo vya majimaji ilijitengeneza tena historia ya kanisa la Abasia ya Peramiho  hivyo kulichukulia eneo hilo la mji wa Peramiho kama eneo la kipekee kwa kuzingatia misingi ya sheria ya Tanzania namba 10 ya mwaka 1964 na maboresho yake sheria 22 ya mwaka 1979 ambayo inayatambua maeneo yote ya kihistoria kulingana na umuhimu wake katika jamii.

Hadi sasa watanzania wengi hapa nchini bado hawajatambua kuwa mji wa Peramiho una historia ya kipekee inayowaunganisha wananchi wa Ruvuma na sehemu nyingine duniani na hasa nchi ya Ujerumani ambao wanaitambua sana Peramiho.

“Wananchi wa Ujerumani  wanaijua sana Peramiho pengine kuliko hata sisi watanzania,ndiyo maana  kizazi na kizazi wanasafiri kwa gharama kubwa hadi katika mji huo ili kufanya utalii wa kihistoria kwa kutembelea katika maeneo mbalimbali ya kihistoria na kujifunza mambo mbalimbali”,anasisitiza Maligisu.

Sera ya taifa ya utamaduni ya mwaka  1997  ina tamka bayana kuwa  eneo lolote la kihistoria linapokuwa limetimiza miaka 100 tayari moja kwa moja linaingia katika urithi wa utamaduni wa  taifa.Kutokana na hali hiyo ukiangalia mji huo wa Peramiho tayari umekidhi vigezo na maeneo yake yote ya kihistoria kuingia katika urithi wa utamaduni wa taifa kwa ajili ya kujifunza elimu na utalii .

“Hivi sasa mimi kama mhifadhi kutoka makumbusho ya taifa tupo katika mchakato wa kuliingiza eneo la Peramiho katika urithi wa utamaduni wa taifa na watu wengi watatembelea kwa lengo la kuhitaji kufanya utafiti, kujifunza na kujua nini kilichopo ndani”,anasema mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya Taifa.


Akizungumzia nini kilisababisha wamisionari wabenedikitine kuchagua eneo la Peramiho na sio mahali pengine,mhifadhi huyo anasema  padre Maurus ambaye wakati huo alikuwa ndiyo mkuu wa jimbo lililoitwa kusini ya Zanzibar mwaka 1888 alipita wakati huo akiangalia namna wabenedikitine kutoka St. Otilia Ujerumani wanavyoweza kufika nchini kueneza injili kusini magharibi mwa Tanzania.

Wabenediktine hao walifika hapa nchini kwa lengo la kufanya uinjilishaji na sio katika mambo ya kisiasa ndiyo maana waliamua kujenga misheni nje ya makao makuu ya serikali.Hata hivyo  mwanzilishi wa uinjilishaji  aliwaonya wabenedikitine kujihadhari kujiingiza katika mambo ya siasa badala yake wajikite katika lengo lililowaleta hivyo walianzisha misheni katika maeneo ya mbali zaidi ya serikali kama Peramiho badala ya Songea mjini.

Hata hivyo historia inaonesha wabenediktine walifikia  katika mlima wa Peramiho ambapo waliamua kujenga kanisa la mwanzo na nyuma ya hospitali ya misheni ya Peramiho ambako kuna chuo cha uuguzi.

Kabla ya kujengwa kanisa katika eneo hilo, wabenediktini hao walisimika msalaba kwa mara ya kwanza Julai 31,1898 na kuongoza misa na hatimaye kujenga monasteri ya masista na kuanza kujenga msingi wa kanisa dogo lenye urefu wa mita 13 na upana mita saba. Kadri miaka ilivyozidi idadi ya wakristo iliendelea kuongezeka na kufanya kanisa hilo la mwanzo kuwa ndogo ndipo wabenedikitine hao waliamua kujenga kanisa kubwa jipya la sasa .

Kwa mujibu wa machapisho ya ujio  wa wabenedikitine  katika Abasia ya Peramiho,padre Kassian Spiss alifanya kazi Kurasini Dar es salaam mwaka 1893 na baadaye akahamishiwa Tosamaganga Iringa mwaka 1897.Hata hivyo padre huyo alitumwa kuanzisha misioni katika nchi ya wangoni yaani mkoa wa Ruvuma hususan Songea Peramiho Julai 31,1898.

Padre Spiss na wenzake mnamo walifanikiwa kufika ungoni na siku iliyofuata walifika katika boma la Songea na kupokelewa na wakuu wa boma wakati huo waliishi kwa siku tatu.Baada ya siku tatu waliendelea na safari kuelekea magharibi,kisha walifuata barabara na kuchepuka kushoto na kusimika hema lao katika kijiji cha Maposeni wakati huo kikiitwa Mbinga mhalule.

Kwa mujibu wa historia hiyo siku iliyofuata padre Kasian alisoma misa kwenye kaburi la sultani Mhalule  ambaye alikuwa anaheshimiwa na wangoni wa eneo hilo wakati huo,Chief wa wangoni aliposikia kwamba padre Kasian na ujio wa wamisionari wamefika katika eneo hilo la wangoni alikwenda kusalimiana nao na kutoa zawadi ya mbuzi dume yaani beberu aliyenona akionesha kuwaunga mkono wamisionari hao.

Baada ya kuhafamiana padre Kasian alimpa chifu Mputa zawadi ya nguo ambayo watoto wawili wa Sultani Mhalule na chifu Mputa akiwa na mdogo wake  Chemchaya waliamua kuhama eneo hilo hivyo walijenga  eneo la umbali  upande wa kaskazini ambapo chifu Mputa aliwaalika wamisionari kumtembelea siku iliofuata katika mji wake mpya wa Maposeni na walikaa kwake kwa siku mbili.

Baada ya muda padre Kassian alikwenda Songea bomani ambapo ndiyo siku hizi wanaita kwa mkuu wa wilaya ili kufuatilia mashauri ambapo wakati anakwenda alipita njia ya mkato ili afike mlima Mbewike.Wakati anapita katika mlima Mbewike ndipo aligundua kuwa  mahali pengine pazuri juu ya mlima Peramiho ndipo akaamua kuanzisha misioni mahali hapo ndiyo Peramiho ya leo.

Mnamo Julai 31,1898 misa ya kwanza ilisomwa Peramiho ndipo ukawa mwanzo wa misioni ya kwanza ilioanzishwa ungonini na kwamba Agosti 5,1898 wamisionari hao walipima kiwanja na kujenga msingi wa kanisa, jengo la kwanza la kanisa lilijengwa kwa miti ,mianzi na kuezekwa kwa nyasi.

Wenyeji wa Peramiho walifanya kazi ya ujenzi kwa kushirikiana na wamisionari bila shida yeyote ambapo kila jumbe alikuwa anakuja na watu wake na kusaidia kazi kila alipohitajika.Majengo ya kwanza ya wamisionari katika mji wa Peramiho yalijengwa mwaka 1898 zikiwemo nyumba za wamisonari  na kanisa dogo.

Mwaka1902 hadi 1905 kanisa zuri  lilijengwa katika mji wa Peramiho pamoja na nyumba nyingi za wamisionari ambapo padre Kasian Spiss alikuwa ndiyo paroko wa kwanza wa Peramiho,Padre ambaye aliwekwa wakfu Novemba 16,1902 kuwa askofu wa kwanza wa jimbo la Zanzibar kusini,makao makuu yake yalikuwa ni Peramiho na Kigonsera.


Katika tukio la kusikitisha Askofu Kasian mnamo Agosti 14,1905 ikiwa takriban saa mbili asubuhi akiwa anarudi Kilwa baada ya kusikia Liwale kuna vurugu,alikutana na wapiganaji wa vita vya Majimaji ambao walimua yeye pamoja na wenzake katika eneo la Mikukuyumbu Liwale.

Baada ya kuuwawa Askofu Kasian nafasi yake ilichukuliwa na padre Franziskus aliyekuwa paroko wa Peramiho ambaye baada ya vita kutokea  alikataa kutorokea  Kigonsera hivyo na yeye aliuwawa na wangoni huko Maposeni .

Ujenzi wa kanisa kuu la Peramiho ulianza wakati Askofu Gallus Steiger  na bruda Gisral Stumpf ambaye aliandaa mchoro wa kanisa hilo mwaka 1940 na  mwaka 1941 msanii wa majengo  Hans Burkard wa Uswis alisanifisha rasimu ya michoro hiyo na kumrejeshea Askofu Gallus mwaka 1943 na michoro kukamilisha na bruda Gislar.

Juni 29,1943 matofali 10,000 yaliofyatuliwa katika eneo la mto Luwawasi chini ya usimamizi bruda Mansuet Mendlel yalifikishwa katika eneo la ujenzi wa kanisa hilo ambapo jumla ya matofali milioni tatu yalihitajika.

Udongo kwa ajili ya kutengenezea vigae pia ulihitajika ambapo vigae vilitengenezwa   na kusafirishwa kutoka Matomondo wilayani Songea hadi mto Ruvuma chini ya usimamizi wa bruda Luitfried Kramer na kazi ya ujenzi wa kanisa hilo ilianza Julai 6,1943 na kumalizika Septemba 9,1943.

Kenchi za mihimili ya kanisa kuu hilo zenye uzito wa tani tano chini ya usimamizi wa mabruda Nonosius Bleicher na Menas Leicht ilifanyika na kupandishwa  kwa mashine maalum iliyotengenezwa na bruda Jucundus Weigele Agosti 1946.

Mnamo Novemba 24,1945 vigae vyote 120,000 vilikuwa tayari kwa ajili ya kuezekea kanisa hilo na mnamo mwaka 1948 kanisa kuu Peramiho lilibarikiwa na padre Heribert  na padre Gerod Rupper akawa padre wa kwanza kuhubiri katika kanisa hilo jipya.

Ukiachia mbali kanisa la kihistoria,lakini pia Abasia ya Peramiho ina seminari kuu,hospitali ya misheni ambayo serikali imeipandisha hadhi kuwa hospitali ya rufaa,chuo cha uuguzi,kiwanda cha uchapaji yaani Peramiho printing press,chuo cha ufundi seremala,magari na umeme na tawi la chuo kikuu cha madaktari Bugando.

                    










No comments:

Post a Comment