Tuesday, August 28, 2012

Samaki wanaotoa umeme kivutio adimu cha utalii



Na Albano Midelo
 TANZANIA ni nchi pekee katika Afrika mashariki ambayo imebahatika kuwa na vivutio vya kipekee vya utalii ambavyo huwezi kuviona katika sehemu nyingine yeyote duniani.

Nchi yetu imebahatika kuwa na maziwa mengi kuliko nchi yeyote katika bara la Afrika.Maziwa hayo ni pamoja na ziwa Viktoria,Tanganyika,Nyasa,Rukwa na maziwa mengine madogo.

 Ziwa Tanganyika lililopo magharibi mwa nchi ni miongoni mwa  kivutio cha utalii.Ziwa hilo lipo katika mikoa ya Kigoma na Rukwa na kuelekea hadi katika nchi jirani za Kongo DRC na Burundi.

 
Ziwa Tanganyika lina sifa kuu nne ambazo pamoja na kuwa ziwa refu kuliko maziwa yote ulimwenguni likiwa na urefu wa kilometa 673 kutoka kaskazini hadi kusini mwa ziwa hilo.

Sifa nyingine ya ziwa Tanganyika ni kuwa na kina kirefu kwenda chini.Ziwa hilo linashika nafasi ya pili kwa kina kirefu ulimwenguni baada ya nafasi ya kwanza kuchukuliwa na ziwa Baikar ambalo lipo  katika nchi ya Rusia.

Kina cha ziwa Tanganyika ni kilometa 1.47 au meta 1470  hivyo ziwa hilo kuwa na kina cha kipekee ambacho ni kivutio cha utalii kianchoweza kuwasukuma watalii  kufika katika ziwa hilo kuona maajabu hayo.

Ziwa hilo linawashangaza wengi kwa ukubwa na ujazo wake ambao ni kilometa za ukubwa 18,900 na kwamba ziwa hilo linachukua asilimia 17 ya maji yote baridi ulimwenguni.

Kana kwamba haitoshi ziwa Tanganyika lina utajiri mkubwa  wa viumbe hai wa aina mbalimbali wakiwemo samaki,mamba,viboko pamoja na viumbe wengine wa majini.

Watu wanaotaka kujifunza kupitia ziwa hilo wanapata fursa ya  mambo mbalimbali ya kibaiolojia na kiuchumi hasa kutokana na samaki wa aina  mbalimbali waliomo katika ziwa hilo.

Ziwa Tanganyika lina aina za samaki zaidi ya 400  na  kati ya aina hizo za samaki kuna aina ya samaki ambao wana uwezo wa kutoa umeme wanaofahamika kwa jina la electric fish haya ni maajabu  mengine ya dunia ambayo yanawashangaza wengi.

Kutokana na sensa ya samaki ya mwaka 1999 ziwa Tanganyika linakadiriwa kuzalisha samaki kati ya tani 165,000 hadi 200,000 zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 80 hadi milioni 100.Miongoni mwa samaki maarufu katika ziwa hilo ni dagaa, migebuka, kambale, sangara, magege,samaki wa mapambo, singidae na kuhe.

Mhifadhi kutoka hifadhi ya Gombe Noelia Mnyonga ambaye analifahamu vyema ziwa Tanganyika,  akizungumzia samaki ambao wanatoa umeme,anabainisha kuwa aina hiyo ya samaki wanatoa umeme pale wanaposogelewa na adui hivyo kuwa kivutio adimu na cha kipekee ulimwenguni.

“Samaki huyu kwa kuwa anatoa umeme iwapo angetangazwa ndani na nje ya nchi watalii wengi wangemiminika kwenda katika ziwa Tanganyika ili kwenda kuwaona na hivyo serikali kupata kipato kikubwa”,anasisitiza Mnyonga.

Anaongeza kuwa watalii hao baada ya kusikia habari za samaki anayetoa umeme hakuna ubishi wangependa kufika ziwa Tanganyika na kuona samaki hao wanatoaje umeme na kwamba aina hiyo ya samaki haipatikani katika maziwa mengine duniani zaidi ya ziwa Tanganyika.

Baadhi ya watalii wanapenda kujifunza maisha ya viumbe wa majini akiwemo samaki huyo anayetoa umeme hivyo wanapopata fursa ya kufika katika maziwa  kama ziwa Tanganyika wangependa kufanya utafiti wa aina mbalimbali za samaki na kufahamu aina na tabia za samaki.

HTop of Form
ata hivyo utafiti wa kimataifa ambao umefanyika mwezi Aprili mwaka huu na nerouetholojist Erick Fortune kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins cha  nchini Marekani unaonesha kuwa samaki hao wana uwezo wa kutoa umeme  kwa kutumia ogani umeme iliyopo kwenye mikia ya samaki hao.

 Utafiti huo unaonesha kuwa samaki huyo anaweza kutumia umeme unaozalishwa mwilini mwake  kwenye mawindo yake na kwamba umeme unaozalishwa na samaki huo ni kidogo na hauwezi kuleta madhara yeyote na kwamba samaki umeme ni wa kipekee na wanavutia watu wengi ambao wanapenda kwenda kufanya uchunguzi zaidi.

Mtafiti huyo anasema katika utafiti kuhusiana na samaki wanaotoa umeme aliweza kujifunza tabia za samaki hao baada ya kufanya majaribio na kuweka vifaa  katika makazi yao ya asili majini ambapo aliweza kusikiliza na kurekodi maisha yao,wanavyoweza kuwasiliana na viumbe wengine kwa kutumia ogani ya umeme,kupata hisia na namna wanavyoweza kujipatia chakula chao kwenye mazingira wanayoishi majini.

Utafiti wa Chuo Kikuu cha Johns Hopkins uliofanyika kwa msaada wa mfuko wa Taifa wa Sayansi (NSF) ulioongozwa na injinia Nuhu Cowan umewezesha  kujifunza zaidi kuhusu jinsi samaki umeme wanavyoweza kufanyakazi ya kudhibiti tabia zao na mazingira yao majini.

"Katika utafiti wetu tumefanya majaribio katika maabara kuhusu samaki wanaotoa umeme  hata hivyo uchunguzi unatakiwa kufanyika zaidi ili kutuwezesha kujibu maswali maalum ya kisanyasi kwa kuwa Watafiti tunataka kuelewa vizuri jinsi samaki hawa wanavyoweza kutoa umeme kwa kutumia sense organs za umeme zilizopo mkiani ambazo zinawawezesha kuwasiliana  na wenzao,kutawala mazingira yao na kupata chakula chao majini, "anaelezea Cowan wa NSF.

Utafiti unaonesha kuwa kwenye mkia wa samaki huyo kuna kiungo kidogo ambacho kinahusika na kuzalisha umeme na kwamba kiungo hicho kinapita hadi juu ya magamba au ngozi ya samaki huyo na kutoa umeme kila anapohisi kuna hatari,au anapotaka kuwasiliana na wengine na anapokuwa kwenye mawindo kwa ajili ya chakula.
   
“Samaki umeme anaweza kutoa umeme katika baadhi ya matukio, mabadiliko, ishara na mawasiliano, samaki umeme  wawili wa kike na wa kiume wanatoa umeme wanapoanza kujamiiana anasisitiza mwanasayansi Cowan katika utafiti wake.

watafiti pia wanataka kujifunza kile kinachotokea wakati samaki umeme zaidi ya wawili wanapokutana  pamoja na kujifunza kutokana na samaki umeme kutegemea organ ya umeme zaidi ukilinganisha na  sense ogani nyingine tano za mwili zikiwemo macho,mapezi,masikio,magamba na pua anasema Elizabeth Cropper, mkurugenzi wa programu ya Biolojia  ya NSF  ilifadhili utafiti huo.

Anabainisha zaidi kuwa samaki umeme kwa kutumia ogani ya umeme kwenye mkia wake inamwezesha kufanya mambo mengi zaidi kama vile kuogelea mbele,nyuma na kufanya mzunguko wa haraka majini,kuwasiliana,kuhisi na kula kuliko kutegemea maono katika sense organ nyingine tano.

Ukiachia samaki huyo anayetoa umeme,ziwa Tanganyika pia lina aina nyingine za samaki wakiwemo dagaa maarufu wa kigoma.Katika miji ya Kigoma na Sumbawanga  wakazi katika miji hiyo wanafanya biashara ya dagaa hao wanaovuliwa katika ziwa Tanganyika.

Biashara ya dagaa kutoka ziwa hilo endapo itaboreshwa  na wadau wake kujipanga vizuri dagaa hao wanaweza kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi na kuinua maendeleo yao kiuchumi.

Hata hivyo baadhi ya wakazi katika miji hiyo wanapeleka dagaa hao katika nchi za jirani ikwemo Kongo DRC,Burundi na Zambia katika kiwango ambacho hakitoi mapato makubwa.

Mhifadhi wa ziwa Tanganyika anatoa wito kwa serikali kutoa fursa kwa wawekezaji kuwekeza katika ziwa hilo kwa kujenga viwanda vya kusindika dagaa ili hatimaye dagaa hao waweze kupelekwa kuuzwa nje ya nchi katika viwango vya kimataifa ili kutoa faida kubwa zaidi .

Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Rukwa Injinia Stella Manyanya ameshauri  kuimarisha ushirikiano baina ya nchi jirani za Kongo DRC , Burundi na Tanzania ili kulifanya ziwa Tanganyika kuwa na matumizi endelevu kwa kuwa ziwa hilo limezungukwa na nchi hizo na lina utajiri wa maliasili ambazo ni urithi wa Taifa.

Ameshauri mabalozi katika nchi hizo wasaidia kuunganisha utalii kutoka katika nchi zote sanjari na kuboresha mazingira ya ziwa Tanganyika ili kuwalinda viumbehai waliomo ndani ya ziwa ziwa hilo wakiwemo samaki.

Hata hivyo uchunguzi umebaini kuwa kina cha ziwa Tanganyika kinapungua mwaka hadi mwaka kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira  ambao unaendelea kufanywa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.

“ Watu wanakata miti ovyo kwenye hifadhi ya ziwa Tanganyika,vyanzo vya maji vinavyotiririka kuelekea kwenye ziwa hilo vimeharibiwa katika kiwango kinachotisha hivyo kuathiri ziwa hilo ambalo ni muhimu kwa uchumi wa Taifa’’anasisitiza mhifadhi wa ziwa hilo Leonia Mnyonga.

Anashauri wadau wote wa mazingira katika nchi zinazozunguka ziwa Tanganyika kuungana kwa pamoja katika kulinda mazingira ya ziwa Tanganyika hasa kuhamasisha kupanda miti katika maeneo mbalimbali hivyo kufanya ziwa Tanganyika kuwa endelevu.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129.


No comments:

Post a Comment