Tuesday, August 21, 2012

Mwandishi asiyeona afanyiwa harambee


Na Albano Midelo
WAANDISHI wa habari kanda ya kusini wamemchangia mwandishi mwenye ulemavu wa macho Musa Chilungo zaidi ya shilingi 340,000.

Kiasi hicho cha fedha kilipatikana katika harambee iliyoongozwa na mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya Christopher Nyenyembe kwenye ukumbi wa chuo kikuu cha Ruaha mjini Iringa.

Waandishi wa habari  zaidi ya 150 kutoka mikoa ya Mbeya,Iringa,Ruvuma,Lindi,Mtwara,Katavi,Rukwa na Njombe walikuwa wanapata mafunzo ya siku mbili ya sensa ya watu na makazi  itakayofanyika usiku wa kuamkia Agosti 26,2012 nchini kote.

Katika mafunzo hayo  yalioendeshwa na ofisi ya Taifa  ya takwimu wanahabari walijifunza umuhimu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012,maeneo ya kuhesabia watu,maswali ya sense,sheria ya takwimu na wajibu na majukumu ya vyombo vya habari katika kufanikisha sensa ya watu na makazi.

Nyenyembe ambaye alikuwa mwenyekiti wa mafunzo hayo aliwafahamisha wanahabari kuhusu ulemavu wa macho aliopata mwandishi Chilungo ambaye hivi sasa ni mtangazaji wa kituo cha redio cha Ruangwa FM kilichopo wilayani Ruangwa mkoani Lindi.
“Ndugu zangu wanahabari Musa Chilungo nimefanya naye kazi kwa miaka mingi akiwa hana ulemavu,sisi wote ni walemavu watarajiwa naomba tumchangie mwenzetu kwa kuanza mimi namchangia shilingi 20,000’’,alisisitiza Nyenyembe.
Chilungo alipata ugonjwa wa macho na hatimaye kupata ulemavu wa macho na kushindwa kuona tena tangu mwaka 2007 na kwamba kabla ya mwaka 2006 wakati akiwa anaona alikuwa mwandishi wa magazeti ya serikali za mitaa( ALAT).
Mwandishi huyo mkongwe ambaye pia kitaaluma ni mwalimu anasema kutokana na kupata ulemavu wa macho mwaka 2010 alistaafishwa kufanyakazi serikalini ambapo hivi  sasa anaishi maisha ya kubangaiza kwa kuwa ana familia ambayo inamtegemea kwa kila kitu.
“ licha ya kwamba naendelea kufanyakazi ya utangazaji katika kituo cha redio ya Halmashauri ya Ruangwa napata posho tu,hali ni ngumu tangu nilipoachishwa kazi  ya ualimu mwaka 2010 kutokana na ulemavu wa macho,watoto wangu wanasoma fedha zinahitajika kwa ujumla maisha yangu hivi sasa ni magumu’’,alisisitiza.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:

Post a Comment