|
Kauli
hiyo ya Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na
Usalama imekuja siku chache baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe kuitaka Serikali ya Malawi kusitisha utafiti wa gesi
na mafuta unaofanywa kwa ndege juu ya ziwa hilo.
Baada
ya Membe kutoa onyo hilo, aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza katika serikali ya
awamu ya nne inayoongozwa na Rais Kikwete, Edward Lowassa alisema wakati
Bunge la Bajeti lilipokuwa likiendelea na vikao vyake mjini Dodoma kwamba,
jeshi lipo tayari kuingia vitani na Malawi, endapo nchi hiyo itakaidi agizo
la kuziondoa ndege zinazofanya utafiti kwenye anga la Ziwa Nyasa.
Kikwete
awakata maini
Katika
kile kinachotafsiriwa na wachambuzi wa musuala ya siasa kuzikana kauli za
Membe na Lowassa, Rais Kikwete alimhakikisha Rais Joyce Banda wa Malawi,
kwamba Tanzania haina mpango wa kuingia vitani dhidi yao, na kusisitiza kuwa
hizo ni chokochoko za wanasiasa na waandishi wa habari.
Rais
Kikwete aliyekuwa kwenye mazungumzo na Rais Banda wakati wa kikao cha
viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliomalizika jana
jioni nchini Msumbiji, aliwataka Wamalawi kuondokana na hofu ya vita.
“Nanakuhakikishia
dada yangu na watu wote wa Malawi, kwamba hatuna nia wala mpango wa kuingia
vitani… hatuna matayarisho ya jeshi wala jeshi halijasogea popote kwani
hakuna sababu.
“Mimi
ndiye kamanda mkuu wa majeshi, na sijapanga wala kutoa maelekezo ya vita,
tuviachie vyombo vyetu vifanye kazi. Hebu tuvipe nafasi. Wanasiasa na
waandishi wa habari wajiepushe na maneno yanayosababisha taharuki na
chokochoko, hayana maana… waachie diplomasia ifanye kazi yake,” alisisitiza.
Rais
Kikwete alisema kumekuwa na sintofahamu ya muda mrefu kuhusu mpaka huo, huku
akibainisha kwamba maofisa wa Malawi na Tanzania wameanza kulizungumzia suala
hilo kwa nia ya kulitatua kwa amani.
Naye
Rais Banda alisema amefarijika baada ya kusikia kauli ya Rais Kikwete
iliyomhakikishia kwamba hakuna vita, huku akieleza kuwa tishio la vita
liliwasumbua wananchi wake na kuwaongezea mshikamano.
“Nimefarijika
sana, suala hili limetusumbua mpaka Wamalawi wote wakaungana bila kujali
tofauti zao… navishukuru vyombo vya habari vya Malawi kwa kuonesha uzalendo
na ukomavu katika suala hili,” alisema Rais Banda.
Rais
Kikwete na Banda walikutana jijini Maputo nchini Msumbiji kwenye kikao cha
viongozi SADC ambapo Tanzania ilichukua Uenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi
na Usalama.
Awali
nafasi iliyochukuliwa na Tanzania ilikuwa inashikwa na Afrika Kusini huku
Uenyekiti wa SADC ukichukuliwa na Msumbiji kutoka kwa Angola nafasi
watakazokuwa nazo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Kwa
mujibu wa Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi, Premi Kibanga, Rais Kikwete
alirejea nyumbani jana akitokea Msumbiji.
Tamko
la Membe na Lowassa
Wiki
mbili zilizopita, Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, ilisema majeshi ya
Tanzania yapo tayari kiakili na kivifaa ikibidi kuingia vitani kutokana na
mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Edward Lowassa alitoa kauli hiyo mkoani Dodoma, alipokuwa
akizungumza na waandishi na habari na kusisitiza kuwa Tanzania inaomba
isifike katika hatua hiyo, lakini ikibidi wanajeshi wetu wapo imara kutetea
mipaka ya nchi hadi tone lao la mwisho la damu.
“Jeshi
letu lipo tayari, na tumeridhika na utayari wao na ‘commitment’ yao. Sisi ni
moja ya jeshi lililojiandaa vizuri sana na miongoni mwa majeshi mazuri
duniani. Tunajivunia vijana wa Tanzania waliopo kwenye jeshi letu. Tupo imara
kiakili, vifaa vya kisasa,” alisema.
Alisema
kamati hiyo inaunga mkono kauli ya serikali iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, kwani ni sahihi inayoelezea
msimamo wa Tanzania kuhusu jambo hilo.
Lowassa
alisema kuwa wanategemea jambo hilo litamalizika kidiplomasia ndani kwa ndani
ama ikibidi kuomba msaada wa watu wengine kusuluhisha kwa kuwa Tanzania na
Malawi ni marafiki na ndugu.
“Watu
waliopo mipakani ni ndugu, tusingependa kufika mahali kutokuelewana mpaka
kuhusisha vyombo vya ulinzi na usalama, lakini kwa faida ya Watanzania
tumepewa maelezo ya jeshi letu, tumeridhika kwamba ikibidi jeshi letu
limejipanga vizuri sana.
“Watanzania
wasiwe na shaka yoyote, wanajeshi wamejipanga vizuri na kwa uhakika na kama
ilivyo ahadi yao, wapo tayari kulinda nchi yetu mpaka tone la mwisho la damu
yao,” alisema na kuongeza kuwa kama wabunge, nao wameridhika na maandalizi ya
jeshi, kwani wapo imara na timamu.
Alisema
serikali haitaki kufika huko, kwani wakati wa vita ya Uganda mwaka 1978,
wananchi waliumia na kwamba kama nchi, inafahamu athari za vita kiuchumi na
kwa maisha ya binadamu.
“Hatutaki
kufika huko kwani si jambo jema, ndiyo maana tunasema tumalize kwa njia ya
mashirikiano na kwa mazungumzo ya kidiplomasia ya mawaziri wanaohusika
ikishindikana tutafute msuluhishi,” alisema.
Mwaka
1978, Tanzania iliwahi kuingia katika vita na Uganda, baada ya aliyekuwa rais
wa nchi hiyo, Iddi Amin Dada, kuvamia sehemu ya Tanzania na kudai kuwa ni
yao.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe naye alitoa tamko
la serikali na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea kufanya utafiti wa mafuta
katika ziwa hilo kuondoka mara moja pamoja na Serikali ya Malawi kuheshimu
mazungumzo yaliyofikiwa. Alisisitiza eneo linalobishaniwa katika ziwa hilo
lipo Tanzania.
Alisema
pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuzipiga marufuku
ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano zilitua katika
eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali
ya Tanzania inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea na
shughuli za utafiti katika eneo hilo zisitishe mara moja…,” alisema Membe na
kuongeza kuwa, Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa
gharama yoyote.
Alisema
kwa kuzingatia nyaraka zilizotengenezwa na wakoloni wa Kiingereza mwaka 1928
na 1938, zinaonesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati.
Alisema
hoja ya Tanzania ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa kwa vile tatizo
kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwepo kati ya Cameroon na Nigeria.
CHANZO;TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment