|
MGOGORO
wa mpaka baina ya Malawi na Tanzania kwenye Ziwa Nyasa, umekuwapo tangu enzi
za ukoloni.
Wakoloni,
kwa nyakati tofauti, wamekuwa wakigawana ardhi na rasilimali za Afrika baada
ya mikikimikiki ya vita na mauaji yasiyozingatia uhuru, haki na usawa wa watu
wenye miliki yao!
Hivi
ndivyo walivyokuwa wakifanya wakoloni tangu 1884/1885 na baada ya kongamano
la kuigawa Afrika kwa utashi wa kibeberu.Afrika
iligawanywa na kumilikishwa kwa Wazungu. Watu wa Afrika walinyang’anywa
uhuru, utu na heshima yao na kufanywa watumwa kwenye ardhi yao.
Afrika
tunayoiona leo, iliwekewa mipaka na wakoloni.
Wakoloni
walijigawia maeneo kulingana na utashi wa nguvu zao za kijeshi na kimamlaka
katika kutawala na kuvuna rasilimali za Afrika.
Kwa
jinsi hiyo, uchambuzi huu unakuja baada ya kufukuta kwa vuta nikuvute juu ya
mgogoro wa mpaka baina ya Malawi na Tanzania katika Ziwa Nyasa.
Ubishi
wa mpaka baina ya nchi mbili jirani, unatokana na mkataba wa kikoloni
uliyoingiwa tarehe 1, Julai mwaka 1890 kati ya Uingereza na Ujerumani maarufu
kama Anglo-Germany Treaty.
Mkataba
huo unaainisha mpaka wa Malawi na Tanzania kwenye mwambao wa ziwa (mashariki
ya ziwa).
Kwa
kutumia kipengele cha mkataba huo; Malawi kwa upande wake inadai sehemu yote
ya ziwa ni eneo lake.
Kwa
upende mwingine, Tanzania inadai kwamba, “mpaka wa ziwani, yaani unaogawa
ziwa katikati baina ya nchi mbili, ndio mpaka halisi.”
Dhana
hizi mbili, zinazokinzana zimeshachukua sehemu kubwa ya mijadala ya
kidiplomasia tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa kwanza wa
Tanganyika/Tanzania) na Hastings Kamuzu Banda (Rais wa kwanza na wa maisha wa
Malawi).
Marais
hawa, kwa nyakati tofauti wamekuwa wakirushiana vijembe vya kisiasa juu ya umiliki
wa eneo hilo lenye maji mengi (nyassa/niassa, kwa lugha za wenyeji wa maeneo
hayo) na hata kwa zaidi ya miaka 50 sasa hakuna suluhisho la kudumu juu yake.
Haijalishi,
hata kama ilishindikana kupata suluhisho enzi zile, sasa ni wakati muafaka
suala hilo liwekwe tena mezani kwa utashi wa kisiasa ili kutafuta suluhuhisho
muafaka.
Utafiti
uliyofanywa na Kanali Fulgence S. Msafiri (wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania,
JWTZ) na kuwasilisha andiko la utetezi wake wa tasnifu kwenye Chuo Kikuu cha
Naval Postgraduate School (Monterey, California) Juni mwaka 2011, unaweza
kutumiwa kama msingi wa udadavuzi wa kadhia ya mgogoro baina ya Malawi na
Tanzania.
Nimeamua
kutumia tasnifu ya Afande Fulgence S. Msafiri kwa kuwa ni andiko lenye sura
ya kutafuta suluhisho la mgogoro huu kwa njia zenye manufaa kwa pande zote
zinazohusika bila ya kuingia kwenye songombingo za kivita mbazo huleta
madhara mengi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Vita
haiombwi; na ubabe ni ushamba! Kwa jinsi hiyo, nampongeza sana Afande
Fulgence S. Msafiri kwa kufanya utafiti uliopelekea kuandikwa kwa tasnifu ya
kitaaluma inayoweza kutumika kama nyenzo ya utatuzi wa mgogoro huu.
Afande
Msafiri (2011) anaandika kwamba matatizo ya kushindwa kupatikana kwa utatuzi
wa kudumu wa mgogoro wa mpaka baina ya nchi mbili (yaani, Malawi na Tanzania)
yanatokana na kufeli kwa (1) mawasiliano na (2) ushirikiano.
Mambo
haya mawili, yaani mawasiliano na ushirikiano baina ya nchi mbili zenye
mgogoro, ni muhimu katika kufanikisha upatikanaji wa suluhisho la mzozo wa
mpaka wa Ziwa Nyasa ambalo ni sehemu ya urithi wa Malawi na Tanzania.
Kushindikana
kwa mawasiliano kwa sehemu kubwa, kunatokana na taarifa za kihistoria,
kulilazimishwa na mfumo wa siasa zilizokuwa zikitumika na nchi hizi.
Enzi
za utawala wa Kamuzu Banda aliyedhaniwa kuwa “kibaraka” wa makaburu na
Mwalimu Nyerere aliyedhaniwa kuendesha siasa za ujamaa na kuwasaidia
wapinzani wa utawala wa Kamuzu Banda; nchi hizi mbili hazikuwa na mawasiliano
ya moja kwa moja.
Baada
ya mageuzi ya kisiasa yaliyoifanya Malawi kuchukua mkondo wa demokrasia ya
vyama vingi mwaka 1993 na ofisi ya rais wa Malawi kuingia kwenye siasa za
vuguvugu, suala la mpaka wa ndani ya ziwa haukupewa kipumbele ilhali kwa
nyakati tofauti kulikuwapo na rabsha na sintofahamu za hapa na pale baina ya
mamlaka za Malawi na Tanzania juu ya umiliki wa maji ya Ziwa Nyasa hali
iliyowahi kupelekea wavuvi wa Tanzania kusumbuliwa ziwani walipokuwa
wakiendesha shughuli za uvuvi na hali kama hiyo ilitokea kwa upande wa pili
(yaani, Tanzania).
Pamoja
na ukweli huu, hakukuwa na hatua za makusudi na za kimkakati katika
kuhakikisha kwamba mgogoro huo unafanyiwa kazi ya kidiplomasia kwa utashi wa
hali ya juu wa kisiasa kwa kuhusisha ngazi muafaka na zinazohusika katika
kufufua mawasiliano ya moja kwa moja na ushirikano utakaopelekea kupata
muafaka wa kudumu.
Mwaka
huu, na hususan kwenye Bunge la Bajeti la 2012/2013, suala la mgogoro wa
mpaka baina ya Malawi na Tanzania juu ya Ziwa Nyasa, umeibuka upya na hata
kupelekea mamlaka za Tanzania kutoa kauli ya utayari wa kwenda vitani kama
Malawi wangekaidi “amri halali” ya mamlaka halali za Tanzania.
Nadhani,
ni muafaka kuonesha hapa kwamba mizozo yote ya mipaka duniani aghalabu
hutokea baina ya pande mbili zenye masilahi kwenye eneo husika.
Kama
mfano, mwaka 1990 Saddam Hussein al-Tikrit aliyekuwa Rais wa Iraq, aliivamia
Kuwait kwa madai kwamba sehemu hiyo (yaani, Kuwait) ni jimbo la Iraq!
Ukweli
wa kihistoria na kistratejia, Kuwait ni nchi inayoaminika kuwa na kiwango
kikubwa cha mafuta yasiyochimbwa chini ya ardhi (huge untapped petroleum
reserve).
Vilevile,
Ethiopia na Eritrea (nchi iliyojitenga kutoka kwa Ethiopia) ziliingia mara
kadha wa kadha vitani kwa mgogoro wa mpaka.
Mifano
ni mingi, lakini mfano wa hivi karibuni ni wa muhimu zaidi.
Sudan
ya Kusini iliyojitenga kutoka Sudan (lililokuwa taifa la kwanza kwa ukubwa wa
eneo katika Afrika), ziliingia vitani kugombea eneo lenye utajiri mkubwa wa
mafuta la Abyei (lililopo mpakani baina ya nchi mbili zilizojitenga).
Kwa
ujumla, migogoro, mizozo na hata wakati mwingine mapambano baina ya nchi
zinazopakana imekuwa ikishuhudiwa duniani kutokana na kushindikana kwa
suluhisho la kisiasa juu ya mipaka ya nchi husika iliyowekwa na wakoloni au
kwa kushindwa kutafsiri au kuanisha mgawanyo wa uhuru, haki na adilifu wa
rasilimali zilizomo kwenye maeneo husika.
Tanzania
imekuwa na mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa kwa muda wa miongo mitano sasa!
Kwa
nini leo; na au kwa nini wakati huu?! Hili ni suala mhimu kwa wapembuzi
kujiuliza na kutafakari juu yake.
Nini
kilichopelekea serikali (kupitia mamlaka zinazohusika) kulipuka na kukaza
misuli ya macho juu ya sakati hili leo ilhali lilikuwapo miaka 50 iliyopita?
Nadhani,
ushahidi wa moja kwa moja unatosha kuonesha ni kwa nini. Malawi imeanza
utafiti wa gesi na mafuta kwenye eneo lenye mzozo na linalobishaniwa baina
yake na Tanzania.
Makampuni
matatu (ya kigeni) yalipewa leseni na serikali ya Malawi kufanya utafiti
kwenye eneo lenye mzozo.
Ushahidi
kutoka kwa wenyeji (upande wa Tanzania) wa meneo yanayobishaniwa wamekuwa
wakishuhidia harakati za watafiti kufanya kazi ya kuchunguza utajiri
(unaosemekana) wa mafuta na gesi kwenye maji ya Ziwa Nyasa upande wa
unaodaiwa wa Tanzania!
Suala
kubwa hapa, ni utajiri wa gesi na mafuta! Malawi, kama wanavyosema na
kuonesha kwenye vielelezo vya ramani za sasa na za kikoloni, wanadhani kwamba
Tanzania inawafanyia “hiana” na kuwaonea husda kwamba, “Ziwa Nyasa (wanaliita
Ziwa Malawi) ni mali yao waliyopewa na Mungu.”
Na
kwa jinsi hiyo, kufanya utafiti wa gesi na mafuta, ni haki yao; huku Tanzania
kwa upande wake ikidai kwamba, “mpaka wake na Malawi ni katikati ya ziwa na
rasilimali ya ziwa hilo, lazima itumike kwa mgawanyo unaozingatia uwiano wa
nusu kwa nusu ziwani.” Hapa ndipo penye songombingo inayozaa “vuta-n-kuvute”
ambayo kama haitashughulikiwa kwa hekima, busara na weledi nchi mbili
zinaweza kuingia vitani kwa kila moja kutaka kulinda “heshima na uhuru.”
Binafsi,
nakubali kwamba nchi yoyote iwayo, iwe ndogo au kubwa, inahitaji kulinda
heshima na uhuru wake! Isipokuwa, bila kujali itikadi za kimtazamo na au
kifalsafa, lazima tukubali pia kwamba, “hekima ni uhuru.”
Nchi
isiyotumia hekima katika kufanya maamuzi yenye taathira kiuchumi, kijamii na
kisiasa kwenye mawanda ya mawasiliano ya watu wa dunia na ushirikiano wa
kikanda na kidunia, haiwezi kuwa huru kwa vile itakuwa inajitenga na jamii ya
watu wengine wanaoishi kwa kutegemeana.
Hakuna
nchi inayoweza kuishi kama “kisiwa” kinachoelea kwenye maji yanayolindwa na
samaki wakali na wenye sumu huku watu wengine kutoka maeneo yanayozunguka
maji hayo wakizuiliwa kushirikiana na watu wa kisiwa husika!
Binadamu
ni kiumbe wa kijamii na kwa jinsi hiyo, ameumbwa awasiliane na watu wengine
na ashirikiane nao katika kuendesha maisha yake kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Nakumbuka,
wakati nikisoma darasa la sita (mwaka 1983), mwalimu wangu mmoja alinisimulia
kisa (alichokitafsiri kwa Kiswahili kutoka kwenye kitabu cha Kiingereza cha
darasa la sita wakati ule) cha Mkisi mmoja aliyevuka Ziwa Nyasa kwenda
kutafuta mbegu ya muhogo Nyasaland.
Nadhani
ni ukweli usiyokuwa na shaka kwamba, makabila anuai yanayozunguka Ziwa Nyasa
yanapatikana nchi zote zinazozunguka ziwa hili.
Jaribu
kuchukua hata mandhari ya pwani zake, upande wa mwambao wa Malawi na mwambao
wa Tanzania wananchi, wanaoishi maeneo hayo wanafanana kwa asili yao na
shughuli zao.
Mila
na desturi za Wanyasa, Wanyakyusa, Wayao, Wamatengo, Wangoni, Wanyanja,
Wanyiha na wengineo wanaounda makabila yanayozunguka Ziwa Nyasa, wana asili
inayofanana sana na hawawezi kutenganishwa na siasa.
Watu
wanaozunguka Ziwa Nyasa wanaishi kwa kulitegemea ziwa hilo tangu maji hayo
yalipojikusanya hapo baada ya nguvu za asili za dunia kutengeneza Bonde la
Ufa lililofanya bonde kuwapo mahala hapo!
Kwa
watu wanaozunguka ziwa hilo (Nyasa), wanalijua ziwa hili kama nyassa (au
niassa), ikiwa na maana eneo lenye maji mengi na hata wale waliyeitwa
wavumbuzi (waliowatangulia wakoloni) walipokuja na “kuvumbua, sema kuona mara
ya kwanza wakiwa Wazungu) waliwakuta watu wa makabila mbalimbali wakilitumia
ziwa kwa manufaa ya maisha yao kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Ziwa
Nyasa, kwa vyovyote vile ni mali ya watu wote wanaozunguka ziwa hilo na si
kinyume chake!
Hakuna;
narudia, hakuna anayeweza kuwanyang’anya watu wanaozunguka Ziwa Nyasa uhuru
na haki yao ya urithi wa asili.
Utashi
wa wakoloni na tamaa ya kuvuna rasilimali kunachochea tamaa na uchu
uliyopitiliza kwa baadhi ya wanasiasa wasiozingatia hekima na busara ya
kutawala siasa katika kutafuta ufumbuzi wa kudumu kwa kuzingatia mwasiliano
endelevu na ushirikano wenye tija na ufanisi kwa wale wote wanaohusika katika
kujenga mujtamaa wa maelewano yanayozingatia utu, heshima na uhuru ya kila
taifa linalohusika kwenye mzozo huu.
Kama
mfano, kwenye sakata jingine kama hili; Malawi ilipewa visiwa viwili vya
Likoma na Chisamula ambavyo vipo kwenye maji ya ziwa upande wa Msumbiji!
Nadhani,
kama isingalikuwa mawasiliano na ushirikano baina ya nchi hizo mbili, sidhani
kama hilo lingaliwezekana!
Hapana
shaka yoyote kwamba, hata kwa upande wa Malawi na Tanzania inawezekana.
Vita
si suluhisho la migogoro ya mipaka; japokuwa baadhi ya watu wanapenda vita!
Naandika hivi kwa kuwa kabla sijaamua kulijadili suala hili kwenye kurasa hii
ya “Mada ya Wiki” tayari mjadala huu ulishaanza kwenye mitandao ya kijamii
kama vile tweeter, facebook, jamiiforums, wanabidii, wanamabadiliko na kwenye
kurasa za maoni za magazeti ya kwenye mtandao.
Maoni
yanatofautiana; wapo wanaotamani mgogoro huu uishe kwa diplomasia na utatuzi
wa kisiasa, wapo wanaodhani kwamba njia muafaka ni kuiadabisha Malawi kwa
kuipiga kijeshi, na wapo wanaodhani kwamba suala hili liachwe kama lilivyo
kwa sasa kwa kuwa nchi ina matatizo mengi ya kiuchumi na kujiingiza kwenye
songombingo za kivita kunaweza kuliingiza taifa kwenye hamkani ya kisiasa
kama ilivyokuwa mwaka 1978 wakati wa Vita vya Kagera.
Kama
nilivyotangulia kuandika, nadhani suluhisho la Afande Fulgence S. Msafiri
(Juni, 2011), linaweza kuwa la kimkakati kama litachukuliwa na kufanyiwa
kazi.
Afande
Msafiri (2011) anaandika kwamba, mgogoro wa mpaka wa ziwani baina ya Malawi na
Tanzania, unaweza kutatuliwa kwa kuzingatia nukta nne (4) kama hivi: Malawi
na Tanzania wakutane na kujadiliana na waamue kutafuta suluhu ya mpaka baina
yao; nchi zote zifanye kazi kwa pamoja kutekeleza makubaliano ya uchoraji wa
mpaka (wa ziwani) kwa mujibu wa kanuni zinazotawala maeneo ya maji (maziwa na
mito) yanayozikutanisha nchi na nchi; kila nchi ichukue hatua za kuzuia
uharibifu wa maeneo oevu yanayolizunguka ziwa; na Malawi na Tanzania
zianzishe muundo wa ushirikiano utakaowezesha kuanzishwa kwa miradi ya pamoja
kama vile uzalishaji wa umeme unaotokana na nguvu ya maji na uvuvi.
Kwa
asilimia mia moja, nakubaliana na ushauri aliyoutoa Afande Fulgence S.
Msafiri (Juni, 2011) na kwa kuongezea ningeshauri yafuatayo katika kupata
muafaka wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. Tanzania na Malawi zikubaliane juu
ya: (1) kuanzisha kamati ya uratibu wa matumizi ya Ziwa Nyasa
itakayoshughulikia mawasiliano na ushirikiano wa kirafiki baina ya serikali
ya Tanzania na Malawi; (2) Tanzania na Malawi zikubali kuanzisha mamlaka ya
bonde la Ziwa Nyasa kwa ngazi ya mikoa inayozunguka ziwa na kuipa mamlaka
hiyo wajibu wa kuangalia mgawanyo wa rasilimali za ziwa; na (3) Tanzania na
Malawi kwa kupitia kamati za ushirikiano wa kikanda, waanzishe taasisi ya
uendelezaji ujirani mwema baina ya makabila yanayozunguka Ziwa Nyasa ambayo
kihistoria, ni watu wanaofanana kwa mila na dasturi zao.
Mwisho,
napenda kutofautiana na wale wanaodhani kwamba njia pekee ya kutatua mgogoro
huu, ni vita!
Kwa
kuwa hata nguli wa falsafa ya vita Sun Tzu kwenye kitabu chake cha “The Art
of War,” ametahadharisha kwamba, “Generali wa vita anaweza kushinda bila ya
kumwaga damu.”
Nadhani
ni muafaka, na kwa ujumla, nakubaliana moja kwa moja na Sun Tzu na Afande
Fulgence S. Msafiri kwamba, “Tanzania na Malawi wanaweza kumaliza mgogoro wa
mpaka kwa njia ya amani na mazungumzo ya kisiasa bila ya kumwaga damu ya
wananchi wa pande mbili na kuepusha hasara za kiuchumi, kijamii na kisiasa.”
Vita
haviombwi; na ubabe ni ushamba, tutumie vema siasa tumalize migogoro yetu kwa
utumizi wa hekima, busara ya hali ya juu na kwa kuzingatia uhuru, haki na
uadilifu.
CHANZO;TANZANIA
DAIMA
|
Binafsi, nilipenda kujua ni akina nani ambao Tanzania inawapeleka Malawi kujadiliana kuhusu suala hili. Afande Msafiri ni muhimu awemo katika ujumbe huu, kwani amefanya utafiti kuhusu suala husika. Ningependa kujua waliomo wana uzoefu au ujuzi gani na suala hili, vinginevyo nitasema Tanzania tunafanya mchezo. Kwamba tunafanya mchezo imejidhihirisha pia katika kauli za wale walioongelea vita.
ReplyDeleteNi upuuzi kwa nchi kushindwa kuelewa kuwa suala kama hili la mpaka Ziwa Nyasa, ambalo lina historia ndefu, nyaraka na vielelezo mbali mbali, na pia lenye kugusa sheria mbali mbali, linahitaji utafiti, tafakari na busara, sio kutunisha misuli.