Na Albano Midelo
KITENGO cha walemavu
wasioona Luhira katika Halmashauri ya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,ndiyo
kitengo pekee kwa ajili ya wasioona ukanda wa kusini .
Kitengo hicho ambacho
ni ukombozi kwa watoto wasioona nchini kilianzishwa mwaka 1982,hata hivyo shule
ya msingi Luhira ni miongoni mwa shule kongwe nchini ilianzishwa mwaka
1929,waziri mkuu wa kwanza wa Tanzania hayati Rashid Kawawa amepata elimu yake
ya msingi katika shule hii.
Mkuu wa kitengo cha
shule ya wasioona Luhira ambaye pia ni mlemavu wa macho mwalimu Salum Hapendeki
anasema kitengo hicho kina wanafunzi 40 wasioona kati yao wavulana ni 20 na
wasichana ni 20 na kwamba uwezo wa kitengo hicho ni kuchukua wanafunzi wasioona
60.
“Tunashindwa kuchukua
wanafunzi 60 wasioona kutokana na shule yetu ambayo ni ya bweni inakabiliwa na
upungufu mkubwa wa vitanda na magodolo,katika mkoa wa Ruvuma pekee kuna watoto
wengi wasioona wenye umri wa kwenda shule ambao hawasomi,kwa mfano tulipata
maombi ya watoto 14 kutoka Tunduru ili wafike kusoma hapa tumeshindwa
kuwachukua tutawalaza wapi?’’,alihoji Hapendeki.
Hata hivyo Hapendeki
anaishukuru wizara ya TAMISEMI ambayo inatoa fedha kila mwaka katika
Halmashauri ya manispaa ya Songea kwa ajili ya kuendeshea elimu maalum ambapo
shule yake inanufaika kila mwezi kwa kupata fedha za chakula,usafiri na vifaa vya kujifunzia na
kufundishia.
“TAMISEMI kupitia
Halmashauri ya manispaa ya Songea pamoja na wadau wengine wa elimu kama vile
Mamlaka ya Elimu Tanzania TEA inatoa fedha na vifaa kwa mfano katika shule yetu
tumepewa fimbo nyeupe za kuongezea wasioona na mashine maalum ya photocopy aina
ya thermoform kwa ajili ya wasioona yenye thamani ya shilingi milioni 18
inatusaidia sana’’,alisisitiza.
Hata hivyo mkuu huyo wa
kitengo cha wasioona anasema rim ambazo zinatumika kwa ajili ya photocopy
katika mashine hiyo ni rim maalum kwa ajili ya wasioona ambazo zinapatikana
jijini Dar es salaam pekee kwa shilingi laki tatu bei ambayo ni kubwa
ukilinganisha na rim za karatasi za kawaida.
Changamoto nyingine
ambazo zinakikabili kitengo hicho ni ukosefu wa umeme wa uhakika hali ambayo
inahatarisha usalama wa watoto hao pamoja na walimu kushindwa kutumia vifaa vya
kufundishia na kujifunzia vinavyotumia umeme hivyo kuchangia kushusha elimu kwa
watoto wenye ulemavu.
Changamoto nyingine
ni shule hiyo kukosa uzio hali inayosababisha watu wasiohusika wakiwemo
waharifu kuingia,upungufu wa mashine za kuandikia aina ya braili na shule kukosa mazingira rafiki ya wenye
ulemavu wasioona.
Baadhi ya wanafunzi
wenye ulemavu wameiomba serikali kuhakikisha kuwa inatoa kipaumbele cha
kupatiwa nishati ya umeme wakati wote ili waweze kupata elimu bora na
kusisitiza kuwa kwao elimu bora ni jicho hivyo ni lazima waipate.
Langson Mtega
mwalimu mlemavu asiyeona anasisitiza kuwa katika mkoa wa Ruvuma kuna idadi
kubwa ya watoto wasioona ambao hawasomi hata hivyo walemavu hao wamekosa
msaada wa kufikishwa katika shule hiyo ili kupata elimu ambayo ni ukombozi
katika maisha yao.
Kulingana na
Mtega changamoto zinazoikabili shule hiyo ya wasioona ni pamoja na uchakavu
na upungufu wa vifaa vya kufundishia kwa walemavu hao zikiwemo Braili za
kuandikia walemavu hao hali inayoathiri utoaji wa elimu bora kwa walemavu
hao.
Aliitaja
changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa nishati ya umeme katika shule hiyo
hali inayosababisha vifaa vingi vya kufundishia vinavyotumia umeme kushindwa
kutumika.
“Hatuelewi kwanini
shirika la ugavi wa umeme nchini TANESCO mkoani Ruvuma linashindwa kutupatia
huduma ya nishati ya umeme wa uhakika na kuaminika kutokana na umuhimu wa
umeme kwa wenye ulemavu wasioona’’,alisema.
Pamoja na changamoto zinazokikabili kitengo
hicho,kitaaluma kila mwaka wanafunzi wasioona wanamudu kufanya vizuri mtihani
wa Taifa wa darasa la saba kwa mfano mwaka juzi kati ya wanafunzi watano
waliofanya mtihani wanafunzi wanne walifaulu na kuchaguliwa kuendelea na
masomo ya sekondari na mwaka jana kati ya wanafunzi wawili waliofanya mtihani wote walichaguliwa
kuendelea na elimu ya sekondari.
Ulemavu wa macho
unatokana na magonjwa ya macho ambayo
hapa nchini yanatishia ustawi wa jamii kutokana na takwimu kuonesha kuwa
idadi ya wagonjwa wenye matatizo ya kutoona na uoni hafifu kuongezeka kwa
kasi kubwa.
Kwa mujibu wa
takwimu za shirika la Afya Duniani Tanzania inakadiriwa kuwa na watu 450,000 wasioona na
wengine takriban 1,350,000 wana uoni
hafifu.
Kulingana na
takwimu hizo duniani kote inakadiriwa kuna takriban watu milioni 30 wenye
matatizo ya kutoona na wengine watu milioni 90 wana uoni hafifu.
Kaimu meneja wa mpango wa Taifa wa huduma za
macho Dk.Bernadetha Shilio anabainisha kuwa serikali kupitia wizara ya Afya
na ustawi wa Jamii imeridhia dira ya mwaka 2020 ya kutokomeza upofu unaoweza
kuzuilika ulimwenguni ifikapo mwaka 2020.
Kwa upande wake
Dk.Hassan Rumbe anabainisha sababu zinazosababisha upofu kuwa ni pamoja na mtoto wa jicho unaosababisha kwa
asilimia 50,kovu kwenye kioo cha jicho inayosababishwa na trakoma,upungufu wa
vitamin A na surua inasababisha upofu kwa asilimia 20.
Magonjwa mengine ambayo
yanasababisha upofu ni magonjwa ya retina kama vile kisukari,umri mkubwa na
kwamba mambo yanayosababisha kutoona kwa watoto ni makengeza,upeo mdogo wa kuona,mtoto wa
jicho,maambukizi yatokanayo na magonjwa ya ngono toka kwa mama na matatizo ya macho ya kuzaliwa nayo.
Hata hivyo cha watu
wasioona nchini wametoa rai kwa serikali kuacha tabia iliyozoeleka ya kutumia
mabomu ya machozi kwenye maandamano au mikusanyiko ya watu kwa kuwa mabomu
hayo yanachangia kuongeza idadi watu
wasioona au wenye uoni hafifu.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129
|

No comments:
Post a Comment