Julai 30 mwaka huu, serikali
ililifungia gazeti la MwanaHalisi kwa muda usiojulikana, kwa kile
kilichoelezwa kuwa ni kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala
za uchozezi.
Wakizungumza na gazeti hili, kwa nyakati tofauti, maaskofu hao walisema kuwa, hatua ya kufungia
vyombo vya habari haioneshi taswira njema na haikubaliki kwa jamii
iliyojengwa katika misingi ya demokrasia.
Askofu Benson Bagonza wa Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, alisema kuwa hatua
ya kukifungia chombo cha habari inaashiria wazi kuwa serikali haipo tayari
kupokea taarifa zinazotolewa na jamii.
“Hali hiyo imetupa shaka hata sisi
maaskofu, kwani ni wazi kuwa wanaweza kutunyamazisha hata viongozi wa dini
iwapo tutakuwa tukiwakosoa,” alisema.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa
Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk. Valentino Mokiwa, alisikitishwa na kitendo
hicho na kusema kuwa jambo hilo limeathiri jamii nzima.
Alisema kuwa taarifa zilizokuwa
zikitolewa na gazeti hilo ziliwasaidia katika kukaa na kulikomboa taifa na
hata wakati mwingine kuweza kuishauri serikali.
Dk. Mokiwa, alisema, kuzuiwa kwa
chombo hicho kumewanyima fursa ya kujua sehemu ya kusimamia na hata jinsi ya
kuisadia serikali ili iweze kuenda katika mstari unaotakiwa.
“Tumesikitika sana maana gazeti
hilo lilikuwa ni msaada mkubwa kwetu sisi viongozi wa dini, ni muhimu
kukubali kukosolewa na jamii kwani kukubali kusifiwa pekee ni kubaya, maana
hiyo ni sawa na methali ya unapakwa mafuta kwa mgongo wa chupa,” alisema.
Naye, Katibu Mkuu wa Baraza la
Maaskofu Tanzania (TEC), Antony Makunde, alisema kuwa, serikali haikupaswa
kuchukua uamuzi huo bali ingekaa na gazeti hilo na kushauriana.
Hata hivyo, alivitaka vyombo vya
habari kuhakikisha vinazingatia misingi ya uandishi ili kuepuka kutokea kwa
migogoro inayoweza kuhatarisha amani nchini.
Kwa mujibu wa serikali, sababu
nyingine iliyosababisha kufungiwa gazeti hilo ni pamoja na kujenga uhasama na
uzushi, likiwa na nia ya kusababisha wananchi wakose imani na vyombo vya
dola, hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa nchi.
CHANZO TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment