Wednesday, August 8, 2012

Mt.Vinsent shule ya wenye ulemavu inayoongoza kitaaluma

Na Albano Midelo
 Hakuna ubishi jamii bado haijaonesha dhahiri nia ya kulisaidia kundi la wenye ulemavu ambapo hata idadi ya shule kwa ajili ya wenye ulemavu ni chache ukilinganisha na idadi ya shule za msingi na sekondari ambazo zinajengwa kwa ajili ya watu wasiokuwa na ulemavu.
 Takwimu kutoka Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma zilizotolewa hivi karibuni zinaonesha kuwa  wilaya nzima ina shule moja tu ya wenye ulemavu huku  watoto wenye ulemavu 71  wenye umri wa kuanza shule katika wilaya  hiyo hawasomi kutokana na  ukosefu wa shule za wenye walemavu.
 Mchango wa madhehebu ya dini katika kuhakikisha  watu wenye walemavu wanapata elimu ni jambo ambalo linafaa kuungwa mkono na serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa shule hizo ambazo zimeanzishwa  zinapata mahitaji yote muhimu wakiwemo walimu waliopata mafunzo ya kufundisha watu wenye walemavu pamoja na  na vifaa vyote muhimu vya kufundishia na kujifunzia.
  Miongoni mwa shule ambazo zinatoa mchango mkubwa kwa walemavu hapa nchini ni Shule  ya msingi  ya mtakatifu vinsenti  iliyopo katika Halmashuri ya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambayo  inahudumia watoto wenye ulemavu katika kundi la viziwi ambao wana mahitaji maalum kama ilivyo katika makundi mengine ya walemavu.
  Mkuu wa shule hiyo Sr. Anna Mgaya anabainisha kuwa shule ya St.Vinsenti awali ilianzishwa mwaka 1984 na kanisa katoliki jimbo la Mbinga baada ya kufanyika maafikiano kati ya kanisa na serikali.
 Shule hiyo yenye mazingira mazuri ya kusomea inahudumia walemavu viziwi kutoka mikoa ya Ruvuma,Lindi,Mtwara,Mbeya,Rukwa,Iringa na baadhi ya wanafunzi wanatoka jijini Dar es salaam.
 “Makubaliano ya kuanzisha shule hii yalifanyika baada ya kufanyika utafiti na kugundulika kuwa wapo watoto wengi viziwi katika kanda ya kusini ambao wanakosa nafasi ya shule baada ya ukanda mzima wa kusini kutokuwepo kwa shule ya walemavu viziwi”,anasema Mgaya.
  Uongozi wa kanisa katoliki ukishirikiana na shirika la watawa wa mtakatifu Vinsenti wa Paulo Mbinga walifanikiwa kupata wafadhili kutoka nchini Ujerumani kupitia chama cha misaada cha MISERIOR ambao walikubali kugharamia ujenzi wa shule hiyo ya walemavu viziwi kuwa Songea.
  Shule ya mtakatifu Vinsentu ilipata usajili Januari 15,1989 na kupewa namba RV/01/02/033 ambapo ilifunguliwa  rasmi na waziri mkuu mstaafu  hayati Rashid Mfaume Kawawa Februari 2,1992.
 Kulingana na Sr.Mgaya shule hiyo  ina uwezo wa kupokea wanafunzi 200 tu na kwamba kutokana na hali hiyo Kila mwaka watoto walemavu viziwi wengi wanakosa nafasi ya kujiunga katika shule hiyo kutokana na shule kukosa uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi zaidi ya hao.
“Idadi ya wanafunzi waliopo hivi sasa katika shule yetu ni 139 kati yao wavulana ni  74 na wasichana ni 65,ambao wanasoma kuanzia  shule ya awali hadi darasa la saba, shule pia ina kitengo cha ufundi katika fani za useremala na ushonaji, kuna kitengo cha ushauri nasaha,upimaji na utengenezaji wa shime sikio,anasema.
 Ameyataja mafanikio ya kuridhisha yaliopatikana tangu kuanzishwa kwa shule hiyo katika nyanja mbalimbali kuwa ni pamoja na  shule kujitosheleza katika majengo na samani,vifaa vya kujifunzia na kufundishia mazingira mazuri ya kujisomea na nyumba za walimu zinazokidhi mahitaji ya walimu.
 Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule,ufaulu wa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba kila mwaka unaridhisha kwa mfano  mwaka 2008 waliohitimu walikuwa 13 waliofaulu ni 13  na mwaka 2010 waliohitimu walikuwa 19 na wote 19 walifaulu kwenda sekondari.
 Hata hivyo Sr.Mgaya anasema  shule hiyo inaendeshwa kwa fedha za serikali katika chakula,usafiri,vifaa vya madarasani licha ya fedha zinazotolewa kutokidhi mahitaji halisi ya uendeshaji wa shule hiyo.
  Anasema Kitengo  cha ufundi katika shule hiyo,  kinatoa mafunzo ya awali katika fani za useremala na ushonaji na kufanya mitihani ya VETA na kupewa  vyeti vya ufundi.
Changamoto zinazoikabili shule hiyo kwa mujibu wa mkuu wa shule ni pamoja na  upungufu wa walimu kulingana na ikama ya walimu wa walemavu,upungufu mkubwa wa watumishi wasiokuwa walimu,ruzuku inayotolewa katika shule haitoshelezi mahitaji na upungufu wa maji kutokana na uhaba wa visima.
 “ Changamoto nyingine kubwa ni ukosefu wa umeme wa uhakika hasa wakati wa usiku,nishati ya umeme wakati wa usiku ni muhimu sana kwa walemavu viziwi wanategemea sana mwanga kwa ajili ya mawasiliano,utafiti unaonesha  kuwa wakati wa usiku  bila mwanga unakuwa umekata mawasiliano kwa walemavu viziwi  hivyo kuhatarisha maisha yao”,anasisitiza.
 Hata hivyo anasema shule hiyo ina watoto 46  wanaoishi katika mazingira magumu kati ya hao 26 ni watoto yatima ambao hawana msaada wowote hivyo ametoa wito kwa mashirika binafsi,serikali na wafadhili kuangalia  uwezekano wa kuitambua shule hiyo kuwa kuwa kituo rasmi chenye watoto yatima.
Matarajio ya shule hiyo ni kuanzisha darasa la kompyuta kwa ajili ya watoto hao walemavu kujifunza somo la kompyuta ili kuendana na ulimwengu wa sayansi na teknolojia ambao unategemea teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA na kwamba tayari kompyuta zimefungwa katika chumba kimoja cha darasa. .
 Sr. Mgaya anabainisha zaidi kuwa walemavu viziwi wana uwezo mkubwa katika masomo ya vitendo hivyo wanaweza kufanya vizuri sana katika somo hilo kama ilivyo katika fani ya ufundi ambapo wanafunzi hao wana uwezo wa hali ya juu.














  

No comments:

Post a Comment