|
SERIKALI imesema eneo linalogombewa na Malawi katika Ziwa Nyasa ni mali ya
Tanzania na sasa imeziamuru kampuni za nchi hiyo zinazofanya utafiti wa
mafuta kuondoka eneo hilo kuanzia jana.
Onyo hilo dhidi ya Malawi lilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye pia amesisitiza kuwa Tanzania
itakuwa tayari dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama.
Hii ni mara ya pili Serikali kuionya Malawi katika mgogoro huo. Wiki
iliyopita aliyekuwa Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni Samuel
Sitta alisema: “Tuko tayari kwa lolote dhidi ya Malawi.”
Sitta alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu Swali la Mbunge wa Mbozi Mashariki,
Godfrey Zambi aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu mgogoro huo.
Jana, akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka
2012/13, bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe alisisitiza kwamba eneo linalobishaniwa katika ziwa
hilo lipo Tanzania.
Alisema pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuzipiga
marufuku ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano
zilitua katika eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali ya Tanzania inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote
zinazoendelea na shughuli za utafiti katika eneo hilo zisitishe mara moja
kuanzia leo (jana),” alisema Membe.Alisema Serikali ya Tanzania iko tayari
kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote na haitaruhusu utafiti huo wa
uchimbaji wa gesi na mafuta uendelee.
Alisema chini ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), wananchi wa Tanzania
watakuwa salama dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama.
Kiini cha Mgogoro
Kuhusu kiini cha mgogoro, Waziri Membe huku akirejea historia ya mipaka tangu
ukoloni, alisema ni hatua ya Serikali ya Malawi kushikilia msimamo kuwa eneo
lote la Ziwa Nyasa lipo Malawi wakati Tanzania inashikilia kuwa mpaka upo
katikati ya Ziwa.
“Wenzetu wanadai ziwa lote lipo Malawi lakini, nyaraka zilizotengenezwa na
wakoloni wa Kiingereza mwaka 1928 na 1938 zinaonyesha kuwa mpaka wa ziwa hilo
upo katikati,” alisema.
Alisema hoja ya Tanzania ina nguvu kulingana na sheria za kimataifa kwa vile
tatizo kama hilo linafanana na mgogoro uliokuwepo baina ya Cameroon na
Nigeria.
Alisema katika kesi iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Dunia, iliamuliwa
kuwa mpaka baina ya nchi hizo mbili upite katikati ya Ziwa Chad ukifuata
msitari ulionyooka.
“Ni dhahiri, tunalo tatizo kati ya Tanzania na Malawi linalohitaji kutatuliwa
kuhusu mahali hasa ulipo mpaka baina ya nchi hizi mbili na lilianza tangu
enzi ya awamu ya kwanza,” alisema.
Waziri Membe alisema tatizo hilo lilishindwa kupatiwa ufumbuzi kutokana na
Rais Kamuzu Banda wakati huo akiwa madarakani kuamini kuwa ‘Tanzania ilikuwa
ni kichaka cha kuhifadhi maadui wa Serikali yake.’
“Baada ya mabadiliko ya uongozi, tulianza kujadili tatizo hilo kwa njia za
kidiplomasia na mwaka 2005 iliundwa tume ya pamoja ya kushughulikia mgogoro
huo,” alisema.
Alisema Rais Jakaya Kikwete alipoingia madarakani alikutana mara mbili na
Rais wa zamani wa Malawi, marehemu Bingu wa Mutharika na kukubaliana iundwe
Tume ya Pamoja ya wataalamu kushughulikia mgogoro huo.
Hata hivyo, alisema wakati tume hiyo ikianza kukusanya nyaraka mbalimbali,
suala hilo lilichukua sura mpya na kuanza kuhatarisha usalama wa Tanzania na
wananchi wake.
Alisema Serikali ilipata habari za kuaminika kupitia Shirika la Maendeleo ya
Petroli (TPDC) kuwa eneo lote la Ziwa Nyasa, kaskazini ya Msumbiji
limegawanywa katika vitalu mbalimbali.
“Kwamba Serikali ya Malawi ilitoa vitalu hivyo kwa kampuni za kutafuta mafuta
na gesi na yakaomba kibali cha kuruhusu ndege za utafiti ziruke katika anga
la Tanzania,” alisema.
Waziri Membe alisema ombi hilo lilikataliwa na JWTZ lakini, Serikali imepata
ushahidi kuwa ndege ndogo tano za utafiti zenye uwezo wa kutua ufukweni na
majini zilionekana zikivinjari na kutua Ziwa Nyasa upande
wa Tanzania Januari 29 na Julai 2 mwaka huu.
Alisema Serikali ya Tanzania iliwasiliana na Serikali ya Malawi kwa maandishi
na kuomba ufanyike mkutano wa mawaziri na wataalamu wa nchi mbili kuhusu
mustakabali wa mpaka wa nchi hizi mbili.
Mkutano huo ulifanyika Tanzania Julai mwaka huu na baada ya majadiliano,
pande zote mbili zilikubaliana kwa kauli moja kwamba lipo tatizo baada ya
kila upande kushikilia msimamo wake.
Alisema pande zote mbili zilikubaliana kuendelea na mazungumzo hayo Agosti 20
hadi 27 mwaka huu, nchini Malawi ukihusisha wataalamu wa mipaka na sheria za
kimataifa wa nchi hizo mbili.
“Katika mkutano huo, Serikali ya Tanzania iliitaka Malawi kutoruhusu mtu au
kampuni yoyote kuendelea na shughuli za utafiti na tunaonya hatutaruhusu
utafiti huo uendelee,” alisema.
Alisema Serikali inathamini uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kuitaka
Malawi kuheshimu makubaliano na kuongeza kwamba njia nzuri na bora ya kutatua
tatizo hilo ni ya mazungumzo ya amani.
“Katika kipindi chote cha mazungumzo Serikali ya Malawi isiruhusu shughuli
zozote za uchimbaji wa madini na mafuta katika eneo hilo kwa sababu ni eneo
la Tanzania,” alisema na kuongeza kuwa Serikali inayo dhamana ya kuwalinda
wananchi 600,000 wanaoishi na kutegemea Ziwa Nyasa.
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Gando (CUF), Khalifa Suleiman Khalifa
alisema tamko hilo la Waziri linaonyesha kwamba kilichopo sasa baina ya nchi
hizo ni kutunishiana misuli.
Alisema vita si suluhisho la mgogoro huo na kushauri kuwa iwapo Malawi
imeweka watafiti wa mafuta ziwani, Tanzania
nayo itafute wa kwake nao waanze kutafiti.
Alisema inavyoonekana mgogoro huo hauwezi kumalizika kwa mazungumzo
yanayofanyika Dar es Salaam, bali kufikishwa kwa wasuluhishi wa kimataifa,
The Hague.
Malawi yajibu mapigo
WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Malawi, Patrick Kabambe alikaririwa na Redio Sauti
ya Ujerumani jana jioni akisema kuwa wataendelea na utafutaji wa mafuta na
gesi katika Ziwa Malawi huku akidai kwamba amesikia Tanzania inapeleka askari
eneo hilo.
Waziri huyo alisema hilo ni Ziwa Malawi na siyo Nyasa na kueleza kuwa
utafutaji wa mafuta na gesi utaendelea na hakuna wa kuwasimamisha huku
akihoji Tanzania kuja juu sasa na si wakati mwingine.
“Tutaendelea kutafuta mafuta na gesi katika Ziwa Malawi na tunashangaa kwa
nini sasa ndiyo wanalalamika na siyo wakati mwingine?” alikaririwa akisema.
Nyongeza na Joseph Zablon
CHANZO MWANANCHI PUBLICATION
|
No comments:
Post a Comment