Saturday, August 4, 2012

Mkapa:Hatutatenda haki kutolishukuru kanisa hadharani


  
Na Albano Midelo
RAIS mstaafu Benjamin Mkapa anatamani kila Jumapili kusali katika kanisa kuu la mtakatifu Kilian la jimbo la Mbinga kutokana na kile alichoeleza kuwa  ni uzuri wa kuhamasisha na kumotisha uchaji  wa Mungu unaofanywa na kanisa hilo.
Rais mstaafu Mkapa alieleza vionjo vyake kuhusu kanisa hilo wakati anawahutubia maelfu ya waumini waliofurika katika maadhimisho ya Jubilei pacha jimboni Mbinga ambapo Rais mstaafu Mkapa alikuwa ni mgeni rasmi.
Akizungumza kwenye sherehe hizo ambazo zilihudhuriwa na maaskofu kutoka nchi nzima,mapadre,watawa viongozi wa serikali na mashirika,Rais mstaafu Mkapa alibainisha kuwa licha ya kusali katika kanisa hilo mara tatu bado hajakifu na anatamani kupata fursa zaidi za kufika kusali na kuabudu kila Jumapili.
Amelishukuru kanisa katoliki la Mbinga kwa kusaidia kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi hali ambayo imesababisha jimbo la Mbinga kupata mafanikio makubwa yaliyotukuka. 

“Kama sio kanisa,ukanda huu wa kusini ungalikuwa nyuma kielimu,mimi mwenyewe ni tunda la juhudi za kanisa,hata nikabahatika kuingia kwenye mkondo wa elimu,tutakuwa sio wakweli na tutakuwa hatutendi haki kama hatutalishukuru kanisa hadharani’’,alisisitiza Rais mstaafu Mkapa.
Kulingana na Mkapa chini ya uongozi wa mhashamu mstaafu Askofu Dk.Emanuel Mapunda alisimamia eneo la elimu ukiwemo  mtandao wa taasisi za malezi na mafunzo zilizoimarishwa kuanzia chekechea,shule za  awali, msingi, sekondari,vyuo vya VETA,kompyuta na ualimu.
“Kwa namna ya pekee naona heshima ya kuungana na mhashamu Askofu Emanuel Mapunda ambaye ni ndugu yangu,rafiki yangu na mwanadarasa mwenza wa miaka ya nyuma tukiwa waseminari pale Kigonsera na tukiwa tunatumia dawati moja’’,alisema Rais mstaafu Mkapa.
Hata hivyo Rais mstaafu Mkapa alibainisha mwenzake ambaye ni Askofu mstaafu Mapunda aliendelea na Mungu hadi kufikia uaskofu na yeye  wakati huo aliacha malezi ya seminari lakini hakuthubutu kuyaacha maadili ya dini yake hadi sasa.

Mkapa anasisitiza kuwa historia ya binadamu daima imekuwa na kipimo kimoja tu cha ufadhili wa kweli ambacho amekitaja kuwa ni huduma kwa njia ya majitoleo na sadaka.
Kwa upande wake Askofu mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea mhashamu Norbert Mtega akihubiri katika adhimisho la misa takatifu ya Jubilei pacha ya miaka 25 ya jimbo la Mbinga amewakumbusha watanzania wakati wanatoa maoni kwa ajili ya kuandika katiba mpya wasisahau kipengele cha dini kwa kuwa katiba inakwenda pamoja na Mungu.
“Katiba ambayo haina Mungu ni sawasawa na kutokuwa na katiba,Mungu ni lazima awekwe mbele  katiba haipaswi kujadiliwa na kundi la  watu wachache  kwa maslahi yao binafsi, hivyo ni vyema  ikajadiliwa  kwa makini zaidi na wananchi wenyewe  kwa kuwa ndio wenye haki,’’,alisisitiza
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:

Post a Comment