Habari zinaeleza kwamba, nguvu
kubwa iliyotumika katika maeneo mbalimbali nchini katika chaguzi za ndani ya
CCM ni moja ya mikakati ya maandalizi ya mpango huo wa kuwasimika wanawake.
Wataka urais wanaolengwa kuzimwa
ni pamoja na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa, Edward Lowassa, Waziri Mkuu
mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe.
Wanawake wanaotajwa kufanikisha
mpango huu ni Dk. Mary Nagu, Prof. Anna Tibaijuka na Dk. Asha Migiro ambao
wote watasukumwa na makundi yenye fedha nyingi ili angalao wawili kati yao
waingie hatua ya mwisho.
”Ambao wanatajwa kutaka kuingizwa
hatua za mwisho ni Migiro na Tibaijuka ili wapate nafasi ya kupigiwa kura na
wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM ambao kwa kiasi kikubwa wameandaliwa kwenye
chaguzi za CCM zinazoendelea kwa mikakati maalum na kwa nguvu kubwa ya
fedha,” kilisema chanzo chetu.
Uchaguzi unaoendelea ndani ya CCM
kwenye nafasi mbalimbali, una umuhimu wa peke yake mwaka huu kutokana na
ukweli kwamba ndio uchaguzi wa mwisho ambao utaonesha sura halisi ya kuwapata
wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2015.
Tayari makundi yameshajipanga kwa
kuanza kufitiniana, kuwekeana mizengwe na mengi yanayofanana na hayo ili
mradi tu watu wao wapite kwenye chaguzi hizi za ndani ya chama ili iwe rahisi
kupata mtu wa kulinda maslahi yao au kujihakikishia ulaji pindi mtu wao
atakapopita.
Kutokana na nguvu ya CHADEMA na
kile kinachoonekana kwa wana CCM wenye ushawishi mkubwa kuogopana kwa sababu
mbalimbali, kuna mkakati wa kuwa na 'plan B' ya kusimamisha wanawake, mkakati
kama uliotumika kumzima aliyekuwa Spika wa Bunge, Samwel Sitta.
Sitta alijikuta akitolewa nje ya
ulingo baada ya majina ya wanawake pekee kupitishwa na Kamati Kuu ya CCM
kuwania nafasi hiyo ya uspika.
Wakati akitetea kiti cha uspika,
Sitta ambaye sasa ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alikuwa
mstari wa mbele katika kupinga ufisadi baada ya kutajwa ya kuwa aliendesha
kampeni ya kumng'oa aliyekuwa waziri mkuu kwa wakati huo, Lowassa, kwa
kulazimishwa na Bunge kujuzulu kutokana na kashfa ya kampuni tata ya kufufua
umeme ya Richmond.
”Hapa Sitta alikuwa hana jinsi ila
kusalimu amri, na yakafanyika yaliyokusudiwa na wabaya wake wanaounga mkono
ufisadi.
“Hii plan B inaweza kutumika
kabisa kwenye uchaguzi ujao 2015 kutokana na mikakati yenye hila inayohusisha
fedha nyingi inayoendelea ndani ya CCM,” kilisema chanzo chetu.
Kwa kadri muda unavyokwenda,
kumekuwa na ongezeko la malalamiko kwenye chaguzi za CCM katika ngazi
mbalimbali kutokana na nguvu kubwa ya fedha kutumika kama njia ya kujipanga
kwenye kupitisha jina la mgombea kwenye nafasi ya urais.
Mfumo ulioko sasa hivi wa
kuwatumia wajumbe wa halmashauri kuu za wilaya/mikoa kuchagua wawakilishi wa
kwenda kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mkutano Mkuu wa Taifa
umeonesha kuwa na dosari kubwa sana kutokana na rushwa kubwa ya fedha
inayotumika kuwapata wawakilishi hawa.
Watu wenye malengo ya kugombea
urais na wapambe wao wamekuwa wanatoa fedha nyingi kwa watu wanaowataka
kwenye mikoa na wilaya ili pindi watakapochaguliwa wakawapigie kura ya
kuwapitisha kwenye NEC na mkutano mkuu wa taifa.
"Kwa kweli rushwa za namna
hii ni hatari sana na zinaweza kutupatia viongozi wa ajabu na wapenda rushwa
kutokana na mbegu waliyoiotesha tokea kwenye msingi. Demokrasia nzuri ni ile
ya kupanua wigo ili pawe na matokeo mazuri na yenye maslahi mapana
zaidi," alisema mstaafu mmoja wa CCM.
Baadhi ya wastaafu na wana CCM
wanaochukia rushwa wanapendekeza kuwapo kwa baraza rasmi la mwisho la
kupitisha jina la mgombea wa urais hata kama amepitishwa na vikao vya NEC na
mkutano mkuu.
"Pengine baraza hili liwe na
marais wastaafu, makatibu wakuu wastaafu, watu wenye weledi mbalimbali kwenye
jamii, na pia mawaziri wakuu wastaafu ambao hawagombei kwenye nafasi hiyo ili
mradi tu apatikane mtu makini kwenye nafasi nyeti kama hii ya urais,"
alisema mstaafu mmoja aliyenukuliwa.
CHANZO TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment