SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Nchini
(TANAPA) limeandaa tuzo maalumu kwa waandishi wa habari nchini wanaoandika
habari bora na nzuri kwa ajili ya kuhamasisha utalii wa ndani na umuhimu wa uhifadhi
endelevu.
Meneja Uhusiano wa shirika hilo,
Pascal Shelutete, alisema juzi kuwa shindano hilo litajumuisha makala
zilizotoka magazetini, vipindi vilivyoandaliwa radioni na kwenye runinga
vilivyofanyika kuanzia Januari mosi mpaka Desemba 31 mwaka huu.
Alisema kwenye mshindi wa kwanza
kwenye kila kundi kati ya makundi sita ya kwanza atapata fedha taslimu sh
milioni 1.5, cheti, ngao na safari ya mafunzo ya zaidi ya siku saba kwenye
moja ya nchi za Jumuiya ya Uchumi Kusini mwa Africa (SADC).
Shelutete alisema washindi wa pili
watapata fedha taslim sh milioni moja na ngao wakati washindi watatu watapata
fedha taslim sh 500,000 na cheti ambapo washindi 18 wanatarajiwa kupatikana
kwenye habari za uhifadhi na tisa wengine kwenye uhifadhi wa utalii wa ndani.
Alisema TANAPA imeamua kutoa tuzo
hizo ili kuongeza hamasa kwa waandishi kuandika habari zitakazowahamasisha
wananchi kutembelea vivutio vilivyopo nchini, ili kukuza utalii wa ndani
kwani kwa sasa wanaoongoza kutembelea hifadhi ni watalii kutoka nje ya nchi.
Shelutete alisema pia shindano
hilo limelenga kutoa elimu zaidi kwa wananchi kupitia vyombo vya habari kuona
umuhimu wa kulinda na kuhifadhi maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kuhifadhiwa
kwa kuepuka kuyavamia au kuingiza mifugo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Alisema waandishi wanaotaka
kushiriki shindano hilo wanaweza kutembelea mtandao wa shirika hilo
www.tanzaniaparks.com na kujaza fomu maalum kisha wataituma kwa mkurugenzi
mkuu wa TANAPA kupitia meneja uhusiano.
CHANZO;TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment