RAIS wa Malawi, Joyce
Banda, ameiondoa nchi yake katika mazungumzo ya mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa
na Tanzania, kutokana na kile anachodai kuwa uchokozi, ubabe na vitisho vinavyofanywa na serikali ya
Tanzania dhidi ya raia wake.
Rais
Banda alisema Malawi sasa itaufikisha mgogoro huo katika mahakama ya kimataifa.
Nchi
hizo mbili ziliingia katika mvutano mkubwa wa Ziwa hilo, ambalo linaaminika
kuwa na rasilimali kubwa ya mafuta na gesi.
Rais
Banda alisema amemuagiza Waziri wake wa Mambo ya Nje,kuvunja kabisa mazungumzo
na Tanzania baada ya nchi hiyo kutangaza rasmi uzinduzi wa ramani mpya katika
eneo la Ziwa hilo.
Aidha
alisema nchi yake haitavumilia unyanyasaji unaofanywa na Tanzania dhidi ya raia
wake wanaofanya shughuli za uvuvi katika Ziwa hilo.
Banda
alitoa kauli hiyo wakati alipowasili mjini Lilongwe akitokea mjini New York,
Marekani alikokwenda kuhudhuria mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.
“Wakati
naondoka kwenda New York, nilifikiria kuwa mgogoro huu ungemalizwa kwa njia ya
mazungumzo,” alisema.
“Lakini
wakati nipo njiani, Tanzania walizindua ramani mpya, wamewadhalilisha,
kuwatisha na kuwabugudhi wavuvi wetu na
wanatembea na boti zao katika Ziwa letu,” alisema kwa uchungu mama huyo.
“Suala
limekuwa tete sasa na tunalichukua katika hatua nyengine. Tanzania imetishia
kushambulia boti za Malawi zitakazoonekana katika Ziwa Nyasa,” alisema Banda.
Kiongozi
huyo wa Malawi alisema alifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa UN, Ban Ki-moon na
kumjulisha juu ya nia ya Malawi ya kulifikisha suala hilo katika mahakama ya
kimataifa ya usuluhisi wa migogoro.
Banda
alisema katika mazungumzo yake na Rais Kikwete walipokutana katika mkutano wa
SADC walikubaliana kumaliza mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo.
Hali
katika mpaka wa nchi hizo mbili bado uko swahari, lakini uamuzi huo wa Banda
huenda unaashiria kuwa mgogoro huo umeingia katika sura mpya.
Wakati
huo huo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki Moon amepongeza msimamo wa
Tanzania kutafuta majawabu ya amani na ya kujadiliana kuhusu mzozo wa mpaka
kati yake na Malawi kwenye Ziwa Nyasa.
Ki
Moon alisema uamuzi wa Tanzania ndiyo njia sahihi na inayokubaliwa kimataifa
kutafuta na kupata suluhisho la migogoro ya namna hiyo.
“Majuzi nilikutana na Rais Joyce Banda wa
Malawi na akanielezea mzozo wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa
Nyasa na mazungumzo ambayo nchi zenu mbili zinafanya ili kupata ufumbuzi wa
amani. Hii ndiyo njia sahihi na Umoja wa Mataifa unaunga mkono njia hiyo,”
alisema.
Rais
Kikwete amemweleza Katibu Mkuu huyo wa UN kuwa Tanzania bado inaamini kuwa njia
sahihi na maelewano zaidi ni kutafuta ufumbuzi wa mvutano huo wa mpaka kwa njia
ya mazungumzo.
“Wazo la awali la kutafuta ufumbuzi wa tatizo
hili la miaka mingi sana lilitokana na Rais wa Malawi, marehemu Bingu wa
Mutharika ambaye aliniandikia barua ya kutaka nchi zetu zianze mazungumzo
kuhusu mzozo huo. Nasi tulikubali. Hivyo, ndivyo tulivyoanza kuzungumza,”
alisema
Rais Kikwete.
Alisema
Tanzania inaongozwa na msingi mkuu wa mipaka inayopita kwenye maeneo ya maji
ambako mipaka hiyo inakuwa katikati.
“Mpaka
kati ya Malawi na Msumbiji kwenye ziwa hilo hilo, umekuwa katikati ya Ziwa
tokea mwaka 1954 wakati nchi hizo zilipokubaliana kusahihisha makosa ya kuuweka
mpaka huo nje ya Ziwa. Mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye mto mkubwa zaidi
unaoingiza maji katika Ziwa Nyasa uko katikati ya mto wenyewe,” alisema
Kikwete.
“Kila mahali ambako nchi zinatengenishwa na
maji, mpaka unakuwa katikati ya nchi. Sisi tunadhani hata kwenye mpaka wetu wa
Malawi kwenye Ziwa Nyasa ni lazima uwe katikati ya Ziwa,” alisema.
Lakini
alisema katika hali ya sasa wananchi wa Tanzania wanapokunywa maji ya Ziwa
Nyasa wanaambiwa wanakunywa maji ya Malawi, kila wanaposafiri ndani ya Ziwa
kufanya shughuli zao wanaambiwa wanasafiri kwenye maji ya Malawi.

No comments:
Post a Comment