Na
Albano Midelo
WAKARA
wa barabara mkoa wa Ruvuma TANROAD wametoa mwezi
mmoja kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa kuanzia Mbambabay hadi Lituhi
kubomoa nyumba zao ambazo zinadaiwa zimejengwa katika hifadhi ya barabara.
Meneja wa TANROAD
mkoa wa Ruvuma injinia Abrahamu Kisimbo anadai nyumba hizo zinabomolewa
kutokana na sheria ya barabara yaani
Road Act namba 13 ya mwaka 2007 kifungu namba 29 ambacho kinasema eneo la hifadhi ya barabara
ni mita 30 kutoka katikati ya barabara kwa kila upande.
Anabainisha kuwa kwa
sheria hiyo hairuhusiwi kwa mtu au taasisi yoyote binafsi kujenga ndani ya eneo
la hifadhi ya barabara na kwamba kutokana na hilo ametoa notisi ya mwezi mmoja
kila mwenye nyumba au jengo kuvunja vinginevyo
ofisi yake itavunja jengo na muhusika atatakiwa kurejesha gharama
zitakazotumika katika utekelezaji wa zoezi hilo.
Katika mji mdogo wa
Liuli pekee nyumba 74 zinatarajiwa
kubomolewa hali ambayo imeleta
malalamiko kwa wakazi hao ambao wanaamini serikali haijawatendea haki kwa madai
kuwa nyumba zao zimejengwa kwa mujibu wa
sheria za halmashauri ya wilaya.
Wakizungumza na
mwandishi wa makala haya wananchi wapatao 74 ambao ni wahanga wa barabara
katika eneo la Liuli wanasema
wamesitushwa na kushangazwa na kitendo
cha TANROAD kuweka alama nyekundu ya x na kumkabidhi kila aliyewekewa alama
hiyo barua ya amri ya kubomoa kwa hiari nyumba yake ndani ya kipindi cha mwezi
mmoja.
Mwenyekiti wa wahanga
hao John Komba anasema kutambuliwa kwa
Liuli kuwa mji mdogo kumetokana na uthibitisho uliofanywa kwa vipimo ambao
ulifanywa na idara ya ardhi ambapo ramani ya mji huo sasa ipo makao makuu
jijini Dar es salaam ili kusajiriwa rasmi.
“Watu wengi wa Liuli
tunaishi ndani ya maeneo yenye alama za mji zinazotambuliwa(beacon) ramani hiyo
inaonyesha mitaa na barabara kuu tunaomba TANROAD waitambue ramani hiyo ya mji
wa Liuli uliopimwa mwaka 2004,kwanini ramani hiyo isifuatwe na TANROAD, barabara
inapitishwaje sehemu nyingine,upimaji wa idara ya ardhi hautambuliki?,alihoji
Komba kwa niaba ya wenzake.
Wamedai kuwa kutokana
na barua ya TANROAD ya Septemba 22,2012
inayowapa mwezi mmoja kubomoa nyumba zao kwa madai kuwa wamevamia hifadhi ya
barabara,wao wanapinga na kudai kuwa TANROAD ndiyo imevamia makazi ya watu kwa
kuacha barabara yao ya asili na kuvamia
barabara ambayo wananchi wenyewe walijiundia kwa shughuli zao mbalimbali.
“Waziri Magufuli
tutendee haki kwa sababu Katika barabara hii TANROAD haikuweka tangazo lolote
wala alama ya beacon kama zilivyowekwa katika maeneo mengine,wala kutolea
taarifa yoyote kwa jamii ili isivuke alama zao hivyo kuthibitisha kuwa barabara
haikuwa na mipaka wala kizuizi chochote,TANROAD wameivamia jamii’’,alisisitiza
mwenyekiti huyo.
Historia inaonesha
kuwa barabara ya Mbambabay-Liuli hadi Lituhi imejengwa tangu mwaka 1968 ikiwa
chini ya Halmashauri ya wilaya na ilikabidhiwa TANROAD mwaka 2007,hali hiyo
ndiyo inawafanya wakazi hao wa Liuli kuhoji nini kiliwafanya TANROAD wasiwape
taarifa za sheria yao mapema iwapo barabara hiyo ilikuwa chini yao.
Katibu wa wahanga hao
Lukas Kaunda amesisitiza kuwa wanatambua vya kutosha kuwa ardhi ni mali ya
serikali na inapotaka ardhi kutoka kwa raia wake hupewa na kuichukua kwa
utaratibu na sio kwa kushitukiza kama walivyofanya TANROAD.
Kutokana na hali hiyo
wakazi hao 74 ambao nyumba zao zinatarajiwa kubomolewa ,wameiomba TANROAD na
serikali iwaandalie maeneo mbadala ya kuishi mara watakapoondoka katika maeneo
yao ya sasa.
Kwa kuwa nyumba zao
zitabomolewa bila sababu mahususi,wananchi wameiomba TANROAD na serikali kuandaa malipo kulingana
na gharama za kujenga nyumba mbadala.
Hata hivyo wakazi hao
wameomba kuwa kwa kuwa nyumba zao zitabomolewa katika majira haya ya
mvua,wameiomba serikali iwaandalie
mahema kwa kujikinga na mvua za masika na kwamba wanalaani kitendo cha serikali
kuikubalia TANROAD kubomoa nyumba zao
kipindi cha masika.
Mwenyekiti wa kijiji
cha Liuli Roja Lihonga anahoji,inakuwaje mahali penye ramani halafu mwingine
anatengua?,hivyo ndivyo halali ya maisha ya mtanzania?,barabara ni moja ya
maendeleo sasa inakuwaje mtu avunje nyumba ndani ya mwezi tena kipindi cha mvua
familia yake itaishi wapi’’,alihoji Lihonga.
Mwenyekiti huyo
alidai kuwa wananchi wa Liuli wamesimamisha shughuli zote za ujenzi kutokana na
kutolewa ramani na kwamba hadi sasa
ramani hiyo haijarudi toka makao makuu licha ya kuandika barua kwa mkurugenzi
mtendaji kuomba ramani hiyo.
Diwani wa kata ya
Liuli Charles Chawila anasema ramani ya mji wa Liuli inaonesha barabara kuu
imepita nje ya mji huo ambapo TANROAD
wanadai kukataa kwa madai kuwa ramani hiyo bado haijarudi toka makao
makuu hivyo hawawezi kufanyia kazi wazo tu la Halmashauri.
Diwani huyo ametoa
wito kwa mkurugenzi wa Halmashauri kufuatilia ramani hiyo haraka kabla ya
ujenzi wa barabara ya Mbambabay-Liuli kuanza ili kuepusha hasara ya wananchi wa
Liuli kubomolewa nyumba 74 ambazo zipo
tayari ndani ya ramani ya mji wa Liuli.
Mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga Shaibu Nnunduma amesema ramani ya mji wa Liuli
inafuatiliwa,hata hivyo amedai kuwa wananchi wamefuata barabara hiyo ambayo
ilikuwepo tangu zamani.
Wananchi hao wanahoji
kuwa wameshirikishwaje katika mabadiliko ya sheria ya TANROAD ya mwaka 2007 ya kupanua barabara meta 30
kila upande kwenye serikali za vijiji na kata kwa madai kuwa sheria hizo zimeanzia
mwaka 1967 na kurekebishwa mwaka 1979 na kubadilishwa tena mwaka 2007.
Shirika linalotetea
haki za binadamu kwa kutoa msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na uwezo(NOLA)
limetoa pingamizi ya notisi ya siku 28 ya kubomoa nyumba kwa wananchi wa kijiji
cha Nkali kata ya Liuli.
Mwanasheria wa NOLA
James Maroda katika pingamizi ambalo amemwandikia meneja wa TANROAD mkoa wa
Ruvuma pamoja na mambo mengine ametoa pingamizi hilo kufuatia ofisi ya TANROAD
kutumia sheria ya mwaka 2007 ya barabara yaani Road Act namba 13 kifungu cha
29.
Mwanasheria huyo
amedai kuwa sheria hiyo ni mpya na kwamba wakazi wa Liuli hawawezi kuwa wahanga
wa sheria hiyo ambayo imetungwa wananchi wakiwa tayari wamejenga nyumba zao
ambapo anasema wanastahili kulipwa fidia ya TANROAD endapo nyumba zao
zitabomolewa.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

No comments:
Post a Comment