JUKWAA la Wakristo nchini (TCF),
limeeleza kusikitishwa kwake na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kukaa kimya
licha ya kuwepo uchokozi na kashfa dhidi ya Ukristo vinavyodaiwa kuenezwa
na baadhi ya waumini wa Kiislamu.
Kutokana na hali hiyo, jukwaa
hilo limedai kuwa kanisa liko katika vita ya kiroho, hivyo ni vyema waumini
wote wakakumbuka kuwa, katika mapambano kama hayo Mungu ndiye mlinzi wa
watu na kanisa lake na jibu litapatikana kwa njia ya sala, kufunga na
maombi.
Kauli hiyo nzito ilitolewa jana
kwenye ibada ya kitaifa ya Sikukuu ya Krismasi, iliyofanyika kwenye Kanisa
la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini mjini Moshi na
kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa kanisa na kiserikali.
Tamko hilo zito la TCF,
linajumuisha taasisi kuu za umoja wa makanisa nchini ambazo ni Jumuiya ya
Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),
Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (PCT) na Kanisa la
Waadventisti Wasabato (SDA).
Akisoma tamko hilo kwa niaba ya
jukwaa hilo, Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Martin Shao, alisema
kuwa tamko hilo lina mambo makuu manane ikiwemo masuala ya kuendelea
kuombea amani ya taifa ambayo imetikiswa kwa kiwango kikubwa.
Alisema tamko lao lililotokana
na kikao chao cha Desemba 6 mwaka huu, linalenga kuitaka serikali kukemea
baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu ambao wamekuwa na tabia ya uchochezi,
kwani wanaweza kuhatarisha amani ya nchi na wao kama umoja wa Wakristo,
hawatakubali hali hiyo iendelee.
Hujuma ya kuchomwa makanisa
Askofu Shayo alisema tukio la
kuchomwa moto makanisa ni uchokozi wa wazi, ulioyakuta makanisa na waumini
wake wakiwa hawana habari na bila maandalizi yoyote, hivyo ni muhimu
kuanzia sasa, Wakristo wote wakae macho na wawe waangalifu zaidi.
Alisema katika siku za hivi
karibuni, kumekuwapo na kashfa na uchokozi wa makusudi unaofanywa na baadhi
ya waumini wa Kiislamu hali ambayo inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Sehemu ya tamko hilo zito na la
kwanza kutolewa na umoja huo wa makanisa, ilieleza kuwepo kwa mbinu chafu
ambazo zimekuwa zikifanywa na baadhi ya waumini wa imani ya Kiislamu
kutumia baadhi ya vyombo vya habari vya dini kukashifu Ukristo, pamoja na
kukaa vikao mbalimbali kutaka kuwaua wachungaji na maaskofu.
Alisema hali hiyo inaleta
wasiwasi, hivyo umefika wakati sasa wa viongozi wa dini na waumini
kujilinda wenyewe kutokana na na mbinu za kutaka kuwaua.
Askofu huyo alisema kitendo cha
Serikali ya Rais Kikwete kukaa kimya, inatoa taswira mbaya, kwamba serikali
inakubaliana na kashfa, hujuma za kuchoma makanisa na mali za kanisa.
Alisema tamko hilo linaelezea
kusikitishwa na mahusiano ya Wakristo na Waislamu kuzorota kutokana na
kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya Waislamu ambao wamekuwa
wakifanya makongamano, machapisho mbalimbali, mihadhara kwa lengo la
kuchafua Ukristo, huku serikali ikifumbia macho.
Dhana ya kuwa Tanzania
inaendeshwa kwa mfumo Kristo
Tamko hilo pia lilieleza kuwa
kumekuwa na hoja kwamba serikali inaendeshwa kwa mfumo wa Kikristo, jambo
ambalo si kweli.
Askofu Shayo alisema maneno hayo
ni ushahidi wa uwepo wa ajenda za waumini wenye imani kali na waliojiandaa
kwa mapambano maovu kutetea dhana potofu kinzani na misingi ya demokrasia
na haki za binadamu kama ilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa na kuridhiwa na
serikali.
“Jukwaa la Wakristo nchini
tunakanusha wazi wazi na kueleza bayana kuwa, nchi hii haiongozwi kwa mfumo
Kristo! Kwa watu walio makini hakuna kificho kuwa viongozi wote waandamizi
wa ngazi ya juu serikalini awamu ya sasa, asilimia 90 ni Waislamu (Rais wa
Nchi na Amiri Jeshi Mkuu, Makamu wa Rais, Mkuu wa Usalama wa Taifa, Jaji
Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi). Kwa mantiki hiyo haiingii akilini kueleza
watu kuwa nchi hii inaendeshwa kwa mfumo Kristo!
“Kwa upande wa Zanzibar asilimia
100 ya viongozi ngazi za juu serikalini ni Waislamu, na sio kweli kwamba
Zanzibar hakuna Wakristo wenye sifa za kuongoza. Kisha, hata uwakilishi wa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba, theluthi mbili ya wajumbe wake ni Waislamu.
Tunayo mifano mingine mingi iliyo wazi, na hii ni baadhi tu. Watanzania
wanapaswa kuelewa wazi kuwa, nchi hii inaongozwa kwa misingi ya utawala wa
kisheria na sio vinginevyo,” alisema Askofu Shayo.
Matumizi hasi ya vyombo vya
habari vya kidini
Tamko hilo lilivishambulia
vyombo vya habari vya kidini kwamba vinatumiwa na viongozi wa dini ya
Kiislamu kuukashifu Ukristo na kuwachochea Waislamu, wakiwataka wawaue
maaskofu na wachungaji, iwe kwa siri au hadharani.
Askofu Shayo alisema japo
serikali imesikia kashfa na uchochezi huo hatarishi, imeendelea kukaa
kimya, na kuwaacha wachochezi hao wakiendelea kuhatarisha amani bila
kuwadhibiti.
“Jambo hili linatia mashaka
makubwa juu ya umakini wa dola kuhusu usalama wa wananchi nchini mwao.
Imani kali za namna hii huchochea vitendo viovu vya uasi na hujuma sio tu
dhidi ya waumini na viongozi wa dini fulani, bali hata na kwa serikali na
viongozi waliopo madarakani, endapo waumini wa dini fulani katika taifa
kama Tanzania lililo na waumini wa dini nyingi tofauti, hawataheshimu na
kutendeana kiungwana baina yao na wale wasio wa dini na mapokeo yao. Hali
hii inasababisha kujiuliza kama je, huu ni wakati mwafaka kwa kila raia au
kiongozi wa dini kujilinda yeye mwenyewe na waumini wake dhidi ya wenye
imani kali?” alihoji.
Mapendekezo
Kutokana na hali hiyo, TCF
ilipendekeza kuwa tabia na mienendo ya kukashifiana ikomeshwe kabisa ili
kujenga heshima/staha na utu wa kila mmoja.
“Tunaitaka serikali yetu na
vyombo vyake vya usalama, sheria na amani kutenda mara moja na bila
kuchelewa, katika nyakati ambazo vikundi halifu kisiasa au kidini
vinapoanza uchochezi ili kupambanisha wanajamii.
“Tabia ya kuachia uchochezi wa
kidini kuendelea pasipo hatua mathubuti kuchukuliwa na dola, ni udhaifu
mkubwa wa uongozi na uwajibikaji.
“Ikithibitika kwamba uharibifu
uliofanywa ulitokana na kikundi mahususi chini ya uongozi wa dini au chama
cha kisiasa au asasi isiyo ya kiserikali, basi taasisi husika iwajibishwe
na kulipa fidia kwa uharibifu uliofanywa,” lilisema tamko hilo.
Mapendekezo mengine ni pamoja na
kuanzishwa kwa baraza mahsusi lililo huru lisiloegemea chama chochote cha
kisiasa wala dini yoyote na litamkwe na kuwezeshwa kikatiba likiwa na
dhumuni kuu la kuilinda na kuiongoza serikali kutofungamana na dini yoyote
na kuhakikisha kwamba dira na dhana ya utu katika mfumo wa uchumi wenye
kujali maslahi ya wote havipotoshwi.
“Na sisi viongozi wa dini za
Kikristo, Kiislamu, Kihindu na nyinginezo tuwajibike katika kufundisha, na
katika majiundo ya waumini wetu, hasa vijana, ili kuwajengea uelewa na
utashi wa kuvumiliana kwa upendo.
“Katika kushuhudia na
kuadhimisha imani na ibada zetu, sote tutambue, tulinde na kukuza maadili,
tunu na desturi za imani za watu wengine wanazoziheshimu na kuzitukuza.
“Vikundi vya imani kali na
pambanishi kwa kutumia kashfa potoshaji sharti vidhibitiwe kwa weledi
mkubwa wa viongozi wa dini husika wakisaidiana na Usalama wa Taifa.
Stahamala (kustahimiliana) ni fadhila inayopaswa kufundishwa na kupenyezwa
katika mifumo ya uongozi na maisha ya jamii na ihifadhiwe kwa kufuatiliwa
kwa karibu sana,” lilisema tamko hilo.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu wa
Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycap Pengo, naye
amepigilia msumari kwa kuiasa serikali kutofumbia macho mihadhara ya dini
inayokashifu dini zingine.
Kardinali Pengo ambaye amepata
kunukuliwa mara kadhaa akielezea kukerwa kwake na mihadhara hiyo, alisema
endapo itaendelea kuachiwa, taifa linaweza kujikuta kwenye vurugu za
kidini.
Alitoa kauli hiyo jana wakati wa
ibada ya Sikukuu ya Krismasi, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu
Bonaventura, Parokia ya Kinyerezi, jijini Dar es Salaam.
Alisema mihadhara inayokashifu
dini nyingine haikubaliki kwani kila mtu anaabudu kwa imani yake.
“Mihadhara ya dini imekuwa
ikitumika katika kukashifu dini nyingine huku serikali ikiangalia na
kushindwa kuwachukulia hatua watu wanaotumia mihadhara hiyo kukashifu
wengine. Hali hii ikiendelea kuwa hivyo, tunaweza kujikuta tuko mahali
pabaya,” aliasa Kardinali Pengo.
Alisema hakuna mtu mwenye haki
ya kukashifu dini ya mtu mwingine na kama serikali lazima ikemee mihadhara
ya kukashifiana ambacho kiini chake hafahamu kilipoanzia.
Kardinali huyo alisema tofauti
za kidini zilizopo nchini zisiwe chanzo cha kuvunjika kwa amani.
“Leo tumeona watu wanatengeneza
mihadhara ya kukashifiana hatujui chanzo cha hiyo mihadhara na tumeona siku
za hivi karibuni watu wanachoma makanisa moto, hivyo ni wajibu wa serikali
kulinda amani ya watu na mali zao,” alisema Kardinali Pengo.
Alisema kuchomwa kwa makanisa
serikali haiwezi kusema sio jukumu lao wakati ina wajibu wa kuhakikisha
wanalinda amani.
Mbali na kuionya serikali kuacha
kufumbia macho mihadhara ya kashfa, Kardinali Pengo pia aliwataka Wakristo
wa kanisa hilo wasiwe watumwa wa mali, kwani watu wenye mali kiasi wanaishi
kwa amani katika roho zao kuliko watu wenye utajiri mkubwa.
CHANZO TANZANIA DAIMA
|
No comments:
Post a Comment