Wednesday, December 26, 2012

Waliokuwa wanasomea kwenye mti sasa wapewa darasa




Na Albano Midelo

HATIMAYE Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma imetoa chumba kimoja cha darasa katika shule ya msingi ufundi Namtumbo kwa ajili ya kuwafundishia wanafunzi wenye ulemavu wa akili wapatao 26.

Halmashauri hiyo imetoa darasa hilo tangu mwezi Septemba mwaka huu hivyo kutatua  changamoto ya muda mrefu ya wanafunzi hao kusomea chini ya mti na kuathiri elimu kwa wenye ulemavu.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa makala haya mwezi Mei mwaka huu katika kitengo cha wenye ulemavu shule ya msingi Namtumbo ulibaini kuwa licha ya wilaya nzima ya Namtumbo kuwa na kitengo kimoja cha wenye ulemavu wilaya ilishindwa kujenga hata darasa moja kwa ajili ya watoto hao hali ambayo inamlazimu mkuu wa kitengo hicho Lezile Kampango kuwafundisha wanafunzi hao chini ya mti na wakati wa mvua anakwenda kuwafundishia katika nyumba yake.

Kitengo hicho ambacho kilianzishwa mwaka 1997 ndiyo kitengo pekee kinachotoa elimu kwa watoto wenye ulemavu katika wilaya nzima ya Namtumbo kwa kuwa hakuna kitengo wala shule ambayo inatoa elimu maalum katika makundi mengine ya wenye ulemavu wa wasioona na viziwi.

Mkuu wa kitengo hicho amesema anaishukuru serikali kwa kumpatia chumba maalum kwa ajili ya kusomea wanafunzi wenye ulemavu hali ambayo inaleta unafuu katika ufundishaji.

Hata hivyo Kampango alidai kuwa tangu alipoletwa katika kitengo hicho mwaka 2005 hadi sasa kitengo hicho hakijawahi kupata fedha yeyote kwa ajili ya chakula pamoja na mahitaji mengine muhimu kwa watoto hao licha ya serikali kutoa ahadi ambazo hazijawahi kutekelezwa.

“Bado watoto hawa wanashindwa kupata chakula hali ambayo imesababisha watoto  kuwa watoro,chakula ni muhimu kwa wanafunzi wenye ulemavu ili waendelee kusoma,mlemavu bila chakula hasomi,naomba serikali itoe ruzuku kwa kitengo hiki vinginevyo kinaweza kufa’’,alisisitiza.

Uchunguzi umebaini kuwa katika kitengo cha walemavu Namtumbo kuna vivutio vichache kama vile mpira,filimbi,ambapo upatikanaji wa chakula sio wa uhakika hali ambayo inatokana na kitengo hicho kukosa ruzuku na wazazi wamekuwa wagumu kuchangia kitengo hicho.

Baada ya kitengo hicho kupatiwa chumba kimoja cha darasa sasa kitengo kitakuwa na upungufu wa chumba kimoja cha darasa ambapo  Kitengo hicho hakina nyumba hata moja ya mwalimu kati ya mahitaji ya nyumba mbili,hakuna stoo kati ya stoo mbili zinazohitajika, hakuna bwalo la chakula,jiko, hakuna bweni hata moja kati ya mahitaji ya mabweni mawili na kwamba hakuna ofisi hata moja ya walimu kati ya mahitaji ya ofisi mbili.

Kulingana na mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo Steven Nana katika msimu wa fedha wa mwaka  2012/2013 Halmashauri hiyo ilitenga bajeti ya kiasi cha shilingi milioni saba kwa ajili ya kitengo cha walemavu wa akili Namtumbo.

Hata hivyo alisema Halmashauri imeshindwa kupeleka kiasi hicho cha fedha katika kitengo hicho kutokana na wizara ya TAMISEMI hadi kufikia Desemba mwaka huu kupeleka kiasi  cha asilimia 14 tu ya shilingi bilioni 16 ambazo zimetengwa katika bajeti ya fedha ya mwaka 2012/2013.

‘’Hali ya kifedha katika Halmashauri ni mbaya ,serikali ikileta fedha kitengo hicho kitapewa fedha kama tulivyopanga,upungufu wa fedha ndiyo ambao pia umesababisha ujenzi wa vyumba vya madarasa kushindwa kukamilika’’,alisema.

Takwimu za idara ya elimu za mwaka 2011 zinaonesha kuwa katika wilaya ya Namtumbo kuna wanafunzi wenye ulemavu  wapatao 181 ndiyo wanaosoma  katika shule mbalimbali wakiwemo wenye ulemavu wa akiri 34,wasioona 18,viziwi 11,walemavu wa viungo 109 na albino tisa.

Hata hivyo takwimu hizo zinaonesha kuwa kuna wanafunzi wenye ulemavu wapatao 71 ambao walitakiwa kuandikishwa shule hawasomi wakiwemo wenye ulemavu wa akiri 21,wasioona mmoja,viziwi 11,wenye ulemavu wa viungo 35 na albino watatu.

Takwimu za shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto ulimwenguni(UNICEF) za mwaka 2002 zilionesha kuwa asilimia 98 ya watoto wenye ulemavu katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hawapatiwi kabisa elimu jambo ambalo ni hatari kwa walemavu.

Imeelezwa kuwa asilimia hii ndogo inasababishwa na kuwepo kwa shule chache maalum hapa nchini kwa ajili ya watu wenye ulemavu,ukosefu wa wataalamu,sera na sheria nyingi za nchi hizo  hazitaji moja kwa moja au kutoa utaratibu mzuri wa kutoa elimu kuhusu wenye ulemavu,ukosefu wa vifaa maalum na muhimu vya kuwawezesha kusoma pamoja na miundo mbinu duni  isiyokidhi mahitaji  ya watu wenye ulemavu.







No comments:

Post a Comment