WASICHANA
nchini wameng’ara katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka huu,
baada ya kuongoza kwa asilimia 50.20 na kuwapita wavulana waliopata
asilimia 49.80.
 |
| Waziri wa elimu Dk.Shukuru Kawambwa |
Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, alitangaza matokeo hayo
jana wizarani kwake na kusema kuwa wanafunzi 560,706 wamechaguliwa kujiunga
kidato cha kwanza katika shule za sekondari za serikali.
Alisema,
kati ya wanafunzi hao wasichana waliochaguliwa ni 281,460, huku wavulana
wakiwa 279,246, na hivyo kufanya idadi ya wanafunzi waliochaguliwa
kuongezeka kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na wanafunzi 515,187
waliochaguliwa awamu ya kwanza 2011.
Kawambwa
alisema, mtihani huo uliofanyika Septemba 19 na 20, kwa mara ya kwanza
ulitumia teknolojia mpya ya ‘optical mark reader’ ambapo mitihani
ilisahihishwa kwa kutumia kompyuta.
Alisema
utumiaji wa teknolojia hiyo mpya umeipunguzia serikali gharama kwa kuwa
mwaka jana walimu 4000 walitumia zaidi ya mwezi mmoja kusahihisha mitihani
hiyo nchi nzima, lakini kwa mwaka huu walimu 285 tu ndio waliotumika kwa
siku 15 kukamilisha usahihishaji huo.
“Matokeo
ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi yanaonyesha kuwa alama ya juu kabisa
ilikuwa 234 kati ya 250 kwa wasichana na wavulana. Matokeo hayo pia
yanaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 3087 walipata alama za daraja la A,
wakati wanafunzi 40,683 walipata daraja la B.
“Jumla
ya wanafunzi 222,103 walipata alama za daraja la C na 526,397 walipata
alama za daraja la D. Waliobaki 73,264 walipata alama E,” alisema Kawambwa.
Hata
hivyo, waziri huyo katika maelezo yake, hakuweza kutaja mikoa iliyofanya
vema na ile iliyoshika nafasi ya mwisho. Kadhalika Waziri Kawamba hakuweza
kutoa nafasi ya kutosha kwa waandishi kuuliza maswali kwa kile alichodai
kuwa na haraka ya majukumu mengine ya kitaifa.
Akizungumzia
udanganyifu katika mtihani alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya
watahiniwa waliofutiwa matokeo kutokana na kujihusisha na vitendo vya
udanganyifu katika mtihani huo imepungua.
Alisema
waliofutiwa matokeo 2012 ni watahiniwa 293 tu ikilinganishwa na watahiniwa
9736 waliofutiwa matokeo kwa undanganyifu mwaka jana.
“Kufuatia
udanganyifu huo, serikali itawabaini wale wote waliohusika katika
udanganyifu huo na kuwachukulia hatua stahiki,” alisema.
kuhusu
tatizo lililojitokeza mwaka jana la wanafunzi kutokujua kusoma na kuandika,
serikali imeanzisha mpango mpya wa kuwachuja wanafunzi hao kwa kufanya
mtihani mwingine kabla ya kuanza kidato cha kwanza.
Alisema,
serikali inafanya hivyo ili kujihakikishia haitarudia kosa la kuwapeleka
wanafunzi wa aina hiyo sekondari, bali endapo watabainika watafutiwa
usajili na kupelekwa kwenye mfumo wa kujifunza kusoma na kuandika.
Wanafunzi
894,839 wa shule za msingi walisajiliwa kufanya mtihani huo wa kumaliza
darasa la saba, wengine 29,012 sawa na asilimia 3.24 hawakufanya mtihani
kutokana na sababu za utoro, vifo na ugonjwa.
CHANZO;TANZANIA
DAIMA
|
No comments:
Post a Comment