Saturday, December 15, 2012

Mazingira duni yanavyoathiri taaluma nchini



Na Albano Midelo

MAZINGIRA bora kujifunzia, kufundishia na kuishi ni miongoni mwa mambo muhimu yanayohitajika ili kuhakikisha elimu bora inatolewa katika shule za msingi na sekondari.

Miundombinu hafifu  katika shule za msingi na sekondari ni miongoni mwa changamoto zinazozikabili shule hizo na kuchangia kushusha taaluma katika shule hizo hali ambayo inasababisha wanafunzi kuwa watoro na walimu kushindwa kufundisha ipasavyo kutokana na kuishi katika mazingira mabovu.

Uchunguzi ambao umefanywa katika kata za Kihagara na Liuli wilayani Nyasa unadhihirisha ukweli huu baada ya kubainika shule karibu zote 12 ambazo zimefanyiwa uchunguzi zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa,madawati na nyumba za walimu.

Katika shule ya msingi Ndonga iliyopo katika kata ya Kihagara umebaini kuwa shule hiyo yenye wanafunzi 309 ina vyumba vinne tu vya madarasa kati ya mahitaji ya vyumba tisa hali ambayo inasababisha chumba kimoja cha darasa kutumika na madarasa mawili kwa wakati mmoja hivyo kuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi.

Shule ya Ndonga kulingana na mkuu wa shule hiyo Gorge Mbapira ina vyumba viwili vya madarasa ambavyo vimeezuliwa na upepo tangu mwaka jana hadi sasa havijaezekwa hali ambayo inawalazimu walimu kuwafundisha wanafunzi  huku wakichomwa na jua hali ambayo inachangia utoro katika shule hiyo ambayo mahudhurio ni chini ya asilimia 50.

Kulingana na Mbapira katika shule hiyo yenye walimu watano kuna nyumba moja tu ya mwalimu mkuu yenye vyumba vitatu,kutokana na uhaba wa nyumba, walimu watatu wanaishi katika nyumba hiyo huku mwalimu mmoja ikimlazimu kuishi jikoni hali ambayo inamwathiri mwalimu huyo kisaikolojia na kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo.

“Shule ina nyumba moja tu ya mwalimu mkuu yenye vyumba vitatu,walimu wanne hawana nyumba,nimeamua kuishi nyumba moja na walimu watatu,mwalimu mmoja anaishi katika chumba cha jiko,hali ni mbaya’’,anasisitiza Mbapira.

Katika shule ya msingi Kihagara yenye wanafunzi 498 mkuu wa shule hiyo Anet Ngindo anasema inakabiliwa na upungufu wa vyumba vya kusomea ambapo darasa la kwanza na la pili wanasomea katika chumba kimoja.

Hata hivyo kitaaluma shule hiyo yenye walimu saba kati ya mahitaji ya walimu 14  inafanya wasitani ambapo  mwaka 2009 mtihani wa Taifa wa darasa la saba walifaulu 18 kati ya 78,mwaka 2010 walifaulu 17 kati ya 34 na mwaka 2011 walifaulu sita kati ya 123 waliohitimu.

Katika shule ya msingi Tumbi kata ya Kihagara yenye wanafunzi 478 ina upungufu wa madawati 40 kati ya mahitaji ya madawati 175 na upungufu wa vyumba vitano vya madarasa.

Katika shule ya msingi Mango yenye wanafunzi 508 iliyopo kata ya Kihagara  inakabiliwa na upungufu wa vyumba vinne vya madarasa kati ya vyumba 15 vinavyohitajika,shule haina nyumba hata moja ya mwalimu.

Katika shule ya sekondari ya Mango kuna upungufu mkubwa wa nyumba za walimu ambapo hivi sasa kuna nyumba tatu tu za walimu,shule haina mabweni, ofisi ya walimu, maabara na maktaba.

Katika shule ya msingi Puulu shule yenye wanafunzi 539 inakabiliwa na uhaba mkubwa wa madawati ambapo madawati yaliopo ni 107 na upungufu ni madawati 134,shule hiyo ina upungufu wa vyumba saba,vyumba vilivyopo ni vinane.

Mkuu wa shule hiyo Catherbet Maluka anasema wanafunzi hawana vyoo vya kudumu ambapo vyoo vilivyopo vya muda vina matundu sita,matundu ya vyoo vya kudumu vinavyohitajika kwa wasichana ni matundu 10 na wavulana ni matundu 12.

Katika shule ya sekondari ya kata ya mtakatifu Paulo ya Liuli kwa mujibu wa mjumbe wa Bodi ya shule hiyo ambaye pia ni diwani wa kata ya Liuli Charles Chawila katika miundombinu inakabiliwa na  upungufu wa mabweni,majengo chakavu,hakuna bwalo,maktaba na maabara yenye upungufu wa vifaa.

Katika shule ya msingi Nambira kwa mujibu wa mwalimu mkuu wa shule hiyo yenye wanafunzi 210 inakabiliwa na changamoto kubwa  ya miundombinu ya majengo ikiwemo wanafunzi kutumia banda ambalo limejengwa kwa miti kwa ajili ya kusomea darasa la tatu.

“Shule inatumia banda ambalo limejengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi kwa ajili ya kusomea darasa la awali lenye wanafunzi 45,wanafunzi hao wanasoma kuanzia asubuhi na inapofika saa tisa banda hilo hutumika kama kilabu ’’,alisema mwalimu mkuu.

Mkuu wa shule ya msingi Hongi Simon Ndunguru anazitaja changamoto katika miundombinu zinazoikabili shule hiyo kuwa ni  upungufu wa madawati 57 hali ambayo inasababisha wanafunzi watano hadi sita kukaa katika dawati moja na upungufu wa vyumba saba vya madarasa vilivyopo ni 12.

Katika shule ya msingi Mwongozo yenye wanafunzi 654,shule inakabiliwa na uhaba upungufu wa vyumba 15 vya kusomea vilivyopo ni vitano tu,ofisi zinazohitajika ni nane zilizopo ni tatu tu na darasa la awali lililopo ni chakavu halifai kwa kusomea na wanafunzi wanakalia vigoda ambavyo wanabeba toka nyumbani.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Nkalachi Fabian Ndunguru  anasema shule hiyo ilianzishwa mwaka 1987 yenye wanafunzi 318 ina vyumba nane vya kusomea kati ya mahitaji ya vyumba 17 na upungufu wa madawati.

Afisa elimu msingi katika Halmashauri ya wilaya ya Mbinga David Mkali ameahidi kuandaa takwimu za mapungufu  yote katika zote za shule za msingi ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa,nyumba za walimu,madawati ili kukabiliana na upungufu uliojitokeza.

Ameahidi kuanzisha mpango wa kuchangia elimu ya msingi katika shule zote za msingi kwa kuwahamasisha viongozi wa vitongoji,vijiji, kata na tarafa ili kufuatilia changamoto katika maeneo yao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Afisa elimu huyo ameahidi kufanya vikao na madiwani  wa kata zote zenye matatizo kuelezwa matatizo ya kielimu ambayo yapo katika shule zilizopo kwenye kata zao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu ili kuboresha elimu .



Katika kuhakikisha kuwa taaluma inapanda katika shule za msingi,Mkali ameitaja mikakati kabambe kuwa ni pamoja na kuanza kuandaa kazi za kitaaluma zinazofanana,kuanzisha mfumo wa walimu kutoa mazoezi mengi darasani na kuwatembelea walimu kila kata ili kujionea na kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.



No comments:

Post a Comment