Saturday, December 15, 2012

Mango Sec; Masomo yote ya Sayansi hayafundishwi


Na Albano Midelo
TANZANIA ni nchi ambayo imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa elimu ya sekondari ambapo hivi sasa kila kata kuna sekondari hali ambayo imewezesha watanzania wengi kufikia elimu ya sekondari.

Hata hivyo pamoja na mafanikio ambayo yamepatikana tangu serikali ilipoanzisha mpango wa uboreshaji wa elimu ya sekondari nchini MMES,kuna changamoto mbalimbali zinazozikabili sekondari za kata hali ambayo inachangia kushusha taaluma bora kwa wanafunzi.

Shule ya sekondari ya Mango iliyopo kata ya Kihagara wilaya mpya ya Nyasa mkoani Ruvuma ni miongoni mwa shule za sekondari za kata za serikali ambazo zinakabiliwa na changamoto lukuki hivyo kuchangia kushuka taaluma.

Shule ya sekondari ya Mango ilianzishwa mwaka 2006 ina wanafunzi 405 wakiwemo wasichana 185 na wavulana 220,ina walimu sita tu wanaofundisha masomo ya sanaa hali ambayo imesababisha wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kufanya vibaya katika masomo ya Sayansi.

Mwalimu wa taaluma katika sekondari hiyo Constatine Haule akizungumza kwa niaba ya mwalimu  anasema shule inakabiliwa na upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya Sayansi ambapo masomo yote ya sayansi katika shule hiyo hayafundishwi kabisa.

“Sekondari yetu imebahatika kuwa na vitabu vyote muhimu kwa masomo ya Sayansi vikiwemo vya Hisabati,Biolojia,Fizikia,Kemia,Kompyuta pamoja na vifaa muhimu kwa ajili ya kufundishia masomo hayo lakini kati ya walimu sita waliopo hakuna hata mwalimu mmoja anayeweza kufundisha masomo hayo’’,alisema.

Amebainisha kuwa wanafunzi wengi wanapenda kusoma masomo ya Sayansi na vitabu vipo vya kutosha lakini hakuna mwalimu wala mtu ambaye anaweza kuwaelekeza na kuwapa wanafunzi mwongozo wasome nini katika masomo hayo.

Kutokana na hali hiyo Haule anasema matokeo ya kidato cha nne katika sekondari hiyo ni mabaya na hayaridhisha ambapo takwimu zinaonesha kuwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mwaka 2009 walikuwa 36 kati ya hao wanafunzi saba walifeli,wanafunzi 29 walipata daraja la nne hakuna mwanafunzi hata mmoja ambaye alipata daraja la tatu,pili na la kwanza.

Matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne katika sekondari hiyo mwaka 2010 yanaonesha kuwa wanafunzi 71 walifeli,wanafunzi 40 walipata daraja la nne,wanafunzi wawili walipata daraja la tatu hakuna mwafunzi aliyepata daraja la pili na la kwanza.

Mwaka 2011 yanaonesha kuwa katika sekondari ya Mango jumla ya wanafunzi 72 walifanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne ambapo wanafunzi 45 walifeli,wanafunzi 24 walipata daraja la nne,wanafunzi watatu walipata daraja la tatu ambapo hakuna mwanafunzi aliyepata darala la pili na la kwanza.

Hata hivyo mtaaluma wa sekondari hiyo anasema shule imejitahidi kitaaluma  katika mtihani wa Taifa kwa wanafunzi wa kidato cha pili ambapo mwaka 2007 wanafunzi 37 walifaulu na wanafunzi saba walifeli,mwaka 2008 wanafunzi 113 walifaulu na wanafunzi 20 walifeli,mwaka 2009 wanafunzi 82 walfaulu na wanafunzi watano walifeli,mwaka 2010 wanafunzi 98 walifaulu na wanafunzi watatu walifeli ambapo mwaka 2011 wanafunzi 88 walifaulu na wanafunzi 18 walifeli.

Amesema licha ya kwamba idadi kubwa ya wanafunzi katika shule hiyo wanafeli,bado kiwango cha taaluma amedai ni bora zaidi ukilinganisha na sekondari nyingine za kata zilizopo mwambao mwa ziwa Nyasa ambako kuna mazingira duni ya kujifunzia na kufundishia.

“Tatizo kubwa linalochangia taaluma kuwa chini katika shule hii na shule nyingine ni wazazi na walezi kukosa mwamko wa kielimu,wanafunzi hawajachanganyika kama zilivyo sekondari nyingine hivyo wanafunzi kubadilika inakuwa ni vigumu’’,alisisitiza.

Amekiri ukaguzi wa mara kwa mara unafanyika katika sekondari hiyo,hata hivyo alizotaja baadhi ya changamoto ambazo zinachangia kushusha taaluma kuwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya Sayansi,wanafunzi wanatoka katika mazingira magumu ,upungufu mkubwa wa nyumba za walimu ambapo hivi sasa kuna nyumba tatu tu na mwamko hafifu wa elimu kwa baadhi ya wanafunzi na wazazi.

Ameitaja mikakati ambayo inachukuliwa kuwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa hosteli ili kuwawezesha wanafunzi kuishi shuleni ukilinganisha na hivi sasa wanaishi mbali na shule na kusababisha utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike.

Baadhi ya walimu wanaofundisha katika sekondari hiyo wamedai kuwa mazingira duni ya kufundishia na kuishi yamesababisha walimu kukata tamaa ya kutoa elimu bora  hasa ukosefu wa nyumba za kuishi walimu pamoja na mshahara ambao haulingani na hali halisi ya maisha.

Wamesema wananchi katika kijiji hicho hawana mwamko mkubwa wa kuunga mkono juhudi za maendeleo ya sekondari hiyo hali iliyosababisha ujenzi wa vyumba vya madarasa,hosteli na nyumba za walimu kufanya polepole.

Takwimu za wilaya zilizotolewa mwishoni mwa mwaka jana na Godfrey Mwakilembe kwa niaba ya Afisa elimu sekondari wa wilaya  zinaonyesha kwamba kuna walimu 412 wanaofundisha shule 51 za sekondari za serikali wakati mahitaji halisi ni walimu 726. Kati ya walimu hao 95 tu ndio wa masomo ya sayansi na hisabati.

Uchunguzi umebaini kuwa, shule nyingi za sekondari hazina maabara kwa ajili ya mafunzo ya sayansi kwa vitendo, maktaba,nyumba za walimu,vifaa vya kufundishia na kujifunzia .

Katika shule ya sekondari ya Ngumbo  masomo yote ya sayansi katika sekondari hiyo yanafundishwa na mwalimu mmoja  tena kwa nadharia kutokana na shule hiyo kukosa maabara na vifaa ambapo  wakati wa mitihani wa Taifa wa kidato cha nne wanafunzi hawafanyi mitihani ya vitendo hali ambayo inakatisha tamaa wanafunzi kuchukua masomo ya sayansi na inadumaza elimu katika sekondari hiyo.

Kutokana na changamoto zinazojitokeza wadau wa elimu kwa kushirikiana na wananchi wana kila sababu ya kuhakikisha changamoto hizo zinatafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129












No comments:

Post a Comment