Na
Albano Midelo
Kaimu mkuu wa shule
Hosea Hinju na baadhi ya walimu katika sekondari ya mtakatifu Paulo ya Liuli wilayani Nyasa mkoani Ruvuma wanakabiliwa
na tuhuma nzito za kudaiwa kujihusisha na vitendo vya ngono na baadhi ya
wanafunzi wa shule hiyo.
Baadhi ya wanafunzi
wa kike wa sekondari hiyo ya kata wamedai kaimu mkuu wa shule na baadhi ya
walimu wamekuwa anawalazimisha wanafunzi
wa kike kufanya nayo ngono hali ambayo imesababisha shule hiyo kukabiliwa na
mmomonyoko wa maadili ambao pia umeshusha kiwango cha taaluma katika shule
hiyo.
“Sisi wanafunzi wa
kike tunasumbuliwa sana na baadhi ya walimu akiwemo mkuu wa shule wakitaka
kufanya ngono,wengine tunakataa lakini wengi wetu wanafanya ngono kutokana na
vishawishi mbalimbali,baadhi ya wanafunzi wanakwenda kuwapikia walimu katika
nyumba zao na kufanya ngono’’,walidai.
Wanafunzi watano wa
kike wanaosoma kidato cha tatu ambao majina yao yanahifadhiwa walidai kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wa kike waliomaliza
kidato cha nne mwaka huu walikuwa wanafanya ngono na walimu akiwemo kaimu mkuu
wa shule hiyo wametaka mkuu huyo aondolewe kwa kuwa anawadharirisha watoto wa
kike.
Baadhi ya wazazi na
walezi ambao watoto wao wanasoma katika shule hiyo ya sekondari ambayo kabla ya
kuchukuliwa na serikali ilikuwa inamilikiwa na kanisa Anglikana Dayosisi ya
Ruvuma wamekiri kupata taarifa kuwa kaimu mkuu wa shule na baadhi ya walimu wa
sekondari hiyo wanafanya mapenzi ya wanafunzi .
Mathias Chikeki
mwenyekiti mstaafu wa Bodi ya sekondari ya mtakatifu Paulo anasema taaluma
katika shule hiyo ilisimamiwa vizuri na mkuu wa shule mwanamke ambaye
amehamishiwa mjini Mbinga na kwamba tangu Hinju amekabidhiwa sekondari hiyo
maadili na taaluma imeporomoka kwa kasi.
“Sisi wazazi na
walezi tuna taarifa kwamba walimu wanatongoza wanafunzi na kufanya nao
mapenzi,tuliitisha kikao na kuwaonya walikanusha kuwa sio kweli,shule ina
walimu zaidi ya 15 wapo wenye stashahada na shahada kwanini wanafunzi wanafeli
katika kiwango cha kutisha’’,alihoji Chikeki.
Matokeo ya mtihani wa
Taifa wa kidato cha nne ya mwaka 2010 na
mwaka 2011 katika sekondari ya mtakatifu Paulo yanadhihirisha kuwa kiwango cha taaluma katika shule hiyo
kinatisha ukilinganisha na sifa ambayo shule hiyo ilikuwa nayo awali.
Kulingana na matokeo
hayo mwaka 2010 wanafunzi 93 walifeli mtihani,daraja la nne walipata wanafunzi
38 ,daraja la tatu wanafunzi wawili tu daraja la pili mwanafunzi mmoja na
hakuna mwanafunzi hata mmoja ambaye alipata daraja la kwanza.
Kwa mujibu wa matokeo
hayo mwaka 2011 wanafunzi 97 walifeli,wanafunzi 40 walipata daraja la nne
hakuna mwanafunzi hata mmoja aliyepata daraja tatu,pili na la kwanza hali
ambayo wazazi na walezi wametaka kaimu mkuu wa shule hiyo kuondolewa kwa kuwa
ameshindwa kusimamia maendeleo ya sekondari hiyo.
Diwani wa kata ya
Liuli Charles Chawala amekiri kusikia tuhuma dhidi ya kaimu mkuu wa shule hiyo
ambapo ameahidi yeye kama msimamizi wa maendeleo katika kata hiyo atafuatilia
ili ufumbuzi upatikane na kurudisha heshima ya sekondari hiyo.
“Kwa ujumla taaluma
katika sekondari ya mtakatifu Paulo imeporomoka kutokana na sababu mbalimbali
zikiwemo ukosefu wa mabweni,baadhi ya wanafunzi hawana mwamko kutokana na
kusumbuliwa kimapenzi na baadhi ya
walimu ingawa walimu wamekanusha’’,alisema.
Hata hivyo anasema
katika sekondari hiyo kila mwaka kunajitokeza kesi za mimba ingawa wanafunzi
hawajawataja walimu kuwa ni miongoni mwa wahusika ambapo mwaka huu pekee
kulingana na hotuba ya mkuu wa shule aliyoisoma kwenye mahafali kuna kesi saba za mimba ambazo zipo mahakamani.
Alipofuatwa ofisini
kwake kwa ajili ya kujibu tuhuma zinazomkabili,kaimu mkuu wa shule hiyo alisema
haruhusiwi kusema lolote kwa waandishi wa habari hadi atakapopata kibali kutoka
kwa mkuu wake ambaye ni afisa elimu sekondari.
“Siwezi kuwapa habari
yeyote inayonihusu mimi na sekondari hii hadi mkuu wangu anipe kibali cha
kufanya hivyo,mimi siwatambui fanyeni lolote siwezi kujibu tuhuma zozote bila
kibali,mkuu wangu amenikataza kutoa habari kwa waandishi,upo waraka ambao unanikataza’’,alisisitiza.
Hata hivyo Afisa
elimu kata ya Liuli Abraham Challe alimshangaa kaimu mkuu wa shule hiyo kukataa
kutoa habari kwa wana habari ambao wanaibua mafanikio na changamoto za kielimu
licha ya diwani wa kata ya Liuli kumuagiza kufanya hivyo.
Alizitaja changamoto
zinazoikabili sekondari hiyo kuwa ni
pamoja na kushuka kwa kiwango cha ufaulu,ukosefu wa vifaa vya maabara na vifaa,
upungufu wa mabweni,maktaba,bwalo la chakula, upungufu wa matundu ya choo na
upungufu wa vifaa vya kufundishia.
Samwel Mawanja katibu
wa kata mstaafu anataja sababu kubwa ya kushuka kwa taaluma katika sekondari
hiyo ni kuwepo kwa uongozi mbovu wa kaimu mkuu wa shule hiyo ambaye alidai kuwa
uwezo wake wa elimu ni wa chini ambaye ana stashahada ambapo kuna walimu wengi
wenye shahada ambao anashindwa kuwaongoza.
Anasema taaluma
imeshuka katika kipindi cha miaka mitano sasa kutokana na kaimu mkuu huyo
alikuwa anatoa adhabu nyingi kwa wanafunzi hali ambayo imesababisha kukithiri
kwa utoro kwa wanafunzi na kusababisha taaluma kuwa chini hadi sasa.
Mikakati ambayo
inatarajiwa kuchukuliwa ili kuinua taaluma katika shule hiyo kwa mujibu wa
diwani wa kata hiyo ni kukamilisha ujenzi wa hoteli ili wanafunzi wote waishi
shuleni,walimu kuwajibika ipasavyo kufundisha, wazazi na walezi kuwasimamia
watoto katika masomo.
Wazazi na walezi
wametoa wito kwa waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi kuhakikisha kaimu mkuu huyo wa shule anaondolewa kwa kuwa
ameshindwa kusimamia maendeleo ya shule hiyo kitaaluma pamoja na matumizi
mabaya ya fedha za ujenzi wa sekondari hiyo.
Wananchi wa kata ya
Liuli pia wametaka kaimu mkuu wa shule aondolewa na kushitakiwa kwa kuwa
ameshindwa kusimamia ujenzi wa kidato cha tano na sita katika shule ya
sekondari ya kata ambapo wamekuwa wanachangia ujenzi wa shule hiyo ambayo
ilitakiwa kufunguliwa tangu mwaka juzi.
“Kaimu mkuu wa shule
hajawahi kutusomea mapato na matumizi
licha ya kwamba wananchi tumekuwa na moyo wa kuchangia,kutokana na hilo
wananchi hivi sasa hawapo tayari kuendelea kuchangia fedha ambazo hawajui kiasi
cha fedha zilizopatikana na zilizotumika’’,walisema wakazi wa Liuli Michael
Shauri,Victor Komba,Mathias Erenest na Samwel Mawanja.
Afisa elimu wa
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga ambaye anasimamia wilaya mpya ya Nyasa David
Mkali akizungumzia tuhuma za uongozi wa kaimu mkuu wa shule ya sekondari ya
mtakatifu Paulo ya Liuli ambaye pamoja
na tuhuma nyingine wananchi wanataka aondolewa kwa kuwa ameshindwa kusimamia
shule hiyo ameahidi kufuatilia tuhuma hizo.
“ Kwa kawaida huwa
haondolewi mara moja,ikithibitika kuwa ameshindwa kuongoza,licha ya kupewa
maelekezo taratibu za kumuondoa zitafanyika,tunatambua shule hiyo ina walimu
wenye shahada na mkuu wa shule ana stashahada,ikumbukwe kuwa walimu wenye
shahada wamefika kuanzia mwaka jana kabla
ya hapo walimu wengi walikuwa na stashahada,wakipata uzoefu wa kazi wanaweza kupata barua za kuteuliwa kuwa wakuu
wa shule’’,alisema.

No comments:
Post a Comment