Na Albano
Midelo
HALMASHAURI ya wilaya
ya Namtumbo mkoani Ruvuma imepiga marufuku shule za msingi zenye upungufu wa
vyumba vya madarasa kutumia vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi
kama vyumba vya madarasa.
Mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo Steven Nana katika mahojiano na mwandishi wa makala haya
alisema katika mkutano wa Baraza la madiwani uliofanyika mwezi Juni mwaka huu
walipendekeza shule zote ambazo zinatumia madarasa ya vibanda vilivyojengwa kwa
miti na kuezekwa kwa nyasi kuvibomoa badala yake kujenga madarasa kwa kwa kutumia tofali za kuchoma.
‘‘Hadi sasa madiwani
katika kata zenye shule ambazo wanafunzi wanasomea vibanda vya nyasi wameitikio
wito vibanda vimebomolewa na kujenga vyumba kwa tofali za kuchoma kwa mfano
kata za Mgombasi, Luchiri na Msindo,kata ambayo bado hawajatekeleza ni uzembe
wa usimamizi wa diwani husika,vibanda vya nyasi sio mazingira rafiki kwa
kusomea wakati wa mvua vinavuja na kuathiri taaluma’’,alisisitiza.
Hata hivyo alisema
wananchi waliamua kujenga vibanda vya nyasi kwa lengo la kukabiliana na
upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa ambapo alisema serikali ilitoa masharti
magumu kwa wananchi kwa kuwataka wajenge vyumba vya madarasa kwa kutumia kokoto
kwenye msingi na kujenga kwa theluji badala ya udongo jambo ambalo wananchi
walishindwa kumudu gharama za ujenzi.
Kutokana na hali hiyo
mwenyekiti huyo anasema walipendekeza wananchi kujenga vyumba vya madarasa kwa
udongo na tofali za kuchoma ambapo serikali iliahidi kuchangia vifaa vya
kiwandani ambapo hadi sasa tayari wananchi wamefyatua tofali na fedha zitakapopatikana wanapewa ili
kukamilisha ujenzi.
‘‘Halmashauri yangu
inakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha katika mwaka wa fedha wa 2012/2013 ilitengewa
shilingi bilioni 16 lakini hadi kufikia mwezi huu Desemba ni asilimia 14 tu ya
fedha ndiyo imefika kutoka TAMISEMI,fedha ikipatikana tutazipeleka katika shule
kwa ajili ya kukamilisha ujenzi’’,alisema
Uchunguzi ambao
umefanywa katika shule tatu za msingi kata
ya Rwinga wilayani Namtumbo ambazo ni Rwinga,Kidugalo na Mkapa umebaini shule
hizo zimefyatua tofali 80,000 kwa ajili
ya kukabiliana na upungufu wa vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.
Mwandishi wa makala
haya mwezi Mei mwaka huu alifanya uchunguzi katika kata ya Rwinga na kubaini wanafunzi
500 katika shule hizo wanasomea kwenye vibanda vilivyojengwa kwa miti na
kuezekwa nyasi na wengine wanasoma madarasa mawili katika chumba kimoja huku
wamegeuziana migongo hali ambayo imekuwa inaathiri taaluma katika shule hizo.
Kaimu mwalimu mkuu wa
shule ya msingi Kidugalo yenye wanafunzi 427 Getruda Turuka alisema katika
shule hiyo tofali zaidi ya 20,000 zimefyatuliwa na kuchomwa kwa ajili ya ujenzi
wa vyumba vya madarasa ili kukabiliana na upungufu mkubwa wa vyumba vya
madarasa ambapo shule hiyo ina vyumba vinne kati ya 13 vinavyohitajika.
Licha ya kwamba
tofali kwa ajili ya ujenzi zimekamilika,hata hivyo serikali ya kijiji cha
Kidugalo ilipanga kuanza ujenzi wa vyumba vya madarasa mapema,lakini uongozi wa
Halmashauri uliwazuia kujenga kwa madai kuwa hakuna uwezo wa kuwasaidia vifaa
vya viwandani ambavyo ni bati,misumari na thaluji.
Said Juma na Tamimu
Mwela ni wenyeviti wa vitongoji vya Lilunde na Namwaya wanasema tofali
zimekamilika na walitaka kuanza ujenzi wamekwamishwa na Halmashauri kuwazuia
kuanza ujenzi katika shule ya msingi
Kidugalo kwa madai kuwa Halmashauri hivi sasa haina fedha.
Katika shule ya
msingi Mkapa ambayo haikuwa na nyumba hata moja ya mwalimu ,hivi sasa kuna
ujenzi wa nyumba ya mwalimu ambayo inaweza kuchukua familia mbili.
Mwalimu mkuu wa shule
hiyo Hans Mwailima anasema kamati ya shule kwa kushirikiana na uongozi wa
kijiji umeamua kuanza ujenzi wa nyumba ya mwalimu hali ambayo inaweza kupunguza tatizo la
nyumba kwa walimu ambapo hivi sasa walimu wote 10 wanaofundisha katika shule
hiyo akiwemo mwalimu mkuu wamepanga.
Hata hivyo amesema
shule hiyo yenye wanafunzi 261 ina
vyumba vinne tu kati ya mahitaji ya vyumba nane,madawati yaliopo ni 62 kati ya
mahitaji ya madawati 106.
Katika shule ya
msingi Rwinga yenye wanafunzi 436
,kamati ya shule kwa kushirikiana na serikali ya kijiji wamefyatua tofali zaidi
ya 25,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya kusomea ili kuepukana na wanafunzi
187 wa darasa la tatu na awali kusomea kwenye vibanda viwili vya nyasi
vilivyojengwa katika shule hiyo.
Mwalimu mkuu msaidizi
katika shule hiyo Hamza Ngonyani amesema kamati ya shule na serikali ya kijiji
wamehamasisha michango ambapo kila mzazi alitoa mchango wa shilingi 2000 na
kufanikisha kufyatua na kuchoma tofali ambazo zinaweza kujenga vyumba viwili
vya madarasa.
Hata hivyo Ngonyani
alibainisha kuwa changamoto kubwa iliyopo hivi sasa ni upatikanaji wa vifaa vya
kiwandani zikiwemo bati na theluji kutoka Halmashauri ya wilaya ambayo imesema
hivi sasa haina pesa za kusaidia kukamilisha ujenzi huo hivyo wameshauriwa
kuacha kuanza ujenzi.
Katika shule ya
msingi Selous hakuna hatua zozote ambazo zimechukuliwa kwa lengo la kukabiliana
na upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa ambapo shule hiyo ina wanafunzi zaidi
ya 100 wanaosoma katika vibanda vya nyasi.
Baadhi ya walimu
wanaofundisha katika shule hiyo ambao hawakutaka kutaja majina yao walidai kuwa
baada ya vyombo vya habari kutoa habari kuhusiana na shule hiyo viongozi kutoka
Halmashauri walifika,lakini hadi sasa hakuna kilichofanyika zaidi ya vibanda
vilivyopo kuviboresha kwa kuezeka nyasi ili kukabiliana na mvua za masika.
Halmashauri ya wilaya
ya Namtumbo yenye kata 14 ina shule za msingi 107 kati ya hizo shule 105
zinamilikiwa na serikali na shule mbili ni za watu binafsi na mashirika ya dini.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

No comments:
Post a Comment