MCHAKATO wa
kumtangaza mtumishi wa Mungu Sr.Bernadeta Mbawala kuwa mwenyeheri ngazi ya
jimbo kuu la Songea unatarajia kufungwa rasmi Januari 14 mwakani.
Hayo yamesemwa na
msimamizi mkuu msaidizi wa mchakato huo Bro.Regnald Cruz ambaye anamwakilisha
Baba mtakatifu wa Roma aliyewasili jimbo
kuu la Songea Jumamosi jioni kwa ajili ya kufuatilia,kukagua na kuangalia hatua
mbalimbali za mchakato huo katika ngazi ya jimbo zinavyoendelea tangu
kuzinduliwa kwake Januari 26 mwaka huu.
Msimamizi mkuu
msaidizi amefurahishwa na kazi nzuri ambayo imefanywa na kamati zote za
mchakato wa mtumishi wa Mungu hali ambayo imesababisha mchakato ngazi ya jimbo
kukamilika kwa takribani miezi kumi tu badala ya miaka miwili ambayo ilipangwa
awali.
Alisema mchakato wa
kumtangaza mtumishi wa Mungu ngazi ya jimbo ni mgumu ambao huwa unachukua kati
ya miaka miwili hadi mitano kabla ya kukamilika na kufungwa kwa hatua ya juu
makao makuu ya Baba mtakatifu Roma.
“Nimeridhika na kazi
nzuri ambayo imefanyika katika mchakato wa kumtangaza Sr.Bernadeta Mbawala
ngazi ya jimbo,mtumishi huyu wa Mungu amekuwa mtanzania wa kwanza kufanikisha
mchakato huu ngazi ya jimbo,naomba endeleeni kusali kwa bidii hadi siku ya
kufungwa rasmi mchakato huu Januari 14 mwakani’’,alisisitiza.
Bro.Cruz alisema
kamati zote zimefanyakazi kubwa ambayo
imevuka vigezo ambavyo vimewekwa na makao makuu Roma,alitolea mfano wanaotakiwa
kutoa ushuhuda ngazi ya jimbo wanatakiwa wawe 30 lakini katika jimbo kuu la Songea
watu 52 wametoa ushuhuda na bado kuna watu wengi ambao hawajapata nafasi ya
kutoa ushuhuda wao.
Msimamizi mkuu huyo
msaidizi ameipongeza kamati ya habari na
mawasiliano kwa kufanyakazi yake vema ya kusambaza habari kupitia
magazeti,redio na mitandao ya kijamii hali ambayo imesababisha watu wengi
kuelewa kuhusu mchakato wa Sr.Bernadeta hivyo kushiriki kikamilifu na
kufanikisha ngazi ya jimbo.
“Nilishangaa
nilipofika Dar es salaam nilipowauliza baadhi ya watu kwamba wanamjua mtumishi
wa Mungu Sr. Bernadeta Mbawala walinieleza kwa ufasaha kila kitu,nilitambua
kuwa hii ni kazi nzuri ya vyombo vya habari hususan vya kanisa kutoa habari na makala mbalimbali
za redio na magazeti,watu wameelewa na sasa mchakato ngazi ya jimbo umefanikiwa
kwa wakati’’,alisema.
Hata hivyo alisema
baada ya mchakato ngazi ya jimbo
kufungwa rasmi mapema mwezi Januari mwakani,kitakachofuatia ni mchakato
wa kumtangaza Sr.Bernadeta Mbawala makao makuu ya kanisa Roma Italia ambako
alisisitiza gharama za mchakato zitakuwa kubwa zaidi na kwamba mchakato huo
Roma unaweza kuchukua miaka kadhaa hadi kukamilika.
Alibainisha kuwa
mchakato ngazi ya jimbo utakapofungwa rasmi Januari 14 mwakani, kamati
zitakazoendelea na kazi ni kamati ya fedha na kamati ya habari na mawasiliano
na kwamba kamati nyingine za mchakato ambazo ni kamati ya mahakama,Teolojia na
Historia zitamaliza kazi siku hiyo ambayo mchakato utafungwa ngazi ya jimbo.
“Watu wenye ushuhuda
wanaweza kuwasiliana na kamati ya habari na mawasiliano ,hata hivyo miujiza
ambayo inatakiwa kutolewa ushuhuda ni wale ambao wameponywa na mtumishi wa
Mungu magonjwa ambayo yameshindikana katika vituo vya afya,ni lazima waonyeshe
kumbukumbu za hospitali ambazo zinaonesha walikuwa na magonjwa hayo awali kabla
ya kupata miujiza ya kuponywa’’,alisema.
Watu wengine ambao
wanaweza kutoa ushuhuda wao kwa mujibu wa Bro.Cruz ni wale ambao wamepata
miujiza ya kipekee katika jamii hivyo ametoa wito kwa watanzania wote ambao
wamepata miujiza watumie nafasi hiyo
adimu kueleza maajabu ya mwenyezi Mungu katika maisha yao waliyoyapata
kupitia Sr.Bernadeta.
Bro.Cruz amekuwa
jimboni Songea kuanzia Jumamosi hadi Jumanne wiki hii ambapo ameweza kukutana
na kamati zote za mchakato ikiwemo kamati ya habari na mawasiliano,kamati ya Historia,
kamati ya Fedha,kamati ya Teolijia na kamati ya mahakama.
Pia alitembelea
Abasia ya Peramiho mahali ambapo yalifukuliwa masalia ya Sr.Bernadeta,alitembelea
katika kijiji cha Likuyufusi wilayani Songea mahali ambapo mtumishi wa Mungu
Sr.Bernadeta Mbawala alizaliwa na kuangalia eneo hilo wananchi wa kijiji hicho
wametoa ekari nne ambazo zinatarajiwa
kuendelezwa ikiwemo kujengwa kanisa.
Bro.Cruz pia ametembelea
katika kanisa la Chipole ambapo sanduku dogo la masalia ya mtumishi wa Mungu Sr
Bernadeta yamehifadhiwa na kanisa kuu la kiaskofu ambapo limewekwa sanduku
kubwa la masalia.
Akizungumza wakati
anatoa salamu kutoka kwa Baba mtakatifu Jumapili kwa waumini katika kanisa kuu
la kiaskofu msimamizi mkuu msaidizi huyo aliwaasa waumini kuendelea kusali kwa
bidii hadi hapo utakapofungwa rasmi mchakato ngazi jimbo Januari mwakani.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment