| Askari wa wanyamapori pori la Selous wakionyesha pembe za ndovu |
Na Albano
Midelo
KAMPUNI ya Game Frontiers Tanzania(GFT) inayojishughulisha na uwindaji wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, kwa kushirikiana na kikosi cha askari wanyamapori katika pori la akiba la Selous, wamefanikiwa kukamata pembe za ndovu zenye thamani ya shilingi milioni 192.
Kaimu mkuu wa pori la akiba la Selous kanda ya kusini Magharibi Likuyuseka, Bernald Lijaji alisema pembe hizo zilikamatwa mwezi Februari 17 mwaka huu majira ya asubuhi, huko katika maeneo ya wazi ya jumuiya ya Mbarang'andu ambayo yamekaribiana na pori la akiba la Selous wilayani humo.
Kulingana na kaimu mkuu huyo wa pori la Selous pembe zilizokamatwa zilikuwa 15 , risasi tisa na bunduki mbili kati ya hizo moja ni aina ya Gobole na nyingine Raifo na kwamba pembe hizo na bunduki zilizokamatwa hivi sasa vinashikiliwa katika ofisi ya pori la akiba la Selous iliyopo wilayani Namtumbo.
“ Majangili ambao
walikutwa wakiwa na nyara hizo za serikali mara baada ya kukurupushwa na askari
wa wanyamapori walitoroka na kutokomea mahali ambako hadi sasa haijafahamika
ingawa bado wanaendelea kusakwa ili wakikamatwa waweze kufikishwa kwenye vyombo
vya sheria’’,alisisitiza.
Alibainisha zaidi kuwa pembe hizo 15 zilizokamatwa ni sawa na
Tembo wa nane waliouawa, na kwamba vitendo vya ujangili katika pori la akiba la
Selous vimekuwa vikiwatesa kutokana na watu wasiokuwa waaminifu kuingia ndani
ya pori na kuua wanyama bila kufuata taratibu na sheria za nchi.
Hata hivyo alisema kuwa jitihada za kuwakurupusha majangili hao zinatokana na ushirikiano uliopo kati ya kampuni ya Game Frontiers(GFT), askari uhifadhi wa vijiji(VGS) na kikosi cha askari wanyama pori (Game reserve) cha pori la akiba la Selous.
Kampuni ya GFT
kwa muda mrefu sasa imekuwa inatoa mafuta na gari ya doria, chakula, mawasiliano
na kuwalipa posho askari ambao hushughulika katika kazi ya kupambana na
ujaingili katika pori la akiba la Selous.
Akizungumza na waandishi wa habari mwakilishi wa kampuni hiyo Mohamed Mpapa alisema mafanikio hayo yanatokana na jitihada walizonazo na ushirikiano wa wananchi walio jirani na pori hilo.
Hata hivyo Mpapa alitoa wito kwa jamii kuendelea kujenga ushirikiano, katika kuwafichua watu wanaohusika na vitendo vya ujangili kuua wanyama waliopo katika hifadhi na kutorosha nyara za serikali pasipo kufuata taratibu zilizowekwa na nchi.
albano.midelo@gmail.com
No comments:
Post a Comment