![]() |
| Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu |
Na Albano
Midelo
WANAFUNZI 8365 kati ya 11364 wamefeli mtihani wa Taifa wa kidato cha nne katika mkoa wa Ruvuma
kwa kupata alama sifuri.
Taarifa ya afisa elimu wa mkoa wa Ruvuma Mayassa Hashim
ambayo ameitoa kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Ruvuma (RCC) inaonyesha kuwa katika
mtihani huo uliofanyika mwaka jana wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 13,daraja la pili
96,daraja la tatu 273 na daraja la nne wanafunzi 2617.
Taarifa hiyo ya elimu
inaonyesha kuwa shule iliyokamata nafasi ya kwanza kimkoa ni sekondari ya
Mtakatifu Luis inayomilikiwa na watawa wa jimbo katoliki Mbinga ambayo daraja
la kwanza wapo wanafunzi wawili,daraja la pili 10,daraja la tatu18,daraja la
nne tisa hakuna mwanafunzi alifeli.
Kwa mujibu wa taarifa
hiyo nafasi ya pili imekamatwa na seminari ya Likonde inayomilikiwa na jimbo
katoliki la Mbinga ambapo daraja la kwanza wapo wawili,daraja la pili 11,daraja
la tatu12,daraja la tatu 13 hakuna mwanafunzi aliyefeli.
Shule ya sekondari ya
Ndongosi ambayo mwaka 2011 ilikuwa ya mwisho kitaifa baada ya kufelisha
wanafunzi wote,mwaka jana shule hiyo imekata nafasi ya mwisho katika shule za
sekondari 163 za mkoa wa Ruvuma baada ya kufelisha wanafunzi wote wa kidato cha
nne
Kufuatia matokeo hayo
mabaya,afisa elimu wa mkoa wa Ruvuma aliitaja
mikakati ambayo inachukuliwa kwa kushirikiana na wadau wa elimu kuwa ni pamoja
na kutoa vifaa vya kujifunzia,kufundishia,kukuza taaluma kwa ufanisi na kutoa
motisha kwa wanafunzi.
“Nawaomba wazazi na
walezi wasisahau wajibu wao kwa wanafunzi ikiwemo kujenga tabia ya kufuatilia
maendeleo ya watoto wao, kuwanunulia mahitaji muhimu ya shule,kuangalia tabia
za watoto wao na kushirikiana na walimu ili kuboresha taaluma katika shule
zao’’,alisisitiza.
Baadhi ya changamoto
ambazo ziliibuliwa katika kikoa hicho na kutajwa kuwa zinachangia kushusha
taaluma ni pamoja na upungufu mkubwa wa walimu,mazingira duni ya kufundishia na
kujifunzia, baadhi ya wakuu wa shule kutoishi shuleni na utoro wa baadhi ya
walimu.
Akizungumza wakati
anafungua kikao hicho cha RCC mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu
aliwakumbusha wadau wote umuhimu wa kudumisha amani,upendo,utulivu na
mshikamano wa kitaifa ambao alisema siku
za karibuni kumekuwa na vitendo vya wazi kushabikia machafuko.
“Kwa bahati mbaya
sana kuna watu wachache wanaendesha vitendo vya uchochezi kupitia imani za
kidini kwa kuhubiri chuki miongoni mwa wananchi katika nyumba za ibada na nje
ya nyumba hizo kupitia mihadhara ya kidini,kutumia kanda za kaseti na video kwa
mwamvuli wa kueneza elimu ya dini kwa waumini wao’’,alisema.
Alisisitiza kuwa
machafuko hayafanyiwi majaribio na kwamba hakuna aliyefanikiwa kupitia
machafuko akatahadharisha kuwa gharama ya kupoteza amani ni kubwa kuliko kitu
chochote hivyo amewataka wananchi kuwakataa wote wanaohubiri chuki za
kidini,kikabila na itikadi za kisiasa kwa lengo la kuwagawa watanzania na kuleta machafuko.
“Serikali
haitamvumilia mtu yeyote,kundi lolote,kiongozi wa kidini au siasa
atakayeonekana kuchochea machafuko na chuki
mkoani kwetu,serikali kupitia jeshi la polisi itamkamata na kumfikisha mbele ya sheria’’,alisema.
albano.midelo@gmail.com

Inasikitisha kweli jamani ..hivi inakuwaje mwaka huu?
ReplyDelete