Wednesday, March 13, 2013

Mashujaa wa vita vya Majimaji wapigiwa mizinga



Wanajeshi wakipiga mizinga kuwakumbuka mashujaa wa vita vya majimaji

Na Albano Midelo
WAZIRI wa maliasili na utalii Balozi Hamisi Kagasheki ametoa mwito kwa wadau mbalimbali wa mikoa ya kusini kuyatambua maeneo yote ya kihistoria na yenye vivutio vingine vya utalii ili kuboresha utalii ukanda wa kusini.

Waziri Kagasheki ametoa mwito huo wakati anazungumza katika kilele cha siku ya kumbukizi la vita vya Majimaji zilizofanyika katika viwanja vya makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea.

Kilele cha makumbusho hayo kilihudhuriwa na wageni mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakiwemo mkuu wa mkoa wa Mbeya Abasi Kandoro,mkuu wa mkoa wa Rukwa Stella Manyanya,mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama na mstahiki Agusto Assifue meya wa jiji la Lichinga nchini Msumbiji.

Waziri Kagasheki amewahimiza wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha kuwa wanavitangaza kwa nguvu zote vivutio vya utalii ambavyo vitaibuliwa pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa sekta ya utalii nchini inavyochangia kuinua uchumi wa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.


“Ni vizuri uendelezaji wa vivutio vya utalii uhusishe kuboresha miundo mbinu kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali kuelekea maeneo ya utalii,kutengeneza ramani ya mkoa,kuwa na wataalamu wa kuongoza watalii,kuajiri maafisa utalii na malikale kuwa na usafiri wa uhakika na kuweka taarifa za vivutio kwenye tovuti’’,anasisitiza.

Ameshauri kila mkoa kushirikiana na wizara yenye dhamana yaani maliasili na utalii pamoja na wadau wengine kutoka sekta binafsi kuhakikisha kuwa uboreshaji wa sekta ya utalii nchini unahitaji wadau wengi na sio jukumu la wizara ,mkoa au shirika la makumbusho ya Taifa pekee.

Akizungumzia kuhusu siku ya kumbukizi la vita vya Majimaji waziri Kagasheki amelitaja lengo la kufanya kumbukizi hizo kuwa ni kivutio cha utalii wa kihistoria na utamaduni ili kuwapa fursa wananchi wa mikoa ya kusini kutangaza utalii wao wa kiutamaduni.

“Nimefurahi kuona kuwa kwa siku tatu ambazo zilikuwa za kumbukiz hili wananchi wamepata fursa ya kutembelea vivutio vilivyopo mkoani Ruvuma,kufanya mdahalo na warsha kuangalia namna ya kuviendeleza na kuweka mikakati au maazimio ya namna ya kuvitunza na kuviendeleza vivutio vya utalii’’,anasema.

Waziri huyo mwenye dhamana ya utalii ameagiza kumbukizi hizo kuwa kichocheo cha mabadiliko chanya kwa jamii ambapo ameshauri watoto na vijana kuibua vipaji vyao,ameahidi wizara yake kuanzia sasa itaanza kuandaa program kwa watoto na vijana ili kukidhi matakwa hayo.

Ametoa rai kwa mikoa mingine nchini kuiga mfano wa mkoa wa Ruvuma kwa kuwa ni njia mojawapo ya kuelimisha jamii umuhimu na kuyaweka vizuri maeneo ya kihistoria yaliopo kusini mwa nchi ili yaweze kutumika katika kutolea vielelezo vya historia ya nchi na kuvutia watalii wengi na hatimaye kutoa ajira kwa watanzania.

Katika hatua nyingine waziri Kagasheki ametoa rai kwa watafiti,wadau na wanajamii wote kufanya utafiti wa habari za  Mama Mkomanile ili taarifa zake zifahamike kwa watu wengi kwa kuwa  alikuwa mwanamke pekee wa mashujaa wa vita vya  Majimaji.

Awali Bi.Eliwasa Maro kaimu mkurugenzi mkuu wa shirika la makumbusho ya Taifa la Tanzania alibainisha kuwa maadhimisho ya tamasha la kumbukizi ya vita vya Majimaji na utalii wa utamaduni kitaifa yamekuwa yakiadhimishwa kila mwaka Februari 27 ambapo dhana ya maadhimisho hayo ni kuchochea mabadiliko ya kifkra na kiutamaduni kwa jamii.

“Makumbusho ya Taifa yamekabidhiwa jukumu la kuendesha kituo cha makumbusho ya Majimaji tangu mwaka 2010,makumbusho haya yanasaidia wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa sherehe za maadhimisho ya kumbukizi zinafanyika kila mwaka zikihusisha dhana nzima ya ukusanyaji,utunzaji na utoaji wa elimu kwa jamii’’,alisisitiza.

Maro amebainisha zaidi kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamelenga katika kuhakikisha kuwa kumbukizi za vita vya majimaji zinakuwa kichocheo cha mabadiliko kwa jamii kifikra na kiutamaduni  ambapo amehimiza kumbukizi hizo ziwe endelevu kwa ajili ya kusaidia urithi za Taifa kwa ajili ya vizazi vya sasa  vijavyo.





Mkurugenzi na mhifadhi kiongozi wa makumbusho ya Taifa ya Majimaji ya Songea Balthazar Nyamusya akzungumzia umuhimu wa makumbusho hayo anabainisha  kuwa baada ya vita vya Majimaji viongozi na askari walioshiriki katika vita hivyo walikamatwa na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa ambapo Februari 27,mwaka 1907 ilikuwa ni siku ya masikitiko makubwa kwa watu wa mkoa wa Ruvuma baada ya watu zaidi ya 60 kunyongwa kwa sababu ya kushiriki katika vita vya majimaji.

Mashujaa hao walinyongewa nyuma ya eneo ambalo hivi sasa linajulikana kwa jina la Songea Club,baada ya kunyongwa miili ya mashujaa hao ilizikwa katika kaburi la halaiki,lililoandaliwa na wafungwa kwa muda wa miezi miwili,siku ya tatu baadaye chifu wa kabila la wangoni  Songea Mbano alinyongwa na kuzikwa katika kaburi  la pekee yake ambapo inaaminika alizikwa kiwiliwili baada ya kichwa chake kukatwa na wajerumani na kukipeleka.

Hata hivyo mhifadhi kiongozi huyo anasisitiza kuwa eneo la Mahenge walilozikwa mashujaa hao ni muhimu katika historia ya mtanzania ndiyo maana mara baada ya uhuru mwaka 1961 baadhi ya wazee walianzisha harakati za kuwakumbuka mashujaa hao pamoja na kuanza kufanya maombi ya kimila katika eneo hilo walilonyongewa mashujaa hao.



 Kwa mujibu wa Nyamusya,Makumbusho ya vita vya majimaji kama yalivyo makumbusho mengine ya kihistoria ni chombo cha kuelimisha jamii kuhusu mambo muhimu ya kujivunia ya Taifa,makumbusho ya majimaji ni historia nzuri na kiburudisho pamoja na kuwa chombo cha kujenga hamasa ya kujiamini kama Taifa na kuimarisha umoja,kuheshimiana na kuishi kwa amani.

 Utafiti umebaini kuwa Makumbusho ya Taifa ya majimaji ndiyo makumbusho pekee nchini ambayo inamiliki  vifaa halisi na zana halisi za jadi ambazo zilitumiwa  na wazee wa jadi katika mambo mbalimbali.

“Mimi nimefanya kazi katika makumbusho ya Taifa Dar es salaam hakuna zana halisi za jadi kama makumbusho ya majimaji,hivyo nadiriki kusema majimaji ni makumbusho pekee nchini yenye zana hizi ukiondoa makumbusho ya Ujerumani ambayo ina vifaa halisi ambavyo vilitumiwa wakati wa vita vya majimaji”,anasisitiza mhifadhi huyo.

Hata hivyo utafiti umebaini kuwa makumbusho nyingi zimekosa vifaa kwa kuwa vilichukuliwa  na kuondoka navyo watawala na kwamba katika makumbusho hayo kilichofanyika ni kutafuta vifaa ambavyo vinafanana na sio halisi  kama makumbusho ya majimaji.

 “Hili ni jambo la kihistoria na ni utalii wa kiutamaduni ambao watalii wengi wa ndani na nje ya nchi watapenda kuja katika makumbusho haya na kujifunza,kuona vifaa na zana halisi zilizotumika ambavyo vimehifadhimiwa katika majengo ya makumbusho ya Taifa ya Majimaji”,anasisitiza.

Makumbusho ya mashujaa wa vita vya majimaji yalijengwa mwaka 1980 lengo lilikuwa ni kutunza hadhi ya sehemu ya makumbusho ya majimaji, shinikizo la ujenzi wa majengo hayo lilitolewa na  kauli ya Baba wa Taifa mwalimu Julius Nyerere kwenye mkutano wea TANU mwaka 1958.

Nyerere aliagiza ijengwe minara katika mikoa yote nchini kwa ajili ya heshima ya kuwaenzi mashujaa wa ukoloni ambao ndiyo chimbuko la kupigania uhuru ambapo tafiti unaonesha kuwa katika maeneo mengine ya nchi walishindwa hata kujenga minara ya mashujaa ambapo Baba wa taifa mwaka 1965 alisisitiza na kukumbushia kile alichoahidi kujenga minara mwaka 1958 sasa kila mkoa ujenge minara hiyo ya mashujaa.

“Mkoa wa Lindi  umejenga mnara mwaka 2008 tena kwa shinikizo la chuo kikuu cha Dar es salaam ambapo mnara huo umejengwa katika eneo la Nandete ndiyo maana nasema Songea ndiyo pekee ambapo katika makumbusho ya Songea zimejengwa sanamu mbalimbali za wapiganaji ambao alikuwa nao chifu Songea Mbano kwenye Baraza lake kupambana na wakoloni’,anasema mhifadhi wa makumbusho ya taifa Philipo Maligissu.

albano.midelo@gmail.com


No comments:

Post a Comment