Na Albano Midelo
WATU wanaoishi katika wilaya ya Songea, mkoani
Ruvuma wapo katika hatari ya kukumbwa na magonjwa mbalimbali na hata kupoteza
maisha kutokana na kutumia maji ya mto ya Luhira ambao umechafuliwa kwa kemikali mbalimbali.
Luhira ni
chanzo cha mto Ruhuhu ambao unamwaga maji yake ziwa Nyasa, mto Luhira unaanzia
kwenye milima ya Matogoro iliyopo nje kidogo ya mji wa Songea,milima hiyo pia
ni chanzo cha mito Ruvuma na Luegu ambayo inamwaga maji yake bahari ya Hindi. Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Songea
(SOUWASA) inategemea chanzo cha maji cha mto Luhira kwa ajili ya kusambaza maji
kwa wakazi zaidi 180,000 wa mji wa
Songea.
Katika
chanzo hicho wakulima wanalima nyanya, karoti, chainizi,spinachi,mboga za
maboga pamoja na mboga nyingine ambapo hupulizia madawa ya kuuwa wadudu
waharibifu ambayo ni hatari kwa afya na baadhi yake yamepigwa marufuku
kimataifa yakiwemo bluecopper, redcopper, DDT na kimatila.
![]() |
| Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu |
Wakulima
wadogo kutoka katika vijiji vinavyozunguka milima ya Matogoro vikiwemo vijiji
vya Mahiro, Matogoro, Ndilima, Chemchem,Mletele na Kikunja ndiyo wanaoendesha
kilimo cha bustani na kupulizia madawa ambayo ni hatari yakitumika jirani na vyanzo vya maji.
Uchunguzi
umebaini kuwa nguvu walionayo wanasiasa kuanzia ngazi ya kijiji, kata hadi juu
ndiyo inachangia kilimo kwenye vyanzo vya maji kuendelea kwa kuwa wataalamu
licha ya kuzuia kilimo hicho wamezidiwa nguvu na wanasiasa hali ambayo
imesababisha kunyamaza kuhofia kuharibu kazi.
Christopher
Michael ni daktari wa mimea,binadamu na
wanyama ambaye anafanya utafiti wake mkoani Ruvuma kuhusu athari zinazotokana
na uchafuzi wa maji anasema kupulizia kemikali jirani na vyanzo vya maji zinasababisha magonjwa zaidi ya 30 kwa
binadamu wanaokunywa au kula vyakula vilivyoathirika na kemikali hizo.
Ameyataja
baadhi ya magonjwa ambayo mtu anaweza kuugua kwa kunywa au kula kemikali kuwa
ni ugonjwa wa ini,saratani ya damu, figo, ngozi,kuoza sehemu za siri, kupata
mzio,kiharusi, kuoza mapafu, macho, magonjwa ya kuhara, amiba, kichocho na kuvimba tumbo ambapo magonjwa huanza
kujitokeza kati ya miezi mitatu hadi miaka 15.
Kwa
mujibu wa Dk.Michael dalili za mtu ambaye ameathirika na matumizi ya kemikali
zenye sumu ni magonjwa ya ngozi, kung’oka kwa kucha, kupungukiwa nguvu za uzazi
kwa wanaume,kope kuwasha na na macho kupoteza uwezo wa kuona,kuungua chembechembe
hai za damu, kuoza mapafu, kuharibika figo, kukosa hewa kwenye ubongo, kupoteza
fahamu na matatizo ya akiri.
“Kemikali
kama bluecopper ikiingia mwilini hakuna dawa za kuweza kuiondoa ,kinachofanyika
hospitalini ni mtu ambaye anakuwa na dalili kwa mfano za kupoteza fahamu
anapewa dripu la maji ,tatizo la vyanzo vya maji kuathirika na kemikali zenye
sumu lipo kila mahali, kinachotakiwa ni kutoa elimu ya kutochafua maji kwenye
vyanzo ’’,anasisitiza Dk.Michael.
Anasema
tangu afike mkoani Ruvuma mwezi Juni 2010
amewabaini wagonjwa zaidi ya 1500
ambao wana dalili zote za kuathirika na madawa ya kemikali nzito zenye sumu
yaani heavy metals na tayari ametoa tiba mbadala na elimu kwa baadhi ya wagonjwa.
Abel Mapunda ni mratibu wa afya na mazingira
hospitali ya misheni Peramiho Songea, anabainisha kuwa matumizi ya kemikali
nzito kama vile zebaki na bluecopper
kwenye vyanzo vya maji yanatakiwa yaepukwe kabisa kwa kuwa kemikali hizo
zinaingia moja kwa moja kwenye maji na zina madhara makubwa kwa afya ya
binadamu na viumbehai.
“Heavy
metals zinaleta matatizo makubwa kwenye mfumo wa fahamu hadi kwenye
ubongo,katika hospitali ya misheni Peramiho tumekuwa tunapokea wagonjwa ambao
wanakuwa wameletwa wakiwa wamepoteza fahamu, tunapowachunguza na kuwapima magonjwa ya malaria, UKIMWI na uti wa mgongo tunakuta
hawana magonjwa hayo’’,anasema .
Hata hivyo anabainisha kuwa utafiti wa awali
unaonesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wagonjwa hao wameathirika na heavy metals
,hata hivyo ili kuthibitisha kuwa wagonjwa hao wameathirika na kemikali hizo
inatakiwa kufanya utafiti zaidi kwa wagonjwa .
Uchunguzi
unaonesha kuwa Katika chanzo cha maji cha Luhira wakulima wanaendelea kulima nyanya, kabichi,
nyanyachungu, mboga za maboga,mchicha na karoti wakitumia mbolea za
chumvichumvi aina ya SA,CAN na NPK pamoja na madawa ya kuuwa wadudu aina ya
bluecopper kimatila,DDT,theonix,sumithion,karate,selecrone.
Madawa
mengine ambayo wakulima hao wanatumia kupulizia kwenye nyanya kwa lengo la
kuzuia ugonjwa wa ukungu ambao unakausha nyanya ni nidithane, milthane, Bravo, rido,ridomil,victory,farmazeb,helicozeb,mancozeb
na lincomil.
Msimamizi
wa chanzo cha maji cha mto Luhira Swalehe Kinana anasema wakulima katika chanzo
cha mto Luhira licha ya kwamba wengi wameanza kuogopa kulima baada ya kuanza
kuchukuliwa hatua za kisheria, hata hivyo bado wanalima ambapo mwaka huu
wamelima eneo lenye ukubwa wa kilometa nne kando kando ya chanzo hicho cha maji.
“Wakulima
hawa bado wanaendelea kutumia kemikali hatari kwenye vyanzo vya maji na huwa
wanapulizia kemikali hizo kuanzia mwezi
Desemba hadi Agosti kila mwaka miezi ambayo kuna wadudu wengi waharibifu wa
mimea,miezi ambayo huwa hawatumii dawa hizo ni kuanzia mwezi Septemba hadi
Novemba tu’’,anasisitiza.
Josephat
Maliselo ni mdhibiti wa ubora wa maji na viwango kutoka SOUWASA anasema kemikali aina ya
bluecopper na redcopper zinapoingia kwenye chanzo cha maji cha mto Luhira
,zinaingia na kupenya moja kwa moja kwa kuwa
hawana vifaa vya kuzuia kemikali hizo
kuingia kwenye maji ambayo yanatumiwa na wakazi wa mji wa Songea jambo
ambalo linaweza kuathiri afya za watumiaji.
Maliselo
ambaye ni daktari wa maji wa SOUWASA anaongeza kuwa maabara yao ya maji iliyopo Songea haina
mashine ya kupima na kutambua kemikali za blue coper au red
copper ambazo zimeingia kwenye maji na kwamba hapa nchini mashine ambazo
zinaweza kupima zipo maabara ya wizara ya maji ,Mkemia mkuu, na chuo kikuu cha
Dare s salaam.
Meneja wa
ufundi wa SOUWASA mwandisi John Kapinga
anabainisha kuwa uharibifu na
uchafuzi unaofanywa kwenye chanzo cha maji cha mto Luhira unachangia kupunguza
kiasi cha maji yanayoweza kutiririka kutoka milima ya Matogoro pamoja na maji
yanayosukumwa kutoka Luhira darajani.
Anasema mamlaka yake katika kipindi cha
kuanzia mwezi wa Septemba hadi Desemba kila mwaka inakabiliwa na uzalishaji
mdogo wa maji na kusababisha mgawo mkali wa maji kwa wananchi wa mji wa Songea
kutokana na uharibifu unaendelea kufanywa na wananchi katika vyanzo vya maji
vilivyopo katika milima ya Matogoro hususani kwenye chanzo cha maji cha mto
Luhira .
Charles Haule,Oliver Mbilinyi na Alois Haule
ni baadhi ya wakulima ambao wanalima bustani katika vyanzo vya maji katika
vijiji vya Mahiro na Chemchem wamekiri kulima katika vyanzo vya maji pamoja na
kutumia kemikali za sumu na kueleza kuwa wanatumia kemikali hizo kwa uzoefu tu
kwa kuwa hawana elimu ya athari za mazingira zinazotokana na kemikali hizo
ambazo wanazitumia kila mwaka.
“Sisi
wakulima tunaozunguka milima ya Matogoro tunalima kahawa ambayo tunapulizia
dawa aina ya bluecopper ambayo wakati wa masika inachuruzika na kuingia kwenye
vyanzo vya maji vilivyopo Matogoro hatujui serikali imedhibiti kitu gani kwa
kutuzuia kulima bustani’’,alihoji mkulima John Nchimbi wa Mahiro.
Luis
Ngonyani ni mtaalamu wa mimea kutoka kampuni binafsi ya RAPCO anasema matumizi ya dawa ya kahawa aina ya
bluecopper karibu na vyanzo vya maji ni
hatari kwa kuwa wakati wa masika dawa hizo zinachurizika na kuingia moja kwa
moja kwenye vyanzo vya maji.
Meneja wa
maji Bonde la ziwa Nyasa Witgal Mkondora anasema bonde hilo linahusika na
kuulinda mto Luhira ambapo amekiri bonde
kupata changamoto ya kushindwa kuwadhibiti wakulima wanaolima jirani na chanzo
cha mto huo kutokana na wakulima kupenda kulima katika maeneo oevu ambayo yana
rutuba nyingi na maji ya kumwagilia.
Hata
hivyo Mkondora anabainisha kuwa sheria
ya mazingira namba 57 ya mwaka 2004 inataka shughuli za kibinadamu kufanyika
umbali wa meta 60 kutoka katika kingo za mto na kwamba wote wanaolima kando kando ya mito wanafanya makosa na wanatakiwa kuchukukuliwa
hatua za kisheria.
“Siku ya
Jumanne na Alhamisi tunafanya operesheni ya kuwakamata wote wanaolima katika
bonde la mto Luhira lenye ukubwa wa hekta 15,000 tumeshawakamata watuhumiwa kadhaa kutoka kata
za Matogoro,Mletele na Ndilima ambao walikuwa wanalima bustani ndani ya chanzo
cha mto, kesi zao zipo mahakamani’’,anasema.
Sera maji
ya mwaka 2002 inalenga kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vilivyopo
vinatunzwa,kulindwa na kuendelezwa kwa utaratibu unaozingatia uwiano wa
mahitaji ya viumbehai wote
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129


No comments:
Post a Comment