Wanafunzi 30,063 waliopata daraja
sifuri katika matokeo yaliyopita, wameula baada ya kupandishwa hadi daraja la
nne kutokana na ukokotoaji upya wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne
yaliyofanywa na Baraza la Mitihani la Taifa (Nacte) na kutangazwa jana.
Marekebisho hayo yalifanyika baada
ya kufutwa kwa matokeo ya awali yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu.
Kufutwa kwa matokeo hayo, ilikuwa ni
utekelezaji wa sehemu ya mapendekezo ya Tume iliyoundwa na Waziri Mkuu Mizengo
Pinda, baada ya wanafunzi 240,909 kupata daraja sifuri kwenye matokeo
yaliyotangazwa mara ya kwanza.Akitangaza matokeo hayo, Waziri
wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alisema sasa watakaokuwa na
sifuri ni 210,846 sawa na asilimia 56.92 wakati wavulana wakiwa ni 104,259 na
wasichana 106,587.
Hiyo ina maana kuwa sasa ufaulu
umepanda na kuwa asilimia 43.08 badala ya ule wa kwanza ambao ulikuwa asilimia
34.5.Dk Kawambwa alisema kutokana na
ukokotoaji mpya wa matokeo ya sasa, idadi ya wanafunzi waliofaulu mtihani huo
kwa daraja la kwanza mpaka la nne imeongezeka na kufikia wanafunzi 159,747
kutoka 126,847.
Wanafunzi waliopata daraja la kwanza
ni 3,242 wavulana wakiwa ni 2,179 na wasichana 1,063 ikiwa ni asilimia 0.88 ya
matokeo yote, daraja la pili ni 10,355 sawa na asilimia 2.8 wavulana wakiwa
7,267 na wasichana 3,088.
Waliopata daraja la tatu ni 21,752
sawa na asilimia 5.87 wavulana wakiwa 14,979 na wasichana 6,773, daraja la nne
ni 124,260 sawa na asilimia 33.54 .
Tofauti na matokeo yaliyofutwa,
ambayo watahiniwa waliopata daraja la kwanza walikuwa ni 1,641, wavulana wakiwa
1,073 na wasichana 568, daraja la pili ni 6,453, wavulana wakiwa 4,456 na
wasichana 1997.
Waliopata daraja la tatu walikuwa
15,426, wavulana 10,813 na wasichana 4,613, waliopata daraja la nne 103,327,
wavulana 64,344 na wasichana 38,983 huku waliopata sifuri wakiwa 240,903,
wavulana 120,664 na wasichana 120,239.
Dk Kawambwa alieleza watahiniwa
waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa ni 480,029 na waliofanya ni 458,139
sawa na asilimia 95.44.
Alisema kuwa watahiniwa wa shule
waliosajiliwa kufanya mtihani huo walikuwa ni 411,225 na waliofanya ni 397,138
sawa na asilimia 96.57 huku wa kujitegemea wakiwa ni 68,804 na waliofanya ni
61,001.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI

No comments:
Post a Comment