Wednesday, May 29, 2013

Ngoma ya sakamimba chanzo cha wanafunzi kuolewa



Wananchi  wakiwemo wanafunzi wakikimbilia ngoma ya sakamimba Tunduru
Na Albano Midelo
MAFUNZO ya unyago,msondo na ngoma ya sakamimba yanayofanywa na kabila la wayao wilayani Tunduru mkoani Ruvuma yamesababisha idadi kubwa ya wanafunzi wa kike katika shule za msingi na sekondari kukatishwa masomo kwa  kuolewa.Utafiti wa kina ambao umefanywa katika   za  sekondari za Frankweston, Mgomba, Tunduru, Mataka, Namwinyu, Lukumbule na Nalasi wilayani Tunduru umebaini kuwa karibu nusu ya wanafunzi wa kike katika shule hizo wameacha masomo yao baada ya kupata mimba na kuolewa  hali ambayo imechangia wilaya hiyo kuwa ya mwisho kitaaluma katika mkoa wa Ruvuma katika elimu ya msingi na sekondari.

Azizi Saidi mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Frankweston  anasema utamaduni wa kufanyiwa unyago umesababisha wanafunzi  wa kike wake kupata mafunzo hayo na kujiona kwamba wapo tayari kuolewa hata wakiwa bado shuleni hali ambayo inasababisha wanafunzi wengi wa kike kuacha masomo.

“Sisi ambao hivi sasa tupo kidato cha nne tunaohudhuria darasani  ni chini ya wanafunzi 100, tulipoanza kidato cha kwanza mwaka 2010 tulikuwa wanafunzi zaidi ya 240,wanafunzi wengi wa kike waliofanyiwa utamaduni wa unyago na msondo wameacha shule kwa kuolewa au kupata mimba’’,alisema.

Salima Sefu mwanafunzi sekondari ya Frankweston  ameomba mila hizo alizodai kuwa ni potofu ni vema serikali ingezitazama upya kwa kuwa wanafunzi wengi wanaolewa wakiwa wadogo bila kuwa na uwezo wa kulea familia hali ambayo pia imechangia ndoa nyingi kuvunjika na kusababisha watoto wao kulelewa na mzazi mmoja .

Hemed Ally mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya Frank Weston akizungumzia mila ya msondo na unyago anasema wanafunzi wa kike baadhi ya mambo ambayo wanafundishwa hayalingani na umri wa wanafunzi kwa kuwa ni mambo ya ndoa namna ya kuishi na wanaume yanayowahusu watu wazima.

Anasema katika mafunzo hayo wanafunzi wa kike wanaelezwa faida za kuishi na mume lakini hawafundishwi madhara ambayo wanaweza kupata kwa kushiriki katika ndoa wakiwa wadogo hali hiyo ndiyo inawahamasisha wanafunzi kujiingiza kwenye ngono na kushawishika kuolewa wakiwa wanafunzi.

“ mimi kama mwanafunzi wa kike nashauri mila hizi ziachwe,hata hivyo wazee wa mila za msondo na unyago hawapo tayari  mila hizo kuachwa kwa kuwa wanaamini zinafundisha malezi kwa watoto wa kike na wapo tayari kupambana na mtu yeyote ambaye anazipiga vita mila na utamaduni huo ’’,

Katika kijiji cha Nalasi wilayani Tunduru mtoto wa kike ambaye ameshavunja ungo anatolewa katika nyumba ya wazazi na kujengewa au kupewa chumba cha pekee yake na kwamba mtoto huyo anakuwa huru kufanya lolote na kurudi nyumbani majira yeyote bila kuulizwa na mlezi au mzazi wake hali hiyo imechangia kuongezeka kwa mimba utotoni na utoro wa kudumu.

 Rehema Sara mwanafunzi wa kidato cha nne sekondari ya Mgomba  anasema mila za unyago na msondo zimesababisha wanafunzi wengi wa kike katika shule hiyo kuacha masomo kwa kupata mimba au kuolewa ambapo hivi sasa katika darasa lao waliofanikiwa kufika kidato cha nne ni wanafunzi 106 tu kati ya wanafunzi zaidi ya 230 walioanza nao kidato cha kwanza.

“ Mimi nilifundishwa mila na desturi za msondo na unyago nikiwa darasa la kwanza mambo ambayo  hayafai kusema ni matusi tangu nilipofundishwa hadi sasa sijasahau ,hizo mila walitakiwa kufundisha malezi pekee na sio mambo ya ndoa ’’,alisisitiza Mariam Jafari mwanafunzi wa kidato cha pili sekondari ya Mgomba.

Sala mkombozi wa kidato cha nne sekondari ya Mgomba ambaye alifanyiwa ngoma ya unyago na msondo akiwa darasa la tatu amekiri baadhi ya mambo wanayofundishwa ni mazuri kwa ajili ya malezi lakini kuna mengine hayafai kwa kuwa wanafundishwa  namna ya kuishi na mume jambo ambalo ni hatari kwa wanafunzi.

Mimi wenzangu wengi ambao nilikuwa nao shule na msingi na wengine ilitakiwa niwe nao katika shule ya sekondari wameacha masomo kwa kuwa wana watoto baada ya kupata mimba na wengine wameolewa na kuachika hivyo wanaangaika na maisha kwa kuwa waliingia kwenye maisha ya ndoa katika umri mdogo.

Sharifa Hamisi mwanafunzi wa kidato cha nne sekondari ya Mataka  anasema mila za msondo na unyago ndiyo chanzo kikuu cha mimba na wanafunzi kuolewa tofauti na siku za nyuma walikuwa wanafundishwa zaidi maadili mema wakiwa na umri wa kuanzia miaka 18 lakini hivi sasa  watoto wa kike wanafundishwa katika umri mdogo kuanzia darasa la tatu.

Hawa Mponda mwalimu shule ya msingi Mlingoti anadai mila za msondo na unyago hivi sasa watoto wadogo kuanzia darasa la kwanza wanaingizwa kwenye mafunzo ya unyago namna ya kuishi na wanaume hali ambayo wanapoendelea kukua wanafanya majaribio na kuleta athari za mimba na kuolewa wakiwa wanafunzi.

Hassan Musa mkuu wa shule ya sekondari Frankweston anasema kipaumbele kwa wakazi wa wilayani Tunduru ni mila za msondo,unyago na jando hali ambayo inasababisha utoro,mimba na wanafunzi kuolewa hali ambayo imechangia kushusha elimu katika wilaya.

“Mimi nimefundisha katika shule mbalimbali za wilaya ya Tunduru,ukitembelea vijijini utabaini kuwa ndoa nyingi zimevunjika na hivi sasa watoto wanalelewa na mzazi mmoja ambaye ni mama,mwanamke anaweza kuolewa zaidi ya mara moja na kuachwa hivyo mama anakosa uwezo wa kumlea na kumsomesha mtoto wake hivyo mtoto kujiingiza kwenye mapenzi na kupata ujauzito’’,alisema.

Elice Mapunda mkuu wa sekondari ya Mgomba amekiri tatizo la mimba kwa wanafunzi kuwa kubwa katika shule za sekondari  na kwamba hali hiyo inatokana na watoto wa kike kuwaficha wanaume ambao wamewapa mimba na kwamba hata hivyo mimba zinaendelea kupungua.

“Mimi ni mngoni wa Songea lakini nimezaliwa Tunduru,nina rafiki zangu wamechezwa msondo na unyago, lakini hivi sasa wamesoma hadi kiwango cha kuwa na shahada mimi sikubaliani sana kuwa mila na desturi hii  ndiyo chanzo cha mimba za utotoni,kwanza watoto wa kike waliopitia mafunzo hayo kikamilifu hawasemi nini wanajifunza huko,hao wanaosema nani amewaruhusu kusema’’,alihoji.

Hadija Said mwalimu wa malezi na ushauri nasaha katika sekondari ya Mataka amekiri shule hiyo mara kadhaa kukabiliwa na mimba za utotoni,utoro wa kudumu na kuolewa wakiwa bado wanafunzi na kwamba mila ya msondo na unyago zamani ilikuwa inafanyika lakini idadi ya wanafunzi waliokuwa wanapata mimba mimba za utotoni na kuolewa haikuwa kubwa kama ilivyo sasa.

Flavian Nchimbi  kaimu afisa  elimu msingi wilaya ya Tunduru anasema tatizo la mimba katika shule za msingi zimepungua ukilinganisha na miaka mitatu nyuma kulikuwa na mimba karibu 250 ambapo takwimu za mwaka jana zinaonyesha kuwa katika shule za msingi zililipotiwa mimba 16 na kwamba kuanzia mwezi Januari hadi Aprili mwaka huu imeripotiwa mimba moja tu.

Kwa mujibu wa Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wasichana 8000 kila mwaka huacha shule kutokana na ujauzito. Kati yao 3,000 ni wanafunzi wa shule za msingi.

Kila siku, wanawake 24 hufariki dunia kutokana na mimba au wakati wa kujifungua. Wanawake watano mpaka sita wanaofariki kati ya hao ni watoto wadogo, watoto hao hufariki dunia kwa kuwa miili yao haijakomaa vya kutosha kwa ajili ya kujifungua.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho amekiri mila na desturi za kabila la wayao zinachangia wilaya hiyo kuwa duni kielimu ambapo amesema tayari serikali imeunda kikosi kazi cha kuonana na viongozi wa mila, makungwi na manyakanga kuwaelimisha juu ya utoaji wa elimu kwa watoto wa kike kupenda masomo.

 “Binti aliyechezwa unyago ukimuuliza umefundishwa nini anasema tumekatazwa kusema tulichofundishwa,ina maana mtu anayeweza kumsikiliza na kumkubali ni kungwi ambaye ndiye mwalimu wake wa unyago kwa hiyo sisi kama serikali tukiwaelekeza wanaweza kutusaidia kuwasisitizia hao watoto umuhimu wa elimu wakati wanawapa elimu ya jando na unyago”anasema.





 
















No comments:

Post a Comment