Sunday, May 26, 2013

Mapacha watano wafariki,waliishi kwa masaa kumi tu



Na Albano Midelo
Dk.Benedict Ngaiza akiwa ofisini kwake Songea
    
WATOTO  wote pacha watano waliozaliwa mwishoni mwa wiki katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma wamefariki usiku wa kuamkia jana .

Watoto hao wote watano walizaliwa salama na Sophia Mgaya (28) mkazi wa Ruhuwiko mjini hapa  kwa kufanyiwa upasuaji  katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma.

Mganga mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya mkoa Songea(HOMSO)Dkt. Benedict Ngaiza, alisema kuwa watoto hao wameishi kwa masaa kumi tu na kufariki dunia kutokana na  kuzaliwa na uzito mdogo wa chini ya kilo moja.

Dkt.Ngaiza  alibainisha kuwa watoto wote wanaozaliwa wakiwa na uzito mdogo wanakuwa na maisha mafupi,hata hivyo alisema hali ya mama wa watoto hao inaendelea vizuri ingawa bado amelezwa katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma akiendelea kupata matibabu..

Tukio ambalo halijawahi kutokea katika hospitali ya mkoa wa Ruvuma  limetokea Mei 24 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi  huku mtoto wa kwanza akiwa na uzito wa gramu 730,wa pili 810,watatu 670,wanne 820 na watano gramu 430.


Kulingana na mganga huyo kati ya watoto hao waliozaliwa,watatu ni wa kiume na wawili ni wa kike  na kwamba huu ulikuwa ni mzao wa pili kwa mwanamke huyo.

Alieleza kuwa katika mzao wa kwanza wa mama huyo alifanikiwa kujifungua mtoto mmoja na katika mzao wa pili  amebahatika kujifungua watoto hao watano ambao wote wamefariki dunia .

 Wakati huo huo jeshi  la Polisi mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na Askari Wanyama Pori linamshikilia mtu mmoja  kwa tuhuma za kukamatwa na pembe za ndovu 11 zenye thamani ya shilingi milioni 38.8.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma Deusdedit Nsemeki,alisema tukio hilo lilitokea  hivi karibuni  huko katika kijiji cha Mandepwende Wilayani Namtumbo.

Nsemeki alimtaja mtu aliyekamatwa kuwa ni Issa Omar Mayono(57)mkazi wa Namtumbo na kudai kwamba alipatwa na mkasa huo baada ya Askari mwenye namba 8057 D/SSGT Amily,akiwa doria na askari wanyama pori ambao ni Joseph Luben(43) Daud Tesha(30) na Joseph Abdalah(57) wote wakazi wa Msamala mjini Songea.

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na Nyara hizo za Serikali zilizokuwa na uzito wa kilogram 42.6 wakati akiwa anasafirisha kutoka  porini katika kijiji cha Mandepwende kuelekea  mjini Namtumbo.

Matukio ya kukamatwa kwa nyara za Serikali katika mkoa wa Ruvuma yamekithiri kutokana na watu wengi wasiokuwa na maadili na kufuata sheria kuuwa wanyama bila ya kuwa na vibali jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Mwezi mmoja uliopita kampuni ya Game Frontiers Tanzania(GFT) inayojishughulisha na uwindaji wilayani Namtumbo kwa kushirikiana na kikosi cha askari wanyamapori katika pori la akiba la Selous, walifanikiwa kukamata pembe za ndovu 15 zenye thamani ya  shilingi milioni 192.

Kamanda huyo wa polisi alisema mtuhumiwa anatarajia kufikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi wa shitaka hilo kukamilika ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.
albano.midelo@gmail.com



No comments:

Post a Comment