Saturday, May 25, 2013

Askofu mkuu mtega awaaga waumini,wengi wamlilia



Na Albano Midelo
Askofu mkuu mstaafu Norbert Mtega akiwaaga waumini

ASKOFU mkuu mstaafu wa jimbo kuu la Songea Norbert Mtega amewaaga rasmi waumini wake katika kanisa kuu la kiaskofu la  jimbo kuu la Songea baada ya kustaafu majukumu ya uaskofu tangu Mei 15 mwaka huu.

Askofu mkuu mstaafu Mtega alitumia misa zote tatu Jumapili hii katika kanisa hilo kuwaaga rasmi maelfu ya waumini ambao walikusanyika kwa wingi ndani na nje ya  kanisa hilo huku baadhi yao wakiwa na majonzi hali iliyosababisha  baadhi ya akinamama  kutokwa na machozi kutokana na kile walichodai kuwa alikuwa ni msaada mkubwa kimwili na kiroho.

Akihubiri katika kila adhimisho la misa takatifu Askofu mkuu mstaafu Mtega ambaye amekuwa askofu mkuu jimbo kuu la Songea kwa miaka 22 alisema aliamua kuandika barua ya kuomba kustaafu kwa Baba mtakatifu kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kiafya .

“Ndugu zangu waumini nipo hapa leo katika adhimisho la misa hii kwa namna ya pekee nitoe ushuhuda kwenu,nimemaliza kazi yangu hapa Jumatano Mei 15 kama kiongozi lakini kama Askofu ningali bado kazini,bado nipo kati yenu kama mwanasongea, mtu wa imani ya kanisa katoliki na mimi ni muumini mwenzenu’’,alisisitiza.


Hata hivyo alisema katika uongozi wake wa miaka 22 akiwa Askofu mkuu wa jimbo kuu la Songea ameshuhudia utendaji wa ajabu wa roho mtakatifu ndani ya wahudumu na waumini wote wa kanisa hilo na kusisitiza kuwa chochote ambacho kimetendeka katika jimbo hilo kwa miaka 22 ambayo yeye alikalia kiti hicho mtendaji mkuu amekuwa mtu asiyeonekana ambaye ni Mungu roho mtakatifu.

“Kanisa ni la Mungu roho mtakatifu,kila kauli na mkakati ni wa roho mtakatifu,mimi nikiwa  katika kiti hicho kwa miaka 22 imeshuhudia mapadre,watawa na waumini wanavyotenda kazi ,nasema hayo yote ni matendo makuu ya Mungu,kwa hiyo leo ninapowaaga wajibu wangu ni kusema asifiwe na kutukuzwa Mungu,nawaomba tuungane katika neno la imani la kumshukuru na kumtukuza Mungu kwa matendo yake makuu’’,alisema.

Katika nafasi hiyo Askofu mkuu mstaafu Mtega amekiri kuwa watendaji wakuu katika kipindi chote walikuwa ni waumini ambao wamewezesha jimbo kuu la Songea kusimama kiimani kwa kutoa mchango wa hali na mali.

Hata hivyo alisema baada ya yeye kustaafu jimbo linaingia katika kipindi cha mpito hadi hapo atakapopatikana Askofu mkuu mteule wa jimbo kuu la Songea na kwamba katika kipindi hiki cha mpito Baba mtakatifu amemweka askofu wa jimbo la Iringa mhashamu Tarcius Ngalalekumtwa awe msimamizi wa kitume.

Alisema katika kipindi  hiki cha mpito Baba mtakatifu  anaendelea na mchakato wake wa kuandaa, kumteua na kumchagua atakayekuwa askofu mkuu wa jimbo kuu la Songea na kwamba waumini waendelee kusali kwa kuwa askofu mteule atapatikana.

“Nawaomba waumini wote tuingie katika kipindi muhimu cha sala  maombi,matumaini na imani kubwa ili afike roho mtakatifu na kujaa kwa Baba mtakatifu na waumini wote ili tupate askofu mkuu haraka iwezekanavyo, pia nachukua nafasi hii kuwaombeni radhi niliowakosea na mimi nawasamehe wote walionikosea’’,alisema.

Akizungumza kwa niaba ya waumini wa jimbo kuu la Songea Naibu Askofu jimbo kuu la Songea padre Camilius Haule ametoa shukurani za dhati kwa askofu mkuu mstaafu Norbert Mtega kwa kujitoa kwa dhati kulihudumia jimbo kuu la Songea kwa miaka 22 kwa kutoa karama zake zote kwa ustawi wa jimbo hilo.

“Baba askofu mkuu tunakushuru kwa kukubali kwako kujitoa kafara kwa ajili ya kutimiza kazi za Yesu kristo katika ekaristi takatifu,neno la Mungu na sakramenti ya kitubio,umedhihirisha kuwa ni  nabii,kiongozi, mchungaji na kuhani unayejitoa sadaka kwa mfano wa Yesu Kristo’’,alisema.

Padre Haule ameahidi kwa niaba ya waumini kumsindikiza kwa sala askofu mkuu mstaafu Mtega anapokwenda nje ya nchi kwa ajili ya kupata matatibu ili Mungu roho mtakatifu aweze kumponyesha katika maradhi yanayomsumbua hatimaye aweze kurudi jimboni Songea akiwa mzima wa afya.

John Komba mkazi wa Songea amesikitishwa na hatua ya askofu mkuu Mtega kustaafu na kudai kuwa bado kanisa lilikuwa linamtegemea katika majukumu mbalimbali kutokana na kazi kubwa ambayo ameifanya katika kipindi chote cha miaka 22 akiwa askofu mkuu wa jimbo kuu la Songea.

“Askofu mkuu mstaafu Mtega ndiye aliyetufundisha kujitegemea,kabla yake waumini tulikuwa tegemezi tunangojea misaada kutoka kwa wamisionari,hivi sasa tunaweza kujitegemea, waumini wanajenga makanisa wao wenyewe katika hili tutamkumbuka sana’’,alisema Komba.

Njafura Njafura ambaye ameishi mjini Songea tangu miaka 1960,alisema askofu mkuu mstaafu Mtega ameleta mabadiliko makubwa katika jimbo hasa kusimamia elimu kikamilifu ambapo hivi sasa kuna vyuo vikuu vya kanisa ambavyo alivitaja kuwa ni chuo kikuu cha SAUT tawi la Songea na chuo kikuu cha mtakatifu Joseph.

“Mimi binafsi sijisikii vizuri kustaafu kwa askofu mkuu Mtega,nimekosa amani kabisa moyoni,hata hivyo waumini wenzangu nawaasa kumuenzi katika mambo yake  mema  kwa kuyaendeleza ikiwemo sera yake ya kulitegemeza kanisa ambayo amefanikiwa kuieneza katika jimbo kuu la Songea, kuna mifano kadhaa ya parokia mpya ambazo zimeanzishwa na waumini wenyewe ikiwemo parokia ya Mjimwema,Bombambili na Subira na nyinginezo’’,alisema.

Catherine Nchimbi(70) ambaye alitokwa na machozi wakati askofu anawaaga waumini kwa kuwapungia mikono,alisema anasikitika sana kwa kitendo cha baba askofu kustaafu kwa kuwa walikuwa wanamtegemea sana kimwili na kiroho na kwamba kitendo cha kustaafu kwake amekipokea kwa shingo upande.

“Sina namna yeyote kwa kuwa amestaafu na leo anatuaga rasmi,baba huyo alinisaidia sana katika maisha yangu ya kiroho na kimwili,sifahamu kwanini amestaafu ghafla,mbona bado ana nguvu za kuendelea kuwahudumia waumini wa Songea,tunamlilia sana ’’,alisisitiza.

Ally Rashid fundi cherehani mjini Songea anasema askofu mstaafu Mtega alikuwa kiungo muhimu kwa dini zote na kwamba licha ya kuwa yeye ni mwislamu,aanakiri kuwa askofu mkuu mstaafu Mtega ameibadilisha Songea hasa katika sekta ya elimu na afya vitu ambavyo ni muhimu bila kujali wewe ni dini gani.

“Taarifa za kustaafu kwake sio tu zimewashitua wakristo pekee bali hata sisi waislamu tunatambua mchango wake,si unaona hapa leo Jumapili baadhi yao waliposikia kwenye vyombo vya habari hawakuamini hadi leo wamefika kushuhudia anapowaaga waumini rasmi,askofu Mtega alijenga mahusiano mazuri na dini zote’’,alisisitiza.

Julius Konala mwandishi wa habari wa gazeti la Tanzania Daima Songea amewatahadharisha wanahabari kuacha kuandika habari za uzushi kuhusiana na kustaafu kwa Askofu mkuu Mtega badala yake kuandika habari za ukweli kutoka vyanzo  vya kuaminika na zilizofanyiwa utafiti wa kina ili kujiepusha na kashfa.

“Baadhi ya wanahabari wameandika askofu mkuu Mtega amejiuzuru jambo ambalo sio kweli,ukweli ni kwamba askofu mkuu Mtega amestaafu majukumu ya uaskofu lakini uaskofu wake umebakia palepale ndiyo maana hata leo ameongoza na kuhubiri katika kanisa kuu la kiaskofu’’,alisema.





No comments:

Post a Comment