Tuesday, May 21, 2013

Uvutaji sigara unavyoteketeza mamilioni ya watu



Na Albano Midelo
BIDHAA za tumbaku kwa vyovyote itakavyotumika inaleta madhara makubwa kwa mtumiaji ikiwemo kumsababishia maradhi mbalimbali na hata kifo.

Takwimu za shirika la afya ulimwenguni(WHO) za mwaka 2003 zinaonesha kuwa kila baada ya sekunde kumi mtu mmoja hufariki dunia kutokana na maradhi yanayotokana na matumizi ya bidhaa za tumbaku.


Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2025 vifo vinavyotokana na  matumizi ya tumbaku vitaongezeka kwa kiwango cha asilimia 70 na kwamba mwaka 2030 watu milioni 10 watakufa kila mwaka kutokana na uvutaji wa sigara ulimwenguni.

 Kulingana na WHO,asilimia 70 ya  wavutaji hao watatoka katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania ambapo wanaume wanaovuta sigara barani Afrika ni asilimia 36 na wanawake wanaovuta sigara katika Afrika ni asilimia tisa. Hata hivyo hapa nchini inakadiriwa kuwa katika baadhi ya mikoa wanaume wanaovuta sigara ni asilimia 46 na wanawake wanaovuta sigara ni asilimia nne tu.


Wataalamu wa afya wanasema matumizi ya tumbaku yapo ya aina nyingi ikiwa ni pamoja na  kubwia,kunusa,kuvuta na kutafuna ambapo wananchi  wengi katika maeneo ya mijini na vijijini wamekuwa wakitumia tumbaku kwa wingi bila kujua madhara yanayoweza kuwapata kiafya.


Kwa mujibu wa WHO matumizi makubwa ya tumbaku yanaendelea zaidi katika nchi zinazoendelea kuliko zilizoendelea kutokana na juhudi za makampuni makubwa yanayotengeneza bidhaa zinazotokana na tumbaku kupanua wigo wao kibiashara kwa kuweka matangazo mbalimbali.



Kwa mujibu wa wataalam wa afya yapo magonjwa mbalimbali ambayo yanaweza kusababishwa na matumizi ya tumbaku yakiwemo Madhara mengine ya tumbaku na bidhaa zake ni pamoja na kuathirika kwa mimba,mtoto anayezaliwa kuwa mlemavu wa akiri, kupungua kwa nguvu za kiume,vidonda vya tumbo,mtoto wa jicho,kunyonyoka nywele na kuziba kwa mishipa ya damu.



 Matumizi ya  bidhaa za Tumbaku iwe kwa kuvuta au kutafunwa husababisha shinikizo la damu ambalo husababisha ugonjwa wa moyo, kiharusi, puma, matatizo ya kifua,kansa ya mdomo,kansa ya mapafu,kansa ya figo,kansa ya matiti,kansa ya tumbo,kansa ya koo,watoto kuzaliwa na uzito mdogo na kuwa na matatizo ya kiafya ambayo humwezesha mtoto kufa haraka akiwa bado mchanga,matatizo ya meno,uvimbe katika ubongo,ngozi kunyauka.




Kwa mujibu wa wataalamu, tiba ya magonjwa hayo inahitaji gharama kubwa  hali inayosababisha wengi kushindwa kutibiwa kutokana na ukweli kuwa  wananchi wengi ni masikini na hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu hivyo wanaugua na hatimaye kupoteza maisha.



Katika kukabiliana na madhara ya matumizi ya tumbaku,dunia imetenga siku maalum ya kutotumia tumbaku duniani ambayo huadhimisha kila mwaka Mei 31, hata hivyo utafiti umebaini kuwa bado tatizo la matumizi ya tumbaku linaongezeka kwa kasi kubwa katika jamii mwaka hadi mwaka.



Sababu kubwa ya kuendelea kwa matumizi ya tumbaku na bidhaa zake ni wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha  kuhusu madhara ya tumbaku hali inayochangia kuongezeka kwa madhara yatokanayo na tumbaku.





Kutokana na madhara hayo makubwa ya zao la tumbaku na matumizi yake katika jamii,serikali ,wadau na jamii kwa ujumla inatakiwa ishirikiane kwa pamoja kuhamasisha na kuelimisha watumiaji wa tumbaku ili waepuke tabia hiyo na hatimaye kulinda afya yao.



Uvutaji wa sigara ni njia moja kuu ya utumiaji wa tumbaku.Moshi utokanao na jani la tumbaku una sumu kali iitwayo'nikotini' na mvutaji sigara huivuta  sumu hii ambayo huchanganyika na hewa ya sumu ya 'kaboni monoksaidi' na lami ya moshi wa tumbaku



Wataalamu wanabainisha kuwa katika sigara kuna kemikali zipatazo 4000. Kemikali zote hizi kwa pamoja ndizo zinazoleta madhara ya moja kwa moja kwa mtumiaji na kwa watu wengine walio karibu na mvutaji sigara.Nikotini pamoja na kemikali hizo za moshi wa tumbaku uliokwama kwenye njia ya hewa humsababishia mvutaji magonjwa,ikiwa ni pamoja na saratani ya koo,mapafu,kizazi na kipofu cha mkojo.Husababisha pia shinikizo kubwa la damu,vidonda vya tumbo,kikohozi sugu na kubanwa kifua.



Kemikali za sumu zipatazo 4000 zimethibitishwa kuwepo katika jani la tumbaku,na ambazo zikiingia mwilini hata kwa kiasi kidogo tu humsababishia mvutaji na walio karibu naye kuathirika.



Kulingana na wataalamu wa afya, moshi wa sigara humfikia mtu asiyevuta toka kwa mvutaji aliye karibu naye na kumsababishia madhara mbalimbali ikiwa  ni pamoja na kukohoa,kupiga chafya ovyo,kuumwa kichwa au kichefuchefu,kubanwa pumzi.



Utafiti umebaini kuwa tabia ya wazazi kuvuta sigara mbele ya watoto wao ni chanzo cha watoto kuwaigiza na kuanza uvutaji wa sigara mapema ambapo inakuwa vigumu kwa mvutaji kukemea uvutaji,ndiyo maana mara nyingi watoto wa wanaovuta sigara huishia kuwa wavutaji.



Makampuni yanayotengeneza mazao ya tumbaku yakiwemo  ya sigara yanatakiwa yaelimishe wazi wazi bila kificho kuhusu madhara ya sigara kwa watumiaji badala ya kuweka matangazo ya kusifia sigara huku madhara  yakiwa hayajaoneshwa wazi wazi.



Matangazo ya kuandika neno 'ONYO'kwa maandishi yasiyoonekana kwa urahisi juu ya paketi za sigara hayawezi kusaidia jamii kutambua kwa urahisi madhara ya bidhaa za tumbaku.



Matangazo hayo yanachochea matumizi ya tumbaku,licha ya wananchi wengi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa za tumbaku



Baadhi ya nchi ulimwenguni zimeshatunga sheria kali zinazomlinda yeyote atakayeathirika kutokana na matangazo yanayoshawishi jamii kutumia au kuzalisha tumbaku ambapo Kupitia vyombo vya sheria,waathirika hudai fidia ya mamilioni ya fedha ambayo makampuni ya tumbaku hulazimika kulipa fidia hizo.

 Hata hivyo serikali imeanzisha sheria ya udhibiti wa bidhaa za tumbaku kwa ushirikiano na chama cha afya ya jamii Tanzania(TPHA) hali ambayo inaonesha matumizi ya tumbaku yanaweza kupungua hivyo jamii kuwa yenye afya bora.


Wakulima katika maeneo ambayo wanategemea kilimo cha tumbaku kama zao la biashara ni vema sasa wakazalisha zao mbadala la tumbaku kama vile ufuta,paprika alizeti na mazao mengine kulingana na hali ya hewa ya eneo husika ambayo hayana madhara katika afya  na hata soko lake ni kubwa.





















                           

No comments:

Post a Comment