Wednesday, June 26, 2013

Imani za kishirikina zinaimaliza Mbeya,tuchukue hatua

Vikongwe  wanauwawa na kupata ulemavu

Kaburi ambalo watu wawili mmoja akiwa hai walizikwa Chunya
Na Albano Midelo

MIKOA ya Mwanza,Shinyanga na Tabora kwa miaka mingi imekuwa ni vinara  kwa mauaji ya wakongwe kutokana na imani za kishirikina.

 Takwimu za mkoa wa Tabora  pekee  zinaonyesha kuwa   mwaka 2010 kutokana na imani za kishirikna jumla ya watu 392 waliuwawa  ambapo  takwimu za mwaka 2011 zinaonesha kuwa watu zaidi ya 370 waliuwa kutokana na imani za kishirikina kwenye mkoa huo.

 Moto wa imani za kishirikina sasa unasambaa kwa kasi hadi katika mikoa ya nyanda za juu kusini hususani mkoani Mbeya ambapo wakazi wake wanadumisha imani za kishirikina na kusababisha vifo vya wazee wasiokuwa na hatia.Uchunguzi uliofanywa katika tarafa za Songwe na Kwimba wilayani Chunya na Kamsamba  wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya unaonyesha kuwa imani za kishirikina katika maeneo hayo unashamiri na  kuleta maafa makubwa yakiwemo kusababisha vifo,ulemavu na uharibifu wa mali za watu kwa kuwa watuhumiwa uchawi wamekuwa wanachomewa moto nyumba zao na mali zao hivyo kuongeza umaskini katika familia.


Kuchoma moto nyumba athari za imani za kishirikina
Imebainika kuwa baadhi ya vijiji kwenye tarafa hizo wazazi na walezi wameshindwa kuwapeleka watoto wao kupata elimu ya msingi na sekondari  kutokana kuwa na mwamko duni wa elimu hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa jamii ya watu kujiingiza katika imani za kishirikina.

Takwimu za mwaka huu pekee zinaonyesha kuwa matukio ya mauaji ya kutisha yanaendelea kutokea takribani kila mwezi yakitokana na imani za kishirikina zinazochangiwa na idadi kubwa ya waganga wa kienyeji ambao wameweka makazi katika tarafa hizo.

Miongoni mwa matukio mazito ya mauaji yanayotokana na imani za kishirikina ni lile ambalo lilitokea mwezi Aprili mwaka huu  Katekisita  katika Kigango cha Kanisa Katoliki kitongoji cha Maweni Kijiji cha Mkwajuni, Florian Mwachiluwi (70) alikufa baada ya kuzikwa akiwa hai katika kaburi moja na mtu anayedaiwa kumuua kwa njia ya kishirikina Peter Robert.

Marehemu Mwachiluwi alikuwa akituhumiwa kwa uchawi kwa muda mrefu, hivyo alipofika makaburini ndipo alipoombwa aingie kaburini  baada ya kuingia kaburini akiwa na watu wengine watatu wenzake walitoka kwa haraka na kumwacha Mwachiluwi peke yake ndipo kundi la watu waliokuwa eneo hilo la makaburi walianza kumshambulia kwa kumpiga mawe na fimbo hadi alizirai ndani ya kaburi.

Walianza kumfukia na alipofukiwa nusu ya mwili wake waliingiza jeneza la marehemu Peter Robert na kuliweka juu yake na kuanza kulifukia kaburi hilo  kwa udongo na baadaye wakachukua jeneza la marehemu na kuliweka juu yake, kisha kumfukia kwa udongo na kisha taratibu za mazishi ziliendelea kwa ajili ya marehemu  Peter.

Katika tukio jingine kikongwe aliyefahamika kwa jina la  Janeth Nenje(80), alinusurika kifo baada ya kucharangwa na mapanga na mtu aliyefahamika kwa jina la Pato Lwiza Mkazi wa Kitongoji cha Chang'ombe,Kijiji cha Mbuyuni Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya.

Inadaiwa mtuhumiwa alimfuata kikongwe huyo nyumbani kwake na kuanza kumcharanga kwa mapanga na kisha kumjeruhi vibaya hali iliyopelekea kukimbizwa katika Kituo cha afya kilichopo kijijini hapo.Mtuhumiwa Lwiza alimtuhumu ajuza huyo kuwa ni mshirikina hali iliyomfanya kuingiwa na hasira na kumtendea ukatili huo.

Katika tukio jingine  Watu watatu wakiwemo wanaume wawili na mwanamke mmoja walipigwa kwa mapanga na kuchomwa moto hadi kufa katika kijiji cha Mbala wilayani Chunya.Msemaji wa familia hizo tatu Mzee Crispin Katoto alidai kuwa mauaji hayo  yanahusishwa na imani za kishirikina.

 Mauaji ya kishirikina yanayofanana na  ya kitongoji cha Maweni wilayani Chunya pia mwaka huu yalitokea katika kijiji cha Kalungu kata ya Ivuna tarafa ya Kamsamba wilayani Mbozi  baada ya Kifo cha Mzee Nongwa Hussein ambacho kinadaiwa kilitokana na uchawi, vijana wenye hasira kali walihusishwa  kwa  kusababisha vifo vya watu wawili kati ya watatu kuzikwa hai.

Walioshutumiwa na kuhusika na kifo cha mzee Nongwa kwa imani za kishirikina ni pamoja na kaka wa marehemu George Hussein, Ernest Molela na Bi. Miziana  Nachela wote wakazi wa kijiji hicho.

Wakati mazishi yakiendelea vijana hao walianza kumtafuta kaka wa marehemu na kufanikiwa kuwakamata Bwana Molela na Bi. Nachela na kisha kuanza kuwaporomoshea kipigo  na kuwazika hai katika kaburi moja na marehemu Nongwa na hivyo kuzikwa watu watatu katika kaburi moja.

Baada ya sakata hilo vijana hao waliondoka makaburini na taarifa kumfikia Afisa Mtendaji wa Kata hiyo Joseph Silwimba, ambaye alifika eneo la tukio na kukuta kitendo hicho cha kikatili kimekwisha tendeka na yeye kuchukua jukumu la kulitaarifu Jeshi la Polisi ambao siku ya pili walilifika eneo la tukio na kuifukua miili hiyo ya watu waliozikwa hai. Miili hiyo ilikabidhiwa kwa ndugu ili kuzikwa upya katika makaburi mengine huku wakiuacha mwili wa marehemu Nongwa katika kabuli la awali

Uchunguzi uliofanywa katika baadhi ya vijiji vya tarafa hizo tatu  umebaini kuwa wakazi wengi katika maeneo hayo ni wa kabila la wanyamwanga na wafipa waliotokea wilayani Mbozi na Sumbawanga  na kuhamia wilayani Chunya katika tarafa za Songwe na Kwimba ambao kwa asili wanaendekeza  imani za kishirikina.

 Mwenyekiti wa kitongoji cha Maweni kijiji cha Mkwajuni Felix Kayanda anabainisha kuwa wakazi wa kitongoji hicho wanaendekeza imani za kishirikina ambapo katika kitongoji hicho  kuna waganga wa jadi zaidi ya 15 ambao wamekuwa wanafanyakazi ya kuagua na kufanya uchochezi wa kishirikina na kudai kuwa hata tukio la kuuwawa kikatili katekista Mwachiluwi lilichochewa na mganga mmoja wa jadi.

 Uchunguzi umebaini kuwa matukio haya ya mauaji ya kishirikina katika wilaya za Mbozi na  Chunya  mkoani Mbeya yanahusiana moja kwa moja kwa kuwa wakazi wake ni wa kabila moja la wanyamwanga ambao baadhi yao wametoka wilaya ya Mbozi na kuhamia wilayani Chunya.

 Kufuatia mauaji ya kishirikina yanayoendelea kuibuka kwa kasi katika wilaya ya Chunya ,mkuu wa Wilaya ya hiyo  Deodatusi Kinawiro amewataka Madiwani wa Halmashauri hiyo kukemea maovu yanayosababisha na imani za kishirikina kwa kuwa yameanza kuonyesha sura mbaya ya wilaya hiyo kwa watu wa ndani  ya nchi na  nje ya nchi.

“Kwa ujumla hivi sasa wilaya imekuwa na viashirio vya mauaji mengi sana yanayohusishwa na ushirikina wa ajabu, ambao unasababisha vifo  katika wilaya mfano huyu mzee mstaafu wa kanisa aliyeuwawa hivi karibuni kwa visa tu na kuanza kumtuhumu uchawi kwa kuanza kumpiga mawe na kisha kumfukia akiwa hai katika kaburi moja na marehemu “alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

 Hata hivyo Kinawiro amewataka madiwani katika kata zote zilizoshamiri vitendo hivyo kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa wanatembelea katika kata zao na kuongea na wananchi kuelimisha madhara ya kuamini ushirikina ambayo mpaka sasa yamekuwa kero kubwa na hata kuwafanya wananchi waishi kwa hofu .

 Alisisitiza kuwa kuanzia mwezi Julai anatarajia kufanya ziara katika vijiji vyote vya wilaya yake hasa katika tarafa za Kwimba na Songwe ambazo zimeshamiri kwa wakazi wake kuwa na imani za kishirikina na hivyo kuhatarisha amani na utulivu kwa kusababisha vifo na uharibifu wa mali.

 Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Diwani Athuman hivi karibuni akihojiwa katika vyombo vya habari,alisema jeshi lake litaendelea kufanya tathimini ili  kutambua uharifu wa aina zote unaofanyika katika mkoa wa Mbeya na kusisitiza kuwa wananchi waache tabia ya kujichukulia sheria mkononi badala yake washirikiane na jeshi la polisi kwa kutumia ulinzi shirikishi.

“Vijana wale ambao mnauwa wakongwe wenye macho mekundu kwa madai kuwa ni washirikina,mtambue kuwa nanyi siku moja mtazeeka na kuwa na macho mekundu,waharifu wasiuwawe bali wanatakiwa kupelekwa kwenye vyombo vya sheria,wote wauaji tukiwakamata tutawafungulia kesi ya mauaji’’,alisisitiza.











No comments:

Post a Comment