Monday, June 24, 2013

Kilimo cha kuhamahama chanzo cha utoro Tunduru


Kaimu afisa elimu msingi wilayani Tunduru Flavian Nchimbi

Na Albano Midelo
KILIMO cha kuhamahama ndiyo chanzo kikuu cha utoro wa kudumu na rejereja kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wilayani Tunduru mkoani Ruvuma.
Wakazi wa wilaya ya Tunduru wengi wao ni kabila la wayao,ambao wanaendesha maisha kwa kutegemea zaidi  Shughuli za kilimo, cha korosho,mihogo na mpunga na sasa wamejikita zaidi katika kilimo cha kuhamahama  cha  zao la Mpunga,hali hiyo imewafanya wananchi wa Tunduru kuwa nyuma  katika maendeleo ya elimu.
Utafiti ambao umefanyika katika baadhi ya shule za msingi na sekondari wilayani humo kwa kuzungumza na wanafunzi,walimu, wazazi,walezi na wadau wa elimu kwa ujumla wamekiri kuwa kilimo cha kuhamahama kinachangia  tatizo la utoro kwa zaidi ya asilimia 90.

Hassan Musa mkuu wa shule ya Frankweston anasema katika wilaya ya Tunduru wazazi wengi katika kipindi cha kilimo kuanzia mwezi Desemba hadi Juni wanahama katika makazi yao ya kudumu na kuhamia mashambani umbali wa kati ya kilometa 25 hadi 30 na kuacha familia zao kwenye makazi yao kwa muda mrefu.
Hali hiyo kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule ndiyo chanzo cha utoro na mimba za utotoni kwa kuwa watoto wao katika kipindi chote wanakuwa huru kutokana na kuishi bila wazazi huku watoto wakubwa wakifanya kazi ya kuwalea watoto wenzao kwa kujiingiza kwenye vitendo vya utoro shuleni na kufanya ngono zinazosababisha mimba zisizotarajiwa.
“Watoto wanaachwa wanajitegemea wenyewe,shuleni wanakwenda wanavyotaka,watoto wa kike wanashawishika katika ngono ambazo sio salama hivyo kuwapa mwanya wa kujiingiza kwenye mimba za utotoni na utoro wa kudumu,watoto wengi Tunduru wana watoto wao kwa mfano mimi mwaka huu  watoto 30 ni watoro kati ya watoto 203   waliotakiwa kuanza kidato cha kwanza  hata hivyo  majina ya wazazi  yao yamepelekwa  mahakamani’’,alisema.
Kulingana na mkuu huyo wa shule wazazi wengi katika wilaya ya Tunduru ni maskini kiasi kwamba wanashindwa hata kulipa ada kwa wanafunzi wao wanaosoma sekondari za kata ambayo ni shilingi 20,000 tu na kwamba hali inasababisha wanafunzi hao kuwa watoro na wengine kujiingiza kwenye vitendo viovu.
Neema Mwakila na Edmund Ndunguru ni walimu shule ya sekondari Frankweston wanasema malezi mabaya ya kuwaacha watoto wajitunze wenyewe yamechangia utoro wa wanafunzi katika shule nyingi na wengine kuamua kuolewa hali ambayo inachangia kushusha taaluma wilayani Tunduru.
Ally Chilova mwalimu wa sekondari ya Frankweston anasema umaskini ndiyo chanzo kikubwa cha utoro  na kwamba familia nyingi za Tunduru ni maskini hali ambayo inawafanya wanafunzi kushiriki katika mapenzi ili kujipatia kipato kwa familia yake na amesisitiza kuwa  vijiji vingi vya Tunduru mtoto wake anakuwa ni kitega uchumi cha kuhakikisha familia inapata pesa kwa kufanya mapenzi.
Umaskini uliopo katika wilaya ya Tunduru kwa kiasi kikubwa unachangiwa na mwamko duni wa elimu ambao ulikuwepo tangu zamani ambapo mapokeo ya elimu yalikuwa kidogo kiasi kwamba mzazi alikuwa anamshauri mtoto wake wa kike kuhakikisha kuwa asifaulu mtihani katika shule za msingi ili aendelee kuwa nyumbani kutumika kama kipato cha familia.
Hata hivyo amesema hivi sasa mwamko wa elimu katika wilaya hiyo angalau umeanza kutokana na mwingiliano wa watu kutoka mikoa mingine pamoja na jitihada za serikali kukabiliana na changamoto zinazodidimiza elimu katika wilaya hiyo.
Telispholi Ngonyani mwalimu wa sekondari ya Frankweston anasema mimba kwa shule za msingi na sekondari wilayani Tunduru zinachangiwa na mwamko duni  wa elimu unaosababishwa na  utoro wa kudumu unaozaa mimba za utotoni na kwamba elimu inaingia taratibu kwa wakazi wa wilaya ya Tunduru ambapo waislamu ni asilimia 90.
Olivia Mapunda mwalimu mkuu shule ya msingi Umoja wilayani Tunduru anasema utoro katika shule za msingi na sekondari unachangiwa na wazazi kuhamia mashambani na kuwaacha watoto nyumbani kwao bila chakula hivyo watoto wengi wanakuwa tegemezi kwa kubeba majukumu ya familia hivyo kupata vishawishi mbalimbali ikiwemo kupata mimba.
“Shule nyingi za msingi wilayani Tunduru,wanafunzi wanatoroka kuanzia saa nne wengine wanaondoka moja kwa moja na wengine wanarudi kwa kuchelewa kutokana na kukosa chakula kwa kuwa wazazi wao wanakuwa mashambani ambako ni mbali kwa wiki nzima na kuwaacha watoto pekee yao hali ndiyo inachangia utoro wa kudumu au rejereja tatizo hilo huanzia mwezi Januari hadi Mei kila mwaka’’,alisema.
 Mapunda anasema wazazi na walezi wakipatiwa mashamba yaliokuwa karibu tatizo la kuwaacha watoto kwa muda mrefu linaweza kumalizika kwa kuwa  wazazi watakuwa jirani na familia yao au sheria iwekwe mzazi mmoja abakie kuwalea watoto badala ya wazazi wote wawili kuhamia mbali kwa ajili ya kutafuta mashamba yenye rutuba.
Kaimu afisa elimu wa wilaya ya Tunduru Flavian Nchimbi  amesisitiza kuwa tatizo la wazazi kuhama katika makazi yao na kwenda kutafuta mashamba mbali ya kuwaacha watoto bila kuwa na mlezi kwa muda mrefu yamechangia utoro wa wanafunzi kwa asilimia 80.
Hata hivyo hatua za kukabiliana na hali hiyo zinachukuliwa na serikali kwa kuwaelimisha wazazi  umuhimu wa elimu kwa watoto wao na wazazi wengine ambao watoto wao ni watoro wa kudumu wanachukuliwa hatua za kisheria kupitia serikali za vijiji,kata,tarafa na wilaya ili kukomesha utoro kwa wanafunzi.
 Kwa mujibu wa Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wasichana 8000 kila mwaka huacha shule kutokana na ujauzito Kati yao 3,000 ni wanafunzi wa shule za msingi.
Kila siku, wanawake 24 hufariki dunia kutokana na mimba au wakati wa kujifungua. Wanawake watano mpaka sita wanaofariki kati ya hao ni watoto wadogo, watoto hao hufariki dunia kwa kuwa miili yao haijakomaa vya kutosha kwa ajili ya kujifungua

No comments:

Post a Comment