![]() |
| Baadhi ya watoto katika kitongoji cha Maweni wakiwa hawana mlezi |
Na Albano Midelo
KITONGOJI cha Maweni
katika kijiji cha Mkwajuni wilayani Chunya mkoani Mbeya kimebakiwa na wanawake
pekee baada ya wanaume karibu wote kukimbia kwa takribani mwezi mmoja na nusu
kuhofia kukamatwa na polisi kwa tuhuma za mauaji.
Katika hali isiyokuwa
ya kawaida wanaume vijana zaidi ya 600 katika kitongoji hicho chenye jumla ya watu 4500 wamekimbia na kuacha wake
zao na watoto wanaangaika kwa kukosa
malezi bora kutoka kwa wazazi wote wawili na wengine wakiwa wamebakia yatima
baada ya kufiwa na mama zao .
Kitongoji hicho
kimebakiwa na wanawake,watoto na wazee wachache wanaume kufuatia operesheni inayoendelea
kufanywa usiku na mchana na jeshi la polisi kuwatafuta vijana wanaotuhumiwa
kumua kikatili katekista wa kigango cha Maweni Amosi Mwachiluwi(70).
| Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro |
Aprili 27 mwaka huu Katekisita Mwachiluwi katika
kitongoji hicho alikamatwa kupigwa na kuzikwa akiwa hai katika kaburi moja na mtu
anayedaiwa kumuua kwa njia ya kishirikina aliyefahamika kwa jina la Peter
Robert.
Inadaiwa baada ya kuingia
kaburini akiwa na watu wengine watatu wenzake walitoka
kwa haraka na kumwacha Mwachiluwi peke yake ndipo kundi la
vijana waliokuwa eneo hilo la makaburi walianza kumshambulia kwa kumpiga mawe
huku wakimwamuru akae chini kisha walianza kumfukia na alipofukiwa nusu ya
mwili wake waliingiza jeneza la marehemu Peter Robert na kuliweka juu yake na
kuanza kulifukia kaburi hilo hivyo kumsababishia kifo.
| Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Diwani Athuman |
Uchunguzi ambao
umefanywa katika kitongoji hicho umebaini kuwa baada ya vijana kukimbia
kusikojulikana nyumba karibu zote
zimeachwa na kuongozwa na wanawake na nyumba nyingine watoto wanajiongoza wenyewe hali ambayo inaongeza umaskini katika familia
kutokana na ukweli kuwa baba ambaye ni kichwa cha familia hayupo hivyo watoto
wengi wanashindwa kupata hata mlo mmoja katika familia.
Mwenyekiti wa
serikali ya kitongoji hicho Felix Kayanda alisema vijana karibu wote walipoamua kuondoka katika
kitongoji hicho kuhofia kukamatwa na polisi,maisha yamekuwa magumu ambapo hivi
sasa kila mara inapotokea tatizo la msiba katika kijiji hicho huwalazimu kwenda
kuwakodi vijana kutoka kijiji cha Mkwajuni kwa kuwalipa kwa ajili ya kuchimba
kaburi na shughuli za mazishi kwa ujumla.
“Leo hapa kijijini
kuna msiba,hakuna kijana aliyerudi hapa,hivyo nimepita kukusanya michango
kutoka kwa akinamama kwa ajili ya kwenda kukodi gari la kubeba msiba na
kuwalipa vijana ambao watachimba kaburi,kwa kweli hali ni mbaya sana haijawahi
kutokea hali kama hii mimi kama kiongozi nipo katika wakati mgumu
sana’’,alisisitiza.
Matrida Jeremia mama
wa watoto watano ambaye mume wake amekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na mauaji
alidai kuwa mumewe hausiki na mauji na kwamba siku ya msiba hakuwepo hata
aliposikia anatumiwa kwa mauaji hakuweza kuamini.
Alisema anapata shida
ya kuleta watoto wake watano ambao ameachiwa na mumewe ambaye yupo mahabusu na
kusisitiza kuwa kuna watoto wameacha shule na wengine ni watoro kwa kuwa yeye
pekee yake hawezi kumudu malezi ya watoto kwa kuwa hana kazi ya maana zaidi ya
kilimo.
Joyce Mwanambilimbi
mkazi wa kitongoji hicho alidai kuwa mumewe ambaye amemwachia watoto wanne
ametoroka kuhofia kukamatwa na polisi hivyo amemuacha anapata shida ya kulea
watoto kati yao ambao mmoja anasoma sekondari na wengine wapo shule za msingi.
![]() |
| Leya Mathias akihojiwa na mwandishi wa makala haya |
“Baadhi ya wanawake
wameamua kujiingiza katika ngono ili angalau kujipatia kipato cha kuendesha
maisha na watoto wao,wengine wameolewa na wanaume wengine,naamini tatizo hili
lisipopatiwa ufumbuzi kwa miezi sita ijayo ndoa zitavunjika na watoto wanakuwa
katika mazingira magumu hivyo kuwaathiri katika maisha’’alisema Joyce
Leya Mathias mama wa
watoto watatu mkazi wa Maweni akizungumza huku anatokwa na machozi,alidai kuwa
mume ambaye amekamatwa na polisi kwa tuhuma za mauaji hausiki na mauaji hayo
alikamatwa kwa kuonea na kusisitiza kuwa hata siku ya mazishi hakuwepo .
“Tangu mume wangu
amekamatwa na kuniacha na watoto watatu maisha yamekuwa magumu,watoto wangu
walikuwa wanafanya vizuri shuleni,walikamata nafasi ya kwanza hadi ya tatu
lakini mtihani wa muhula wa mwezi huu wa sita wote wamekamata nafasi ya mwisho
kwenye mitihani yao kwa kuwa walikuwa watoro,muda mwingi nilikuwa nakwenda nao
shambani kwa kuwa sina msaidizi yeyote’’,alidai mama huyo.
Mwanamke huyo
ameshauri kuwa njia pekee inayowezesha vijana hao kurudi katika kijiji hicho ni
jeshi la polisi kuwaachia vijana waliokamatwa kwa tuhuma za mauaji na
kuwakamata vijana waliohusika na tukio hilo ambao bado hawajakamatwa hadi sasa
licha ya kufahamika kwa majina.
Mwenyekiti wa kijiji
cha Mkwajuni Credo Kayanza alikiri kuwa watuhumiwa karibu wote waliokamatwa na
polisi hawakuhusika na tukio hilo na kwamba serikali ya kijiji tayari imepata
majina sahihi ya wote ambao walipanga na kuhusika moja kwa moja na tukio hilo
la kinyama ambalo alifanyiwa katekista Mwachiluwi.
“Kuna vijana
wamekamatwa na hivi sasa wapo mahabusu katika gereza la Ruanda Mbeya,hata hivyo
wengi waliokamatwa sio walengwa wanatakiwa waondolewe,walengwa wenyewe bado
wapo hapa kijijini wanafahamika na majina tunayo,hivyo mimi kama mwenyekiti wa
kijiji nilikwenda kwa OCD kushughulikia tatizo hilo’’,alisema Kayanza.
Diwani wa kata ya
Mkwajuni Chesco Ngairo alisema tukio hilo la mauaji limeharibu sifa ya kijiji
cha Mkwajuni na kwamba kamati ya ulinzi na usalama katika kata imejipanga
kuhakikisha kuwa watuhumiwa wote halali wa mauaji hayo wanakamatwa na
kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Alisema kutokana na
asilimia kubwa ya wanaume kukimbia katika kitongoji hicho yeye kwa kushirikiana
na mwenyekiti wa kijiji waliitisha mkutano wa kuwataka vijana ambao
hawakuhusika na kitendo cha mauaji warudi kijijini kwa kuwa sio vijana wote
katika kitongoji cha Maweni walihusika katika mauaji hayo.
Hata hivyo Ngairo
alisema hadi sasa hakuna kijana hata mmoja ambaye amerudi katika kitongoji
hicho,hivyo kuleta athari kubwa katika jamii inayohusika ambapo amemuomba mkuu
wa kituo cha polisi cha Mkwajuni kupunguza operesheni ya kukamata ovyo badala
yake kuwatafuta walengwa ambao majina yao yapo .
Mwenyekiti wa kijiji
cha Mkwajuni Kayanza amekiri kukimbia
kwa wanaume katika kitongoji hicho kumesababisha athari nyingi zikiwemo watoto
kulelea na mzazi mmoja yaani mama na wengine kujiletea wenyewe kutokana na kukosa
wazazi wote wawili na kwamba umaskini katika eneo hilo unaongezeka kwa kuwa
nguvu kazi ambayo ni wanaume hawapo hali inayosababisha mwanamke kupata kazi ya
kulea watoto pekee yake.
“Athari ni nyingi mno
kwa mfano hivi sasa kila unapotokea msiba hawawezi kuzika hadi mimi
nimehudhuria katika mazishi hayo,wananchi hivi sasa hawana imani na usalama,ndoa nyingi zinaweza kuvunjika muda
sio mrefu kwa sababu wanawake wanaweza kuolewa na wanaume wengine na hata waume
zao huko walikokimbilia wanaweza kuoa na kuanzisha familia nyingine’’,alisema.
Mkuu
wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro ametaka madiwani katika kata zote kuwa
mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa wanatembelea katika kata zao na kuongea
na wananchi kuelimisha madhara ya kuamini ushirikina ambayo mpaka sasa yamekuwa
kero kubwa na hata kuwafanya wananchi waishi kwa hofu .
“Kwa
ujumla hivi sasa wilaya imekuwa na viashirio vya mauaji mengi sana
yanayohusisha ushirikina wa ajabu ambao unasababisha vifo vingi katika wilaya mfano huyu mzee mstaafu wa kanisa
aliyeuwawa hivi karibuni kwa visa tu na kuanza kumtuhumu uchawi kwa kuanza
kumpiga mawe na kisha kumzika akiwa hai kaburi moja na marehemu “alisema Mkuu
huyo wa Wilaya.
Amewaasa
wananchi kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi ambapo athari zake wameziona
katika tukio hilo ambapo vijana wamezihama nyumba zao na kuwaacha wake na
watoto wao wanateseka kwa kukosa malezi ya wazazi wote wawili.
“Wananchi
waache kucheza na dola kwa kufanya uharifu,hata hivyo kama kweli wana majina
ambayo ni ya watuhumiwa halali ambao wameachwa watupe majina hayo ili
kuwakamata watuhumiwa wa mauaji wote
halali,serikali haiwezi kukaa kimya inapowaona baadhi ya raia wanawauwa wenzao
kwa imani za kishirikina ’’,alisisitiza.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Diwani
Athumani alisema jeshi la polisi linaendelea na msako wa kuwatia mbaroni
watuhumiwa wote wa mauaji hivyo ametoa
mwito kwa wananchi kutoa ushirikiano wa kuhakikisha watuhumiwa wote wanakamatwa
na kufikishwa mahakamani.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129


No comments:
Post a Comment