Na Mwandishi wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk Edward Hoseah, amefunguka na
kueleza sababu za taasisi yake kushindwa kuwakamata walarushwa wakubwa kwa kuwa
Serikali imemfunga mikono.
Akitoa majumuisho katika Mkutano
Mkuu wa Chama cha Wabunge Wanaopambana na Rushwa nchini (APNAC) jana, Dk Hoseah
alisema kuwa Serikali imeitenga Takukuru na kuwafanya waishi kama yatima.
Huku akishangiliwa na idadi kubwa ya
wabunge, Mkurugenzi huyo alisema kuwa amekuwa akishangazwa na lawama ambazo
amekuwa akibebeshwa kila wakati kuwa ameshindwa kumaliza rushwa wakati bila
kuziangalia sheria.
“Mnanipa lawama kila wakati, lakini
huwezi kuanzisha chombo kama TAKUKURU halafu ukamfunga mikono mhusika, na mimi
mmenifunga mikono nifanyeje jamani? Alihoji na kuongeza:
“Hata katika rasimu ya Katiba bado
mmetutenga kama watoto yatima, wenzetu wote mmewaweka tena hata CAG mmesema
kuwa mamlaka yake akiteuliwa basi asiingiliwe wala kuhojiwa…mamlaka gani mtu
asihojiwe jamani, mimi nikiuliza Takukuru mnasema subirini Serikali ya
Tanganyika.”
Gazeti la Guardian la Uingereza la
Jumapili ya Desemba 19, 2010, lilitoa taarifa ya siri kuhusu wala rushwa
wakubwa kulindwa Tanzania. Gazeti hilo lilichapisha taarifa za mtandao wa
WikiLeaks uliokuwa ukimilikiwa na mwandishi wa habari wa Australia, Julian Paul
Assange, ukimnukuu Dk Hoseah.
Dk Hoseah alinukuliwa na WikiLeaks
akimueleza mwanadiplomasia wa Marekani aitwaye Purnell Delly, Julai 14 jijini
Dar es Salaam mwaka 2007 kuhusu uwezo na nia ya Rais Kikwete katika
kushughulikia ufisadi.
Alidai Rais Jakaya Kikwete alikuwa
anakwamisha kuchunguzwa kwa vigogo wa Serikali wanaotuhumiwa kwa vitendo vya
rushwa, na pia anahofia maisha yake kama mkuu wa Takukuru. Hata hivyo, Dk
Hoseah kwanza alikiri kukutana na ofisa huyo ofisini kwake Julai 2007, lakini
alikanusha kuzungumza kuwa Rais Kikwete alikuwa hataki sheria ichukue mkondo
wake katika kuwachunguza vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa.
Atoa ushauri kwa Serikali
Kwa mara ya kwanza jana kiongozi
huyo aliitolea uvivu Serikali kuwa imekuwa ikichangia mambo mengi katika rushwa
ikiwamo usiri mkubwa katika rasilimali za nchi.
“Lazima Serikali iwe wazi, huwezi
kuwaficha wananchi rasilimali zao eti ni siri kwa sababu ya sera mbovu,
tunawaambia wananchi watanufaika na mirabaha ya asilimia tatu hiyo siyo sahihi
jamani ndiyo maana tunashindwa kutoa majibu kwa wananchi wetu hilo ni tatizo
jingine linalosababisha mambo ya rushwa,”alisema na kuongeza: “Siyo kila jambo
ambalo serikali inapewa ushauri ni baya.”
Alipinga kitendo cha viongozi kuwa
na kigugumizi katika uwajibikaji na akataka itungwe sheria kali ya kutaka
kiongozi awajibike mara anapokuwa ametuhumiwa kwa jambo lolote aachie ngazi na
kupisha uchunguzi kama ilivyo kwa nchi zingine.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI

No comments:
Post a Comment