![]() |
| Wachuuzi wa samaki forodha ya Liuli Nyasa wakiuza samaki |
Na Albano Midelo
JANGA
la kutisha linaweza kuwakumba wakazi wa wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma ambao kwa
wiki nzima sasa wanakula samaki ambao huenda wamekufa kwa sumu.
Utafiti
wa awali unaonyesha kuwa takribani wiki moja sasa wavuvi katika ziwa Nyasa
kwenye maeneo ya kata tano za Lituhi, Kihagara Liuli, Lipingo,Mtipwili hadi
vijiji vya mpakani na nchi ya Msumbiji, wanaokota samaki ambao wamekufa ndani
ya ziwa hilo wakielea juu ya maji na kuwauzia wananchi huku wakichanganya na
samaki ambao wamewavua wao wenyewe.
utafiti
huo wa awali unaonyesha kuwa wavuvi wanapokuwa ndani ya ziwa kila siku wanawakuta samaki wengi wamekufa
wakiwa wanaelea juu ya maji kisha kwa siri kubwa wanawaokota na kuwachanganya
na samaki waliowavua na kwenda kuwauzia walaji ambao sio rahisi kutambua kwa
kuwa samaki wote wanaoonekana sawa bila kujali kuwa wamewavua au wamewaokota
wakiwa wamekufa.
Baadhi
ya wavuvi waliohojiwa kwa njia ya simu wamekiri kwa wiki nzima sasa samaki
wanaendelea kufa ndani ya ziwa Nyasa na kwamba hawajui sababu za vifo hivyo
licha ya kwamba wanawaokota samaki waliokufa na kuwauzia walaji na kwamba hadi
sasa hakuna mtu aliyedhuruka kwa kula samaki hao.
Morisi
Nyirenda mvuvi katika forodha ya Nkali
kata ya Liuli amethibitisha kuwa kuna samaki wengi wanakufa na kwamba wao kama
wavuvi wakiwa ndani ya ziwa wanawakuta samaki wamekufa na kuwachanganya na
waliowavua kisha kuwauzia walaji kwa madai kuwa bado hawajui iwapo samaki hao
wana madhara kwa binadamu kwa kuwa kwa wiki nzima sasa wote waliowauzia
hawajalalamika kuwa wamepata madhara.
Samweli
Kaseke na Isack Kamanga wavuvi wa forodha ya Hongi na Nkali kata ya Liuli wamewataja aina ya samaki ambao wanaongoza kufa kwa
wingi kila siku kuwa ni pamoja na ligong’wa, njeringu ,likuku, vindongo, vigong’o,
vituhi, hango, ngisi,mbufu,lihenji,magege na batazibi.
Mvuvi katika eneo la Lituhi Nicodemu Ndomba
amekiri kuwaokota samaki waliokufa katika eneo hilo aina ya mbufu,,mchena na
perege na kwamba tatizo la kufa samaki ovyo katika eneo hilo lina siku nane
sasa ambapo wananchi wanauziwa na wavuvi samaki hao bila kujali kuwa
samaki wamekufa kwa tatizo gani.
Aliyataja
maeneo ya kata za
Kihagara,Liuli,Ngindo,Lipingo na Mtipwili hadi vijiji vya mpakani na nchi ya
Msumbiji ,tarafa za Ruhekei na Ruhuhu wilayani humo kwamba yamekumbwa ya tatizo
la samaki kufa ovyo na kwamba hivi sasa wanaendelea kupita katika maeneo hayo
na kuwatangazia wavuvi na wananchi wasitumia kwa kitoweo samaki waliokufa
wenyewe kwa kuwa wanaweza kuwaletea madhara ya kupata magonjwa mbalimbali au
hata kusababisha vifo.
“Hili
ni tatizo kubwa katika wilaya yetu ya Nyasa mimi kama kiongozi wa ngazi ya
wilaya tayari nimeripoti wizarani ili utafiti wa kina kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali ufanyike kutambua sababu zinazosababisha vifo vya samaki ovyo kwa
kuwa ufumbuzi usipopatikana unaweza kuathiri wakazi wa mwambao kiafya na
kiuchumi’’,alisisitiza.
Kulingana
na mtaalamu huyo wa samaki,utafiti wa awali umebaini kuwa samaki wanaokufa na kuelea juu ya maji wameonekana kuwa na
majeraha ya kubabuka katika sehemu mbalimbali za mwili zikiwemo
usoni,tumboni,kichwani,mkiani na
mgongoni.
Victor
komba mwanaharakati wa mazingira wilayani Nyasa anadai kuwa inawezekana mgogoro
wa mpaka kati ya Tanzania na Malawi ukachangia kuibuka kwa tatizo hilo na
kwamba inawezekana serikali ya Malawi imelihujumu ziwa Nyasa upande wa Tanzania
kwa kupiga bomu la sumu ili kuuwa samaki hivyo ni vema watafiti wakafika mapema
katika ziwa Nyasa ili kufanya utafiti wa kina na kubaini sababu za samaki kufa
ovyo.
“Maisha
ya wakazi wa Nyasa kwa asilimia kubwa wanategemea uvuvi hivyo kuibuka kwa
tatizo hili la samaki kufa ovyo linaweza kuongeza ugumu wa maisha mara
dufu,tunaomba serikali na wadau
mbalimbali wafanye haraka kufanya utafiti na kuwaondoa wananchi katika hatari
ya kupata magonjwa endapo samaki
wanaokula watakuwa wameathirika na sumu’’,alisema.
Samaki
wa ziwa Nyasa wanauzwa katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo ya
Ruvuma,Mbeya,Njombe,Iringa,Dodoma,Dar es salaam, Morogoro, Lindi,Rukwa,Katavi
pamoja na mikoa mingine mingi.Ziwa
Nyasa linanufaisha watanzania wa wilaya ya Ludewa mkoa wa Njombe, wilaya ya
Kyela mkoa wa Mbeya na wilaya ya Nyasa mkoa wa Ruvuma na kwamba samaki wa ziwa
Nyasa wanaliwa katika sehemu mbalimbali nchini.
Kulingana na utafiti ambao ulifanywa na jumuiya
ya nchi zilizo kusini mwa Afrika(SADC) kwa kushirikiana na nchi ya Uingereza kwenye ziwa Nyasa mwaka
2007,ulionesha kuwa ziwa hilo lina kiasi cha tani 165,000 za samaki na kati ya
kiasi hicho tani 35,000 za samaki ni jamii ya samaki wa maji ya juu ambao
wanaweza kuvuliwa bila kuathiri uvuvi kila mwaka.
albano.midelo@gmail.com,simu
0766463129

Jamani mbona taabu sana maana wanyasa bila samaki ugali haumezeki...Nategemea watakuwa salama..Hizo sehemu nimeishi na najua jinsi wanavyothamani samaki....
ReplyDelete