MABADILIKO makubwa
yametokea katika shule za msingi wilayani Tunduru ambapo idadi ya wanafunzi
wanaopata mimba katika shule za msingi imepungua kutoka mimba zaidi ya 250 kwa mwaka miaka mitatu iliyopita
hadi kufikia mimba 16 tu mwaka 2012.
Flavian Nchimbi kaimu afisa
elimu msingi wilaya ya Tunduru alisema tatizo la mimba katika shule za
msingi zimepungua ukilinganisha na miaka mitatu nyuma ambapo zaidi ya nusu ya mimba zilizoripotiwa za mkoa
wa Ruvuma kwa wanafunzi zilitokea wilayani humo.
“Kwa mfano mwaka 2010
katika mkoa wa Ruvuma kulikuwa na mimba za wanafunzi 544 kati ya hizo mimba
karibu 250 ziliripotiwa kutoka wilaya ya Tunduru pekee huku idadi nyingine
inayobakia ni kwa wilaya za Songea,Mbinga na Namtumbo kwa hivi sasa
tumefanikiwa sana kupunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi
katika wilaya ya Tunduru hadi mimba 16 tu mwaka mwaka jana’’,alisema.
Aliongeza kuwa mwaka
huu huenda idadi ya mimba katika shule za msingi ikapungua zaidi kutokana na
takwimu kuonyesha kuwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Mei mwaka huu ni
mimba moja tu ndiyo iliyoripotiwa.
Hata hivyo afisa
elimu huyo alikiri msukumo ambayo ulifanywa na vyombo vya habari kutoa
kipaumbele katika tatizo la mimba za utotoni na utoro ambao ulikithiri na kuathiri sekta ya elimu, uliamsha uongozi
katika ngazi mbalimbali kuchukua hatua za kuhakikisha matatizo hayo yanapatiwa
ufumbuzi wa kudumu.
Alizitaja hatua
ambazo zilichukuliwa kuwa ni pamoja na kuamua kufanya operesheni
maalum ya kuwatafuta wanafunzi watoro na
ambao wameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya mimba,kuwasaka wanaume
waliowapa mimba ili kuwachukulia hatua za kisheria na kutoa fundisho kwa wanaume
wengine wenye tabia hiyo.
“Tunafungua kesi nyingi kila mwaka kwa wazazi na walezi ambao
wameshindwa kuwapeleka watoto wao shule
za msingi, wanaume waliowapa mimba wanafunzi,wanaume wanaoa wanafunzi pamoja na
wanafunzi watoro wa kudumu, tumeshirikiana na Baraza la madiwani,viongozi wa
dini kimila na wadau wengine kuweka
msukumo katika elimu ndiyo maana sasa hata idadi ya mimba zimepungua
sana’’,alisisitiza Nchimbi.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho alisema Kutokana na na takwimu mbaya za mimba za utotoni
zilizokuwepo na kuiathiri sekta ya elimu wilayani humo yeye binafsi amefanya
ziara katika vijiji vyote vya wilaya hiyo na kuwawaagiza viongozi wa serikali
za vijiji,kata na tarafa kuwachukulia hatua wazazi na walezi wote ambao
wameshindwa kusimamia mahudhurio ya watoto shuleni,mimba za utotoni na
kushindwa kuwapeleka watoto wao waliofaulu shule za msingi kujiunga na
sekondari.
“Hali ya elimu sio
nzuri wilayani Tunduru,tumeamua kufanya operesheni maalum ya kuwatafuta
wanafunzi ambao wameshindwa kwenda kidato cha kwanza mwaka huu, tumefungua kesi
1054 za wazazi ambao wameshindwa kuwapeleka watoto wao waliofaulu shule za
msingi kwenda sekondari,tutahakikisha
tunaweka msukumo wa kudumu katika elimu ili wilaya yetu iweze kupata
maendeleo makubwa katika sekta ya elimu ’’,alisisitiza
Kwa mujibu wa Takwimu za kitaifa za Wizara ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi za hivi karibuni zinaonyesha kuwa wasichana 8000 kila mwaka huacha shule kutokana na ujauzito
kati ya hao wanafunzi 3,000 ni shule za msingi na 5000 ni wanafunzi wa shule
za sekondari.
albano.midelo@gmail.com
.

Inasikitisha sana kwa kweli...sijui mwisho utakuwaje?
ReplyDelete