Walimu wadaiwa kuhongwa mifugo
kutowaandikisha wanafunzi
Utafiti uliofanywa
katika baadhi ya shule za msingi na sekondari katika tarafa za kwimba na Songwe
wilayani Chunya mkoani Mbeya umebaini kuwa mwamko wa elimu katika maeneo mengi
ni duni.
Katika maeneo hayo
wazazi na walezi hawana mwamko wa kuwapeleka watoto wao shule na hata wanafunzi
wanaosoma wengi wanaacha shule kwa utoro,mimba na kuolewa kutokana na mila na
desturi zinazoendelezwa na wakazi wa wilaya hiyo wengi wao wakiwa ni wafugaji,wachimba madini,wavuvi
na wakulima.
Katika kijiji cha
Mkwajuni wanafunzi katika shule za msingi wapo wengi ambao ni watoro wa
rejereja na wengine ni watoro wa kudumu,ambapo ukitembea katika maeneo
unakutana na watoto wa darasa la kwanza hadi la tano ambao wanazurura bila
kwenda shuleni.
Mwenyekiti wa
serikali ya kijiji cha Mkwajuni Kredo Kayanza alisema wakazi wa kijiji hicho ni
wagumu hata kuchangia michango mbalimbali ya elimu katika shule za msingi na
sekondari hali ambayo inawafanya watoto wao kusoma katika mazingira magumu.
“Kijiji hiki kina
shule za msingi tatu ,nusu ya wanafunzi katika shule hizo wanakaa chini
kutokana na upungufu madawati,shule ya msingi Mkwajuni ina wanafunzi 980, shule
ya Maweni ina wanafunzi zaidi ya 700 na shule ya msingi Osterbay ambayo
haijafikia bado darasa la saba ina wanafunzi zaidi ya 400,shule zote
zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vyumba vya kusomea hivyo kuna mlundikano mkubwa wa wanafunzi
katika chumba kimoja wanaofikia hadi 80’’,alisema.
![]() |
| Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro |
Baadhi ya wazazi
walipohojiwa kwanini wanashindwa kuchangia michango mbalimbali ya elimu
,walidai kuwa ni kutokana na shule za msingi na sekondari kutoza michango mingi
ambayo watanzania wengi masikini ambao hawana uhakika wa kula hata mlo mmoja
wanashindwa kumudu hivyo watoto wao wanafukuzwa na kuwa watoro.
Leya Mathias mkazi wa
kitongoji cha Maweni Mkwajuni aliitaja sababu kubwa ambayo inachangia utoro kwa
wanafunzi katika kijiji cha Mkwajuni ni wazazi na walezi kushindwa kulipia
michango mingi hivyo kuamua watoto wao kubakia nyumbani na kufanyakazi za
shambani,uvuvi na uchimbaji madini.
“ Watoto wengi katika
shule za msingi na sekondari hapa Mkwajuni wameacha shule kwa kuwa mzazi mmoja
anashindwa kulipia michango mingi ya fedha za madawati,mlinzi,tofali mimi pekee
yangu mwanamke nitatoa pesa zote hizo kutoka wapi,ndiyo maana watoto wanabakia
kuwa watoro ’’,alisema.
Hata hivyo mwenyekiti
wa serikali ya kijiji cha Mkwajuni Kayanza alikanusha madai hayo kuwa sio
sahihi kwa kuwa michango yote inayotozwa imepitishwa na kukubaliwa na wananchi
wenyewe kwenye vikao na kwamba sababu kubwa ni mwamko duni wa elimu walionao
wazazi na walezi wengi katika wilaya ya Chunya.
Wafugaji wahamiaji
kwenye bonde la Songwe wilayani Chunya wanadaiwa wamewekeza zaidi kwenye mifugo
kuliko elimu hali ambayo imesababisha watoto wao waliostahili kuanza shule ya
msingi kuendelea na kazi za uchungaji wa
mifugo badala ya kusoma.
Wafugaji hao wahamiaji wanaishi katika vijiji
vya kata za Galula, Mbuyuni na Totowe ambapo
takwimu za mifugo katika Halmashauri ya wilaya ya Chunya zinaonesha kuwa
wafugaji hao hadi kufikia Desemba 2010 walikuwa na mifugo ya aina mbalimbali zaidi ya 800,000
wakiwemo ng’ombe,mbuzi,kondoo na punda.
Uchunguzi unaonesha
kuwa familia za wafugaji wamewaachisha masomo watoto wao kwa lengo la kuchunga
mifugo na hata wale ambao wanaendelea na masomo wanasoma kwa kufanya utoro wa
mara kwa mara .Hali hiyo ndiyo iliyosababisha asilimia 90 ya wafugaji hao
wahamiaji ambao walifika kwenye bonde hilo miaka ya 1980 kutojua
kusoma,kuandika na kuhesabu.
Imebainika baadhi ya
maeneo katika bonde wafugaji wanawahonga mifugo baadhi ya walimu wakuu ili
wawafute shule watoto wao na kuendelea kuchunga mifugo yao wakati wote,hali
hiyo ndiyo moja ya sababu za wilaya hiyo kuwa nyuma katika elimu na kukabiliwa
na umaskini wa kifkra na kiuchumi.
John
Bedas mkazi wa kijiji cha Galula anadai kuwa umaskini wa kipato kwa wananchi wa
Wilaya ya Chunya umesababisha wazazi na walezi kuwaficha watoto wao msituni
wakati wa zoezi la kuandikishwa shule za msingi na baada ya kupita zoezi hilo
huwapeleka kuvua samaki ,kuchimba dhahabu,kuchunga mifugo pamoja na kilimo.
Imeelezwa
kuwa kutokana na hali wilaya ya chunya imekuwa na watoto wengi ambao hawasomi
kutokana na kujishughulisha na kazi hizo na
hivyo kusababisha wilaya hiyo kuwa nyuma katika elimu.
Ofisa Elimu shule za Msingi Wilayani chunya
Ally Mbawala alisema kuwa watoto walio wengi wa shule za msingi hawasomi na
hata wazazi wa watoto hao wamekuwa hawana mwamko wa elimu,hivyo watoto wao
wamekuwa wakiacha shule kabisa na kukimbilia kuvua samaki na kutafuta dhahabu
na kuchunga mifugo .
“Tatizo
hili kama wilaya linatuumiza vichwa
uongozi wa wilaya unafanya jitihada kwa kushirikisha wazazi na walezi ili
kuweza kulimaliza tatizo hilo la utoro kwa wanafunzi wa shule za msingi ambalo
kwa kiasi kikubwa limeweza kuathiri kiwango cha elimu kwa watoto hao’’,alisisitiza.
Uchunguzi
pia umebaini kuwa zaidi ya wanafunzi 500 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha
kwanza katika Shule mbali mbali za Sekondari Wilayani Chunya msimu huu
wameshindwa kuripoti Mashuleni kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo
kujiingiza katika biashara za uchimbaji wa Madini,kuchunga mifugo na Uvuvi.
Kutokana
na hali hiyo Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Deodatus Kinawiro, amewataka Wazazi wa
Wanafunzi hao kuhakikisha wanawapeleka watoto wao Shuleni haraka kabla ya
kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa mzazi atakayekaidi agizo hilo.
Taarifa
kutoka kwa Afisa elimu wa Wilaya hiyo inaonyesha kukithiri kwa utoro wa wanafunzi mashuleni,na
kuifanya Serikali kushindwa kufikia malengo yake ya kufuta ujinga miongoni mwa
wananchi.
Kinawiro
alibainisha kuwa Wilaya ya Chunya inakabiliwa na Wimbi kubwa la wafugaji wenye
tabia ya kuhamahama jambo ambalo husababisha kuwakatisha masomo wanafunzi ili
hali wengine wakijikita kwenye shughuli za uchimbaji wa madini na uvuvi katika
Ziwa Rukwa.
Alisema
operesheni ya kuwasaka wazazi na walezi wanaoshindwa kuwapeleka watoto wao
shule itakuwa ni ya kudumu na kusisitiza kuwa mzazi yeyote ambaye hatampeleka
Mwanaye Shule bila kujali kisingizio cha aina yoyote atakamatwa na kufikishwa
mahakamani kujibu mashtaka ya kumwachisha masomo mwanafunzi na kumpatia ajira
kinyume cha Sheria.
Mkuu
huyo wa Wilaya alisema Idadi ya watoto 500 ni kubwa sana hivyo hali hiyo
ikiachwa itazalisha Wajinga wengi jambo ambalo litakuwa mzigo kwa taifa na
kwamba vijana wengine wanaweza katika uhalifu baada ya kukosa fedha kutokana na
ajira walizojiingiza katika umri mdogo.
Hata
hivyo Kinawiro alisema Wilaya ya Chunya
kitaaluma inafanya Vizuri katika ngazi ya Mkoa ukilinganisha na Wilaya zingine
za mkoa wa Mbeya na kwamba hayupo tayari kuona sifa hiyo inapotea kutokana na wazazi
wachache kuzembea na kutokujua umuhimu wa kumsomesha mtoto, na kuongeza kuwa
Halmashauri inaunga mkono juhudi za Serikali kwa kuimarisha ujenzi wa Mabweni
ili kuhakikisha watoto wa kike hawakatizwi masomo kutokana na mimba
zisizotarajiwa.
Kwa mujibu wa Takwimu za Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, wasichana 8000 kila mwaka huacha shule kutokana na ujauzito.
Kati yao 3,000 ni wanafunzi wa shule za msingi.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129


No comments:
Post a Comment