Saturday, July 6, 2013

Makampuni ya mabasi Chunya yatishia kusitisha safari



 Ni kutokana na unyanyasaji wa polisi
 Na Albano Midelo
WAKAZI wa Bonde la Songwe wilayani Chunya mkoani Mbeya wametoa mwito kwa mkuu wa wilaya na mbunge wa jimbo hilo kusaidia kupambana na askari polisi ambao wamekuwa wanadaiwa kuyanyanyasa makampuni ya mabasi yanayotoa huduma za usafiri wa abiria.
Mbunge wa jimbo la Songwe Philipo Mulugo
Askari  polisi wanaopangwa barabara ya Mbalizi  wilayani Mbeya na wa kituo kidogo cha Galula wilayani Chunya wamekuwa wanadaiwa kuomba rushwa waziwazi kwa makampuni ya usafirishaji wa abiria katika  barabara ya Mbalizi,Galula hadi Mbuyuni na Mbalizi hadi Mkwajuni hali ambayo imekuwa kero kubwa kwa wafanyakazi wa makampuni ya usafirishaji wa abiria katika barabara hizo.
Makampuni ya mabasi ya abiria ambayo yanakumbwa na kero ya askari kuwaomba pesa tena bila kuandikiwa risiti ni pamoja na  BOY SASA EXPRESS,G.M SAFARIS na Kampuni ya KANYEGELE ambapo imekuwa ni jambo la kawaida kwa wafanyakazi wa mabasi hayo kutenga fedha kwa ajili ya askari wa barabarani kila siku.
Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatus Kinawiro
Wafanyakazi wa kampuni ya mabasi ya abiria ya GM Safaris ambayo inasafirisha abiria kila siku kutoka Mbalizi hadi Mbuyuni wilayani Chunya wametishia kusitisha safari katika barabara hiyo kutokana na kero kubwa inayofanywa na polisi kudai rushwa ambapo kila siku  wanatumia kati ya shilingi 50,000  hadi 100,000 kuwapa askari polisi wanakuwa katika barabara hiyo.

Uchunguzi umebaini kuwa makampuni mengine ya mabasi ya abiria kwa miaka ya nyuma katika barabara hiyo yaliamua kusitisha kutoa huduma kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya askari polisi kudaiwa kuwatoza pesa nyingi za rushwa bila kuandikiwa risiti hivyo mabasi kufanya biashara ya usafiri kwa hasara kubwa hali iliyosababisha kusimamisha huduma na wananchi kuendelea kuteseka kwa miaka mingi kusafiri kwa kutumia magari ya mizigo.
Wafanyakazi wa Kampuni hiyo ambayo imeanza kusafirisha abiria katika barabara hiyo kwa takribani wiki mbili sasa,wamedai kuwa hawawezi kuendelea kutoa huduma katika barabara hiyo kutokana na askari polisi kila siku wanadai kiwango kikubwa cha pesa tena bila kosa na kwamba fedha hizo wanachukua bila kuandikiwa risiti yeyote.
Mwandishi wa habari hizi ambaye siku ya Juni saba mwaka huu alipanda basi la kampuni hiyo lenye namba za usajiri T.793 BNF akiwa amekaa kiti cha kwanza alishuhudia askari polisi wakimtaka kondakta wa basi hilo kuwapa kiwango cha pesa walichapanga wao wenyewe tena bila kuandikiwa risiti wala kuambiwa pesa hiyo wanatoa kwa kosa gani.
Hali hiyo imewafanya wafanyakazi wa basi hilo kudai kuwa wakati wowote wanatarajia kuacha kutoa huduma ya usafiri wa abiria katika barabara hiyo ambayo kabla ya kampuni hiyo wananchi walikuwa wanasafiri kwa kutumia magari ya mizigo hivyo kuwa kero kubwa kwa wananchi  na kuhatarisha maisha yao.
John Tarimo mfanyakazi wa basi hilo alisema kabla ya kuanza safari katika barabara hiyo,walikuwa wanatoa huduma kutoka mjini Njombe hadi Ludewa na kwamba askari polisi wa huko hawakuwa wanadai rushwa kubwa kama ilivyo kwa polisi na Mbeya ambao wanadai rushwa bila aibu wala kuogopa.
“Haiwezekani sisi tuendelee kutoa pesa ambayo haina jasho kwa askari ambao wanalipwa mishahara kila mwezi,pesa yote tunamaliza kuwapa askari,wafanyakazi tutawalipa nini, matengenezo ya gari tutafanyia nini kwa kweli polisi wa barabara hii ni kero kubwa sana hali ikiendelea hivi kwa wiki moja  tutasimamisha kutoa huduma ya usafiri wa abiria,wananchi waendelee kutumia magari ya mizigo’’,alisisitiza Tarimo.
“Kero kubwa inayotukabili kila siku barabarani ni pale tunapokutana na trafiki ambao mbaya zaidi wanaomba pesa kwa kujipangia kiwango anachotaka mwenyewe,sasa nauli kiasi gani utawatoza wananchi ili kutimiza mgawo kwa askari hao,gari linadai matengenezo,mafuta,matairi na kuwalipa wafanyakazi mishahara, tangu asubuhi tunajinyima lakini wenzetu wanachukua pesa kiulaini,tulitaka kuleta basi la pili lakini sasa tunaona hii biashara itatushinda’’,alisisitiza Tarimo.
Dreva wa basi hilo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini alidai kuwa askari hao wanabadilisha zamu za kuwa barabarani ambapo asubuhi anapotoka Mbuyuni kwenda Mbalizi  anawapa fedha askari wengine na mchana anaporudi anatoa rushwa kwa askari wengine na kwamba hata kama gari limebeba abiria ambao wote wamekaa kwenye viti askari hao wanadai kupewa pesa.
Baadhi ya abiria waliokuwa wanasafiri katika basi hilo wamewalaani askari polisi hao kutokana na kitendo cha kudai rushwa pesa nyingi hadharani kutoka kwa kampuni hiyo na kwamba wametoa mwito kwa kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya kuwawajibisha askari hao ambao hawastahili kuwa askari.
“Kila mmoja katika basi ameshuhudia namna askari hawa wanavyosimamisha basi hili kuanzia askari wa kituo kidogo cha polisi cha Galula wilayani Chunya hadi askari polisi waliokuwepo  kuanzia eneo la Mshewe hadi Mbalizi wilayani Mbeya ,hatuwezi kukubali basi hili lisimamishe huduma kwa sababu ya tamaa ya kujipatia fedha haramu,ni lazima tutawachongea kwa wakubwa wao’’,alisema John Shitindi mkazi wa Galula.
Joyce Malimali mkazi wa Chang’ombe amemuomba mbunge wa jimbo Songwe Philipo Mlugo ambaye pia ni Naibu waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi kuwasaidia ili askari hao waweze kuwajibishwa kwa kuwa warudisha maendeleo nyuma kutokana na vitendo vyao vya kudai rushwa vinavyowakatisha tamaa wawekezaji katika jimbo la Songwe.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Diwani Athuman
“Sisi wanawake na watoto ndiyo ambao tutapata shida kubwa endapo kweli kampuni hii itasitisha kutoa huduma za usafiri wa abiria kwa kuwa hatuwezi kupanda kwenye magari ya mizigo ambayo yanakuwa yamewekwa mizigo mingi kama vile mifugo na magunia kuchanganywa na watu ni hatari kwa usalama’’,alisema Joyce.
Mkuu wa wilaya ya Chunya Deodatusi Kinawiro  ambaye pia ni mwenyekiti wa ulinzi na usalama wa wilaya hiyo ameahidi kuhakikisha kuwa tatizo hilo linatafutiwa ufumbuzi wa kudumu na kwamba kwa kuanzia atawasiliana na kamanda wa polisi wa mkoa wa Mbeya Diwani Athumani kuwachukulia hatua vijana wake ambao wanakiuka maadili ya jeshi la polisi.
“Haiwezekani polisi kudai kupewa pesa bila kutoa risiti za kuonyesha wanatoa pesa kwa kosa gani na shilingi ngapi,natambua changamoto za usafiri wa mabasi ya abiria katika bonde la Songwe kampuni hiyo ya G.M Safari naitambua nawaomba wasikate tamaa waendelee kutoa huduma hiyo muhimu,kama kuna tatizo tuwasiliane,serikali tutachukua hatua dhidi ya askari wanaokwenda kinyume  cha sheria’’,alisisitiza.
Katika hatua nyingine baadhi ya madereva wa bodaboda katika vijiji vya Galula,Ifuko,Magamba,Chang’ombe na Kanga wilayani Chunya wameelezea adha wanayopata kutoka askari polisi wa kituo kidogo cha polisi cha Galula kuwadai pesa kati ya shilingi 30,000 hadi 100,000 ambayo huwapatia askari hao tena bila kuandikiwa risiti kwa madai kuwa pikipiki zao zina makosa ya barabarani.
Vijana hao ambao hawakutaka majina yao kuwekwa mtandaoni ,walidai kuwa imekuwa ni jambo la kawaida kwa askari hao kushika pikipiki zao kila siku na kwamba askari hao wamefanya huo kuwa ni mradi wao kwa kuwa wanakusanya pesa nyingi ambazo zinaishia kwenye matumbo yao kwa kuwa wanalipa bila kuandikiwa popote na kwamba ukiuliza risiti unaishia kupigwa na pikipiki yako kushikiliwa .
Vitendo vya polisi kudai rushwa vimekuwa vinadaiwa kufanyika karibu kila kona za nchi,hata hivyo ushahidi wa kukiuka maadili ya jeshi la polisi kwa kudai rushwa unaweza kumfukuza kazi polisi,isipokuwa inakuwa ni vigumu kumpeleka mahakamani bila ya ushahidi hali hiyo ndiyo inachangia vitendo  vya kudai rushwa kwa polisi kuendelea.
Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk Edward Hoseah, Akitoa majumuisho katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wabunge Wanaopambana na Rushwa nchini (APNAC),akataka itungwe sheria kali ya kutaka kiongozi au mtumishi wa umma awajibike mara anapokuwa ametuhumiwa kwa jambo lolote aachie ngazi na kupisha uchunguzi kama ilivyo kwa nchi zingine.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:

Post a Comment