Na Albano Midelo
![]() |
| Askofu wa jimbo la Tunduru-Masasi Castory Msemwa |
ASKOFU wa jimbo la
Tunduru-Masasi mhashamu Castory Msemwa ametoa rai kwa waumini wa kanisa
katoliki nchini kuomba kwa ajili ya
miito mitakatifu kutokana na idadi ya wanaojiunga kuendelea kupungua kwa kasi.
Mhashamu Msemwa
alitoa rai hiyo wakati anahubiri katika adhimisho la misa ya shukrani ya
jubilei ya miaka 25 ya upadre,miaka tisa ya uaskofu na miaka 58 ya kuzaliwa
iliyofanyika katika kigango cha Mtulila parokia ya Matola jimboni Njombe .
Akionyesha namna
tatizo la miito mitakatifu linavyoendelea kukua,mhashamu Msemwa anasema wakati
anatimiza miaka 25 ya upadre katika kigango chake cha Mtulila na parokia nzima
ya Matola hakuna hata mseminari mmoja
ambaye yupo seminari kuu hivyo inahitajika kuendelea kuungana kuomba kwa ajili ya miito.
“Siamini kama kweli
hakuna vijana wanaoweza kujiunga na mito mitakatifu katika ngazi ya kigango na
parokia,tunahitaji sala katika familia zetu,kama hatufanyi hivyo tuelewe wazi
kuwa tunamkosea mwenyezi Mungu,kila mmoja wetu amesalimiwa na Mungu lakini
hatutaki kuongea na Mungu,maana yake hatutaki kusali katika familia
zetu,hatutapata mapadre wala watawa’’,alisisitiza.
Amewatahadharisha
waumini katika parokia ya Matola yenye waumini zaidi ya 11,000 kutosahau alama zinazowafanya kuwa wakristo
zikiwemo kushindwa kutoa hadithi za Mungu na kutosali ndani ya familia hali
ambayo imesababisha watoto kutojua hata ishara ya msalaba hadi wanapopata
mafundisho katika shule za msingi hali inayosababisha miito kuwa migumu.
Kwa mujibu wa Askofu
Msemwa,wakati anapewa daraja takatifu mwaka 1987 katika kigango cha Kitulila
pekee kulikuwa na watawa wa kike na wa kiume 27 na kwamba watawa waliongezeka
toka mwaka huo hadi sasa hawazidi watawa 10 licha ya takwimu kuonyesha kuwa
kuwa katika familia kuna ongezeko kubwa la vijana.
Akizungumzia sababu
za waumini wa kanisa katoliki kuhamia madhehebu mengine yakiwemo ya
kilokole,mhashamu Msemwa aliitaja sababu kubwa inayochangia kuongezeka kwa
tatizo hilo kuwa ni wazazi na walezi katika familia wameanza kuzembea kusali
kuacha kulea familia zao katika misingi ya kanisa katoliki hivyo vijana kuamua
kufuata yale wanayoyaona yanapendeza katika masikio yao na kuamua kuokoka.
Ameshauri wazazi na
walezi kuhakikisha kuwa mizizi ya imani ya kanisa inaingia sawasawa kwa watoto
wao ili waweze kuimarishwa zaidi katika imani kwa kuwa ni vigumu kuingia
mbinguni bila kuwa na imani iliyokomaa ambayo inanzia katika ngazi ya familia
na kwamba wazazi na walezi waache kuwategemea makatekista kuimarisha imani.
Xavery Mlelwa paroko wa parokia ya Madunda
ambaye apewahi pia kuwa paroko katika kigango cha Mtulila anasema sehemu kubwa
ya jimbo la Njombe ikiwemo parokia ya Matola yenye waumini zaidi ya 11,000
asilimia kubwa ya watu ni wakristo hivyo ameshauri kwa lengo la kufufua imani
ni vema kuanzia ngazi ya familia.
“Ni kweli sisi
tumelegea katika imani kwa kuwa hatuna changamoto nyingine kama maeneo mengine
ambayo yana waumini wa kiislamu,kumbe ukiishi na mtu ambaye mmetofautiana
kifikra au imani unaweza kujiimarisha zaidi hivyo kwa kuwa tupo watu wa aina
moja tumejisahau na kushindwa kuilinda imani’’,alisema padre Mlelwa.
Baadhi ya waumini na
wanafamilia wa mhashamu Askofu Msemwa wametoa maoni tofauti kuhusu jubilei ya
miaka 25 ya upadre na miaka tisa ya uaskofu ambapo dada yake askofu Msemwa ambaye ni mtawa wa shirika la Vinsent Sr.Lucia
Msemwa alisema kaka yake alionekana mapema kuwa anaweza kuwa mchungaji wa watu.
“Kaka yangu Askofu
Msemwa ambaye ni mtoto wa nne kati ya watoto kumi katika familia yetu,alikuwa
anamsaidia baba kuchunga mifugo mbalimbali
tangu akiwa shule ya msingi na aliendelea kuchunga hadi alipofikia
seminari kuu akirudi likizo alipenda kumsaidia baba kuchunga nadhani alikuwa
anaandaliwa kuwa mchungaji wa watu’’,alisema Sr.Lucia Msemwa dada yake Askofu.
Uchunguzi umebaini
kuwa familia ya Askofu Msemwa tangu awali imejengwa katika imani
iliyokomaa,kutokana na ukweli kuwa kuanzia baba yake mzazi Askofu Msemwa anayeitwa Paulonus Msemwa(93) bado yupo hai
alizaliwa mwaka 1920 katika maisha yake alikuwa mwalimu wa dini (katekista)
hivyo kuwalea watoto wake katika misingi ya imani.
Hali hiyo ilimfanya
mtoto wa kwanza wa mzee Msemwa aliyezaliwa mwaka 1950 anayeitwa Menas Msemwa kufanyakazi ya ukatekista ,pia dada yake
Askofu Msemwa anayeitwa Sr.Lucia Msemwa ni mtawa wa shirika la Vincent lakini
kubwa zaidi familia hiyo kubahatika
kutoa Askofu Desemba 7 mwaka 2004 baada ya Askofu Castory Msemwa kuteuliwa na
Baba mtakatifu kuwa Askofu wa jimbo la Tunduru-Msasi.
“Katika familia yetu
tulipata malezi bora baba yetu mzazi alikuwa ni mwalimu wa dini, mdogo wangu
ni Askofu Msemwa,mimi mwenyewe nilikuwa katekista hadi nilipostaafu,dada yangu alikuwa
kiongozi wa kanisa katika parokia ya Matola,dada yangu mwingine ni sista katika
shirika la Vincent hadi sasa’’,alisema Menasi Msemwa kaka yake Askofu Castory
Msemwa.
Hata hivyo kaka huyo
wa Askofu aliitaja siri kubwa iliyosababisha Askofu Msemwa kupanda kwa haraka
kutoka daraja takatifu la upadre hadi kuteuliwa kuwa Askofu ni sala na maombi na kwamba wazazi wao tangu wakiwa wadogo
waliwawekea msingi wa kusali sala mbalimbali ikiwemo lozari kabla na baada ya
kulala.
Baba mzazi wa Askofu
Msemwa mzee Paulunus Msemwa anasema amefurahia sana jubilei ya miaka 25 ya
upadre wa mtoto wake, na kwamba watoto wake aliwajenga katika misingi ya
kiimani,hata hivyo alidai kilichomfurahisha zaidi ni kuhojiwa,kupigwa picha na
mwandishi wa habari kwa kuwa katika maisha yake yote ya umri wa miaka 93
hajawahi kuandikwa katika chombo chochote cha habari.
“Sijawahi mimi
kuandikwa na chombo cha habari,kwa mara ya kwanza ni leo tu,naona sasa wameona
umuhimu wa familia hii kuandikwa na kuingia kwenye historia ili wengine
watakaosoma au kusikia kuhusu familia hii waweze kujifunza hasa mambo ya imani na kusali kuanzia ngazi ya
familia’’,alisisitiza mzee Msemwa.
Askofu Castory Msemwa
alizaliwa Februari 13,1955 katika kigango cha Kitulila parokia ya Matola jimbo
la Njombe kwa wazazi Paulunus Msemwa na Yulina,alibatizwa Uwemba mwaka
1955,elimu ya msingi kuanzia mwaka 1968 hadi 1973 shule ya msingi Matola,kidato
cha nne sekondari ya Mafinga kati ya mwaka 1974 hadi 1977,alijiunga seminari
ndogo ya Likonde kidato cha tano na sita kati ya mwaka 1978 na 1980.
Mhashamu Msemwa mara
baada ya kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT ,alijiunga na
seminari kuu Peramiho mwaka 1981,alipata daraja takatifu la upadre mwaka 1987
na kuteuliwa na Baba mtakatifu kuwa Askofu wa jimbo la Tunduru-Masasi mwaka
2004.
Mhashamu Msemwa ambaye alifanya jubilei ya miaka 25 ya
upadre mwaka jana, amehitimisha adhimisho la misa ya shukrani ya Jubilei ya
miaka 25 ya upadre wake mwaka huu katika kigango cha Kitulila parokia ya Matola
jimbo la Njombe ambako ni nyumbani kwake alikopatia daraja takatifu la upadre.
Mhashamu Msemwa
kuanzia Oktba 9 hadi 20 alifanya ziara katika parokia saba kati ya 45 za jimbo
la Njombe kwa lengo la kufanya misa za shukrani kwa ajili ya Jubilei ya miaka
25 ya upadre wake .
Katika ziara hiyo ya
misa ya shukrani ya jubilei ya miaka 25 ya upadre mhashamu Msemwa ametoa
sakramenti ya kipaimara kwa watoto 1258 kutoka parokia saba za jimbo la Njombe.
Kati ya watoto hao
parokia ya makete watoto 146,Ikonda watoto 115,Matola 275,Madunda 334,Kifanya
270,kigango cha Boimanda watoto 62 na kigango cha Kitulila ambacho amezaliwa
askofu Msemwa ametoa sakramenti ya kipaimara kwa watoto 56,amefungisha ndoa
jozi tano na kutoa ubatizo kwa watoto kadhaa.
albano.midelo@gmail.com

No comments:
Post a Comment