Tuesday, November 5, 2013

Tatizo la umeme Songea kitendawili


Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu
Na Albano Midelo
“TANESCO wanakata na kurudisha umeme bila taarifa na hata ratiba ya mgao haijulikani hali inasababisha hasara kubwa kwa wananchi ikiwemo kuungua vifaa vya umeme na vyakula vinavyohifadhiwa kwenye majokofu kuharibika’’,anasema diwani wa kata ya mjini manispaa ya Songea Joseph Fuime.
Fuime alidai kuwa tatizo la umeme Songea haliwezi kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kuendelea kutumia   mashine chakavu za kufua umeme ambazo vipuri vyake vinaharibika mara kwa mara badala yake alishauri serikali kuunganisha mkoa wa Ruvuma na umeme wa giridi ya Taifa.
“Serikali iliahidi mara baada ya kuanza kuchimbwa makaa ya mawe ya Ngaka wilayani Mbinga kutajengwa kinu cha kufua umeme katika mji wa Songea hata hivyo tangu mwekezaji ameanza kuchimba makaa ya mawe hadi sasa hakuna dalili za kufungwa kinu hicho pia mwekezaji ameshindwa hata kuwalipa fidia  wananchi wanaoishi katika eneo la mgodi’’,alidai Fuime ambaye pia ni katibu wa CHADEMA mkoa wa Ruvuma.

Uchunguzi uliofanywa katika maeneo mengi  ya mji wa Songea umebaini kuwa vibaka wakati wa usiku wameongezeka na kusababisha nyumba nyingi kukatwa nyanya za madirishani na wengine kuibiwa vitu mbalimbali zikiwemo simu za mikononi,mavazi,kompyuta za mkononi na samani mbalimbali.
Waandishi wanakwama kutuma habari zao kwa haraka na hata vituo vya matangazo vilivyopo mjini Songea vikiwemo Redio Maria,radio Jogoo,TBC Taifa, vinashindwa kurusha matangazo kwa wananchi kutokana na kukatika kwa umeme mara kwa mara.
John Mapunda mfanyabiashara soko kuu la Songea anasema Kukatika kwa umeme na kuwaka bila taarifa katika mji wa Songea kunawasababishia hasara kubwa wafanya biashara wa vyakula hasa wanaouza samaki wabichi kutoka ziwa Viktoria, Tanganyika, Nyasa na bwawa la Mtera ,wao wanatunza samaki hao katika makojofu ambayo yanatumia umeme wa TANESCO hivyo samaki wengi wanaoza.
 “TANESCO katika manispaa ya Songea  inaonyesha dhahiri kuwa mashine zao haziwezi kufua umeme wa kukidhi hata katika mji wa Songea,wananchi tunahoji kwanini umeme huo umesambazwa hadi mji mdogo wa Peramiho  badala ya kusubiri umeme gridi ya Taifa’’,alihoji Mapunda. Frank Mbunda mkazi wa Mahenge mjini Songea anadai kuwa TANESCO wameshindwa kumaliza tatizo sugu la umeme ambalo  linachangia umasikini kwa wakazi wa Songea ambao wanashindwa kufanyakazi zao za kiuchumi.
Mwanaharakati Mohamed Kudeka mkazi wa Songea anatoa wito kwa serikali kuachana na umeme wa majenereta ambao matatizo yake ya kuharibika kwa vipuri yamekuwa yanajirudiarudia na kusababisha kero kubwa kwa wakazi wa mji wa Songea ambao wanashindwa kufanya kazi za kiuchumi na kusababisha umaskini.
“Mchawi ni ugonjwa wa majenereta ambayo vipuli vyake vimechoka na kuchakaa,tumechoka na kero hii kama sio ubovu wa vipuri  utasikia mafuta ya kuendeshea mitambo yamekwisha,mara fundi wa kufunga vipuri anatoka nje ya nchi TANESCO tuambieni ukweli tumechoka’,anasisitiza.
Brighton Mwandata mmiliki wa studio ya kurekodi muziki Matarawe mjini Songea anasema umeme katika mji wa Songea haujapatiwa ufumbuzi wa kudumu anashindwa kurekodi kutokana na tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara wakati mwingine inamgharimu kukodisha jenereta kwa gharama kubwa.
Hassan Juma mwanachuo katika chuo kikuu cha mtakatifu Joseph Songea anasema tatizo la umeme limechangia kuathiri masomo katika kozi yao ya shahada ya sayansi ya kompyuta ambayo inahitaji matumizi ya kompyuta ambayo haiwezi kufanya kazi bila nishati ya umeme.
“Mji wa Songea umebahatika kuwa na vyuo vikuu karibu vitano hivyo serikali inatakiwa kujitahidi kutafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo la umeme ambalo linaathiri maendeleo ya elimu na uchumi kwa ujumla’’,alisisitiza.
 RAIS Jakaya Kikwete mwezi Agosti 2009 alifanya ziara katika mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuangalia shughuli za kimaendeleo pamoja na changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa huo.
  Siku ya kwanza ya ziara yake Rais wakati anapita barabarani akitokea uwanja wa ndege wa Songea wananchi walikuwa wakipiga kelele na kudai umeme huku wamewasha taa mchana  kutokana na hali halisi ya tatizo sugu la umeme katika mji wa Songea ambalo linakwamisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
 Rais Kikwete kwa namna ya pekee aliguswa  na alisikitishwa na kasi ndogo ya kushughulikia ufumbuzi wa tatizo la vipuri vya mashine za kufulia  umeme katika mji wa Songea hali liyosababisha kumwagiza meneja wa TANESCO mkoa wa Ruvuma wakati huo injinia Monica Kebara  kufuatilia ili kujua vipuli vya mashine hizo vipo wapi na alitaka kupata ripoti ya vipuri hivyo na mwenendo  mzima wa matengenezo ili wananchi  wafahamu kila hatua.
Rais Kikwete hakuishia hapo,badala yake aliahidi kuileta mashine mpya ya kufua umeme ambayo aliamini ingeweza kumaliza tatizo la mgawo mkali wa umeme katika mji wa Songea makao makuu ya mkoa wa Ruvuma hivyo mgawo mkali wa umeme kubakia kuwa historia.
Baada ya kufungwa mashine mpya ya Rais Kikwete aina ya  ABC yenye uwezo wa kuzalisha megawati 1.6  angalau tatizo la mgawo mkali katika mji wa Songea lilipungua kwa miaka takribani miaka mitatu,ingawa matatizo ya mafuta na vipuri yaliendelea na kuathiri umeme katika mji wa Songea.
Hata hivyo tatizo la mgawo mkali wa umeme limeongezeka mwaka huu kutokana na kile ambacho kinatajwa na TANESCO kuwa ni kuharibika kwa mashine kutokana na vipuri kuharibika.
Kutokana na tatizo la umeme kuongezeka katika mji wa Songea kaimu mkurugenzi wa shirika la umeme nchini  Mhandisi Felchesmi Mramba wiki iliyopita alilazimika kufanya ziara ya siku moja mjini Songea ili kujionea hali halisi ya tatizo la umeme katika Manispaa ya Songea ambao alisema unatokana  na kuharibika kwa vipuri vya mashine ya kufua umeme aina ya ABC.
Hata hivyo Mramba alithibitisha kuwa vipuri vipya vya mtambo huo  vimeshafika nchini kutoka nchini uholanzi na kwamba mwishoni mwa juma hili ufungaji wa vipuri hivyo ulitarajiwa kukamilika katika mji wa Songea.
Meneja wa TANESCO mkoa wa Ruvuma mwandisi Fransis Maze amekiri kuwa vipuri vipya kutoka Uholanzi tayari vimewasili mjini Songea na wiki hii mafundi wamemaliza kazi ya kuvifunga katika mashine za kuzalishia umeme aina ya ABC.
“Hivi sasa tunasubiri kipuri kimoja aina ya turbo charger ambacho kimekwama Dar es salaam kutokana na taratibu za uwanja wa ndege kutokamilika,tunatarajia hadi mwisho wa mwezi huu Oktoba kifaa hicho kitakuwa kimefika Songea kazi ya kukifunga itachukua takribani masaa mawili hivyo mwanzoni mwa mwezi ujao tatizo la mgawo mkali wa umeme Songea litakuwa limepatiwa ufumbuzi’’,alisema.  
Hata hivyo meneja huyo wa TANESCO mkoa wa Ruvuma  alibainisha kuwa mahitaji ya umeme katika mji wa Songea ni kilowatts 4300 na kwamba umeme unaozalishwa hivi sasa ni kilowatts 3050  hali inayosababisha mgawo mkali wa umeme hasa katika maeneo pembezoni mwa mji.
“Hakuna mgawo mkali katikati ya mji ambako kuna taasisi muhimu ambazo zinahitaji umeme kama vile benki, hospitali, viwanda vidogo,ofisi za serikali,mgawo mkali upo maeneo ya pembezoni mwa mji’’,alisema Maze.
Wakati wakazi wa Songea wanalia na umeme,waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhungo amesema tatizo la umeme nchini lazima litoweke,ndiyo maana serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuongeza uzalishaji wa umeme,ukiwemo mradi wa Kinyelezi ambao utazalisha  Megawati 330 na utagharimu dola za Marekani milioni 350.
 TANESCO kwa kushirikiana na ufadhili wa serikali ya Sweden chini ya shirika lake la SIDA,inaanza utekelezaji wa mradi wa umeme kutoka Makambako mpaka Songea ambapo awali kulikuwa na mpango wa kuweka mradi wa kujenga njia ya umeme wa kilovolti 220 mpaka Madaba na kilovolti 132 kutoka Madaba mpaka Songea.
 Taarifa ya wizara ya nishati na madini inaeleza kuwa ujenzi wa mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa gridi kutoka Makambako hadi Songea ambao utahusisha pia kujenga mifumo ya kusambaza umeme vijijini katika Wilaya za Ludewa, Namtumbo na Mbinga ni hatua muhimu ya kuleta maendeleo endelevu katika mikoa ya Kusini
Wizara ya nishati na madini imedhamiria kupunguza utegemezi wa umeme wa maji kwa kuendeleza vyanzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na umeme utakaozalishwa kwa kutumia makaa ya mawe kupitia miradi ya Kiwira (Megawati 200) na Mchuchuma (Megawati 400).
Sera ya Serikali katika umeme ni kuhakikisha wananchi wengi wanapata nishati ya umeme,ingawa takwimu hivi sasa zinaonesha kuwa wananchi wanaopata nishati ya umeme haizidi asilimia 10 ya wananchi wote nchini na kati ya asilimia 10, ni asilimia moja tu ya wananchi wanaoishi vijijini ndio wanaopata nishati ya umeme.
















No comments:

Post a Comment