Kila
mwezi tembo 850 wanauwawa
Na Albano Midelo
TEMBO waliopo nchini
wanaokadiriwa kuwa sio zaidi ya 70,000
watakuwa wamefutika katika uso wa dunia nchini kwetu miaka michache ijao
endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa kukabiliana na majangili.
Katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyopo kusini mwa Tanzania
ambayo ni Hifadhi ya Taifa kubwa kuliko zote nchini yenye ukubwa wa kilometa za
mraba 20,226 ina tembo zaidi ya 30,000 ,utafiti umebaini kuwa majangili
yamekuwa yanawauwa tembo hao kwa kasi hali inayotishia uwepo wa wanyama hao ndani ya
hifadhi hiyo.
Mkuu wa idara ya
ulinzi katika hifadhi hiyo Paulo Gwaha anasema baadhi ya majangili ambao walikamatwa katika hifadhi hiyo
walikutwa wakitumia silaha za kisasa zikiwemo zile ambao zilitumika katika vita
ya Idd Amini wa Uganda kati ya mwaka 1978 hadi 1979.
Kwa mujibu wa Gwaha Katika kipindi cha mwaka 2010/2011 jumla
ya majangili 745 walikamatwa na kwamba tangu Desemba 2011 hadi kufikia mwezi
Machi mwaka 2012 jumla ya majangili 480 walikamatwa ambapo idadi kubwa ya
majangili walikamatwa kabla hawajasababisha madhara katika hifadhi hiyo.
Takwimu kutoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire za mwaka 2007
zinaonyesha kuwa mwaka huo tembo waliouwawa walikuwa 42,mwaka 2008 tembo 29 na
mwaka 2009 jumla ya tembo 33 waliuwawa.
Utafiti ambao ulifanywa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
mwaka 1985 ulibaini kuwa vitendo vya ujangili ambavyo vilikuwa vinafanywa na
jamii inayozunguka hifadhi hiyo vilisababisha idadi ya tembo katika hifadhi
hiyo kupungua kutoka tembo 2500 hadi kufikia tembo wasiozidi 500 .
Afred Kikoti mhifadhi kutoka Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)
anabainisha kuwa utafiti ambao ulifanywa mwaka 2011 unaonyesha kuwa ujangili
unasababisha katika Tanzania tembo zaidi ya 30 kufa kila siku sawa na tembo 850
kwa mwezi na tembo zaidi ya 10,000 wanauwawa kila mwaka hali inayohatarisha
wanyama hao kufutika katika Tanzania.
Takwimu zinaonyesha kuwa katika pori la akiba la Selous hadi
kufikia mwaka 2007 kulikuwa na tembo zaidi ya 70,000 hata hivyo idadi ya tembo
katika pori hilo imeshuka kutokana na kukithiri kwa ujangili hadi kufikia tembo
43,000 mwaka 2009 ambapo hivi sasa inakadiriwa huenda idadi ya tembo katika pori
hilo imeshuka na kufikia 30,000 tu.
Shehena ya meno ya tembo iliyokamatwa nchini
China mwaka 2012 kutoka hapa nchini ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani
milioni moja na nusu. Wiki mbili kabla ya hapo takribani tani nne za meno ya
Tembo zilikamatwa huko huko HongKong katika nchi ya China.
Matukio
haya mawili ya shehena za meno ya tembo ni sawa na Tembo 900 waliouwawa.Hali
hiyo inadhihirisha wazi kuwa ujangili umeshamiri kwa kasi ya kutisha na
kuhatarisha maisha ya wanyamapori hususani tembo.
Takwimu
za Serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii zinaonyesha kuwa mwaka 2010
hapa nchini jumla ya Tembo 10,000 waliuwawa, takwimu hizo ni sawa na Tembo 37
waliuwawa kila siku.
Kulingana na takwimu hizo hali ilikuwa
mbaya zaidi mwaka 2012 ambapo jumla ya Tembo 23,000 waliuwawa sawa na wastani
wa Tembo 63 kila siku, kutokana na kasi hii ya ujangili, ifikapo mwaka 2018
inakadiriwa Tanzania haitakuwa na Tembo hata mmoja.
Waziri
wa maliasili na utalii Balozi Hamis Kagasheki anatahadharisha kuwa nchi ya
Ivory Coast ambayo ilipewa jina hilo baada ya kuwa na wanyama wengi aina ya
tembo katika bara la Afrika, kutokana na serikali ya nchi hiyo kushindwa
kuwalinda na kuwatunza tembo, hivi sasa nchi hiyo haina mnyama hata mmoja aina
ya tembo.
Takwimu za wizara ya maliasili na utalii
zinaonyesha kuwa bara la Afrika mwaka 1930 lilikuwa na tembo milioni 50 na
kwamba hadi kufikia mwaka 2013 tembo waliobakia katika bara nzima la Afrika
ni laki tano tu.
Kwa mujibu wa takwimu hizo hapa
Tanzania miaka ya 1960 kulikuwa na tembo kati ya 250,000 hadi 300,000 na kwamba
wanyama hao walipungua hadi kufikia
130,000 mwaka 2002 na idadi ya tembo hapa nchini imeendelea kupungua kwa
kasi ambapo hivi sasa takwimu zinaonyesha kuwa inakadiriwa kuna tembo wasiozidi
55,000 tu.
Sera
ya Taifa ya wanyamapori ya mwaka 1998 inaelekeza kuwa aina zote za viumbe hai
zihifadhiwe,wanyamapori wasitumiwe kiasi cha kuifanya idadi yao ipungue na kuwa
katika hatari ya kutoweka,kuinua mchango unaotolewa na wanyamapori katika pato
la Taifa,kuhakikisha kuwa Taifa linaendelea kumiliki wanyamapori na kusimamia
kwa niaba ya wananchi.
Hata
hivyo Kasi ya ujangili inayoendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka inaelezwa kuwa
imechangiwa na mambo mbalimbali yakiwemo
kukua kwa uchumi wa nchi ya China na nchi nyingine za Kusini Mashariki mwa
Asia.
Waziri
Kagasheki amethibitisha kuwa miaka ya karibuni makonteina matatu yaliyosheheni
meno ya tembo yalikamatwa katika nchi za Hong Kong,Vietnam na Philipines ambapo
imebainika kuwa mwanzo wa safari ya makonteina hayo ilikuwa ni bandari ya Dar
es salaam nchini Tanzania.
Ujangili
dhidi ya tembo umeziathiri nchi zote za Afrika zenye Tembo kutokana na
kushamiri kwa Biashara ya Pembe za Ndovu.Hata hivyo utafiti unaonyesha kuwa
nchi za Tanzania, Kongo-DRC na Msumbiji zipo kwenye hatari zaidi ya Tembo wake
wote kutoweka kama ilivyo katika nchi ya Ivory Coast kutokana na nguvu kubwa
waliyonayo wafanyabiashara haramu wa Pembe za Ndovu.
Hata hivyo waziri Kagasheki amezitaja baadhi
ya sababu zilizosababisha kushamiri kwa biashara haramu ya meno ya tembo hapa
nchini kuwa ni umaskini wa watu,rushwa, mmomonyoko wa maadili kwa watumishi wa
umma, mahakama na jeshi la polisi.
“Upo mtandao mkubwa wa watu wenye
fedha,viongozi wa ngazi za juu serikalini,kuna maofisa usalama wa
Taifa,TRA,mtandao unaojihusisha na biashara hii ni mkubwa ndani na nje ya
nchi,unaotumia silaha na teknolojia ya kisasa,kasi ya kuuwawa kwa tembo hivi
sasa inatisha kwa kuwa wanauwawa kwa maelfu’’,alisisitiza.
Waziri Kagasheki ameutaja mkakati wa
wizara yake kuwa ni kuitisha mkutano mkubwa wa kimataifa wa wadau wa utalii
utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu kwa ajili ya kutafuta njia sahihi ya
kudumu katika kutokomeza ujangili wa wanyama hasa tembo katika hifadhi hapa
nchini .
Naibu waziri
wa maliasili na utalii Lazaro Nyalandu anadai kuwa miongoni mwa wanaokwamisha
vita dhidi ya ujangili ni wabunge kutokana na baadhi yao kudaiwa kujihusisha na
biashara ya pembe za ndovu.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli, alisema idadi ya tembo imepungua
sana katika mbuga za wanyama nchini, hali ambayo imefanya idadi sahihi ya tembo
waliobaki kutojulikana hivyo inatakiwa kufanyika utafiti ili kupata takwimu sahihi
za wanyama hao waliopo katika hatari ya kutoweka.
Mwandishi wa habari Julian Rademeyer raia wa Afrika
Kusini,amechunguza mtandao mzima wa biashara haramu ya meno ya tembo.
Mwandishi huyo anasema katika nchi za Kusini Mashariki mwa Asia kama Vietnam,
meno ya tembo yana bei kubwa kuliko
dhahabu na dawa za kulevya.
Anabainisha zaidi kuwa biashara hii imejaa
tamaa za mali na rushwa ya kiwango cha kutisha na kwamba kuna ushahidi wa namna
biashara haramu ya pembe za tembo ilivyotumika kuendeleza vita Msumbiji na
Angola kwa nguvu ya Serikali ya Makaburu wa Afrika ya kusini.
Katika
kitabu hicho Mwandishi anathibitisha kuwa Meno ya tembo huko Asia hutumika kama
mapambo kwa kutengeneza mapambo ya thamani na kwamba meno haya hutumika kama
dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa wanaume na hivyo kusababisha bei yake
kuongezeka.
Wahariri
wa vyombo mbalimbali vya habari hapa nchini katika kuhakikisha kuwa tembo
waliobakia wananusurika wamependekeza maazimio mbalimbali ikiwemo Jeshi la
Wananchi wa Tanzania JWTZ sasa kutumika kulinda hifadhi,serikali kutangaza
rasmi kuwa mauaji ya tembo ni janga la kitaifa pia serikali izuie katika
kipindi maalum utalii wa uwindaji.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129
|
|

No comments:
Post a Comment