Monday, November 25, 2013

Misitu milima ya Livingstone Nyasa yavamiwa


Pichani ni milima ya Livingstone Kihagara Nyasa

Na Albano Midelo
WAKULIMA wanaodaiwa kutokea wilayani Mbinga mkoani Ruvuma wamevamia misitu ya hifadhi ya milima ya Livingstone  iliyopo kando kando mwa ziwa Nyasa mkoani Ruvuma na kuteketeza maelfu ya misitu kwa kuifyeka na kuichoma moto.
Hayo yamefahamika kwenye mafunzo ya  hifadhi ya  ardhi na vyanzo vya maji yaliofadhiliwa na shirika lisilo la kiserikali la The Foundation For Civil Society  na kushirikisha washiriki  60 kutoka vijiji 12 vilivyopo katika kata nne zilizopo kwenye Halmashauri ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na kufanyika katika ukumbi wa Tigo mji mdogo wa Liuli.

Mafunzo hayo ambayo yameendeshwa na  mtandao wa mazingira mkoa wa Ruvuma (RUNEA) yameshirikisha washiriki kutoka kata za Mbambabay,Liuli,Kihagara na Lipingu ambao wameanza kupata athari za kimazingira ambazo zinatokana kuvamiwa,kufyeka na kuchomwa moto milima ya hifadhi ya Livingstone hali iliyosababisha mvua kupungua katika kiwango kikubwa kwa wakazi wa vijiji vya kata hizo.
Washiriki katika mafunzo hayo walidai kuwa eneo kubwa la hifadhi ya milima ya Livingstone limeteketezwa na  wakulima waliotokea wilayani Mbinga ambao wanaendesha kilimo cha kuhamahama na baadhi yao wameanzisha makazi ndani ya mlima wa hifadhi hali iliyosababisha safu wa milima ya livingstone kubakia wazi na kuanza kuleta athari za kimazingira kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa.
Mmoja wa washiriki Onesmo Nkandawile ambaye ni afisa mtendaji wa kata ya Mbambabay alidai kuwa kilimo cha kuhamahama katika mazao ya mpunga na ulezi kinachofanyika kila mwaka kwenye milima ya Livingstone kinateketeza ekari nyingi za misitu ya asili na kusababisha kiwango cha mvua kupungua  ukilinganisha na miaka michache nyuma kabla msitu huo haujavamiwa na kuteketezwa.
“Kwa kweli hali ni mbaya wakulima kutoka wilayani Mbinga  wamevamia msitu wa hifadhi,mkulima mmoja anakata miti ya asili kati ya ekari tatu hadi tano kila mwaka anaichoma miti kisha kulima mpunga na ulezi kwenye milima ya hifadhi,wapo ambao wameanzisha makazi katika milima hiyo,hivi sasa mvua zimepungua  mwambao mwa ziwa Nyasa’’,alisisitiza Nkandawile.
Ameshauri elimu ya utunzaji wa mazingira kutolewa mara kwa mara kwa wakazi  wote kupitia  mikutano ya hadhara pamoja na kuhamasisha upandaji wa miti kila mwaka ili kukabiliana na upungufu mkubwa uliopo hivi sasa kwenye safu za milima ya Livingstone.
Afisa mtendaji wa kata ya Lipingu Michael Milinga anasema misitu ya asili ya milima ya Livingstone katika kata nzima imevamiwa na watu wa kabila la wamatengo ambao walikaribishwa na wenyeji wa mwambao mwa ziwa Nyasa  miaka ya nyuma ambapo hivi sasa wameteketeza msitu wa asili katika milima hiyo kuanzia juu ya milima hadi kandokando  na kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira katika milima hiyo.
Hilda Chua,Monica Njaku,Nathani Mpangala,Abdon Ndunguru na Jerome Ndomba wakazi wa kata ya Kihagara kwa pamoja wameishauri serikali kuwachukulia hatua kali,wote wanaohusika na vitendo vya ukataji miti ovyo na uchomaji moto kwenye hifadhi ya milima ya Livingstone ambao bado wanaendeleza uharibifu unaosababisha milima hiyo kubakia mitupu baada ya maelfu ya misitu kufyeka na kuchomwa moto.
Mwezeshaji katika mafunzo hayo ambaye pia ni afisa wa maliasili na mazingira katika Halmashauri ya wilaya ya Nyasa Bugingo Bugingo alisisitiza shughuli zozote za kibinadamu ikiwemo kilimo haviruhusiwi  katika milima ya hifadhi kama ilivyo kwenye milima ya Livingtone ambayo kisheria imehifadhiwa.
“Ukanda wote wa milima ya Livingstone iliyopo kando kando mwa ziwa Nyasa ni hifadhi ndiyo maana imeingizwa kuwa moja ya vivutio vya utalii,hairuhusiwi  kuguswa na kufanya shughuli zozote za kibinadamu wote waliolima na kuweka makazi wataondolewa kwa mujibu wa sheria’’,alisisitiza Bugingo.
Akitoa mada ya hifadhi wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji,mwezeshaji ambaye pia ni afisa maliasili na mazingira wa wilaya ya Nyasa Bugingo Bugingo  alisema uharibifu wa mazingira ni utekelezaji wa mifumo mibaya ambayo uharibu hali ya asili iliyopo unaotokana na mambo mbalimbali.
Aliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni kukata miti ovyo,kuchoma moto misitu ovyo,kilimo cha umwagiliaji kisicho endelevu,kulima matuta kwa kufuata mteremko na kilimo kwenye miteremko mikali kisichofuata kanuni bora za kilimo na kusababisha mmomonyoko wa udongo na upotevu wa rutuba.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo sababu nyingine za uharibifu wa mazingira ni kufuga mifugo mingi,kuendesha kilimo katika vilele vya milima na kingo za mito,uchimbaji madini,kokoto,mchanga na matofali usiofuata utaratibu. uharibu mazingira  ya misitu,ardhi na vyanzo vya maji.
 Alizitaja athari za  uharibifu wa mazingira kuwa ni pamoja na kutoweka kwa uoto wa asili, kupungua kwa mazao ya misitu kama vile mbao,kuni,asali,uyoga na matunda,kuongezeka kwa joto duniani na kusababisha kutoboka kwa tabaka salama angani(o-zone layer),mafuriko,ukame,jangwa,njaa,uchafuzi wa hewa kutokana na mlundikano wa hewa ukaa(carbon dioxide) na upotevu wa rutuba kutokana na mmomonyoko.

Hata hivyo ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira Bugingo amewashauri  wadau wote kuacha kukata miti ovyo,kudhibiti uchomaji wa moto holela,kupanda na kuitunza miti inayohifadhiwa maji kwenye vilele vya milima na vyanzo vya maji hususani safu za milima ya Livingstone,mito na mabonde yote ya ziwa Nyasa.
Uchunguzi ambao umefanywa na gazeti hili umebaini kuwa kuna idadi kubwa ya watu wameweka makazi ya kudumu na tayari wamefyeka misitu  ya asili kwenye  safu za milima ya Livingstone ambayo awali kulikuwa na wanyamapori wa aina mbalimbali wakiwemo mbega weupe,nyani,sungura ,chui na wanyama wengine ambao  wametoweka baada ya mlima kubaki bila miti  kutokana na kufyekwa miti na kuchomwa  na wavamizi kwa ajili ya kilimo na makazi.
Uchunguzi umebaini kuwa wananchi wameweka makazi na kulima kwenye hifadhi za milima Livingstone baada ya kupata baraka kutoka kwa wanasiasa ambao wamekuwa wanawazuia wataalamu wa maliasili na mazingira  kusimamia sera na sheria za mazingira zinazopiga marufuku shughuli zote za kibinadamu  kwenye hifadhi na vyanzo vya maji.
 Kwa upande wake mwenyekiti wa mtandao wa mazingira mkoa wa Ruvuma (RUNEA) Method Ngerangera ameelezea masikitiko yake kufuatia uharibifu mkubwa ambao umefanywa na wavamizi kwenye milima ya hifadhi ya Livingstone na kusababisha maelfu ya ekari za misitu ya asili kuteketezwa kutokana na kilimo na kuweka makazi.
Hata hivyo Ngerangera ameahidi ofisi yake ambayo inahusika  kulinda na kuzuia uharibifu wa mazingira,itatoa bure miche 500 ya miti ya asili kwa ajili ya kupanda kwenye maeneo ya hifadhi ya milima ya Livingstone ambayo yamebakia wazi hasa katika kata za Liuli,Mbambabay,Kihagara na Lipingu na ametoa mwito kwa serikali kutumia sheria zilizopo ili kuwakamata wote ambao wanaendelea kufyeka misitu na kuchoma moto kila mwaka katika hifadhi ya milima ya Livingstone.

 Kwa mujibu wa sera ya Taifa ya misitu ya mwaka 1998, Tanzania ina karibu hekta milioni 33.5 za misitu ambapo theluthi mbili ya hekta hizo  ipo mashakani kutokana na ukosefu wa usimamizi mzuri hali inayosababisha watu kuvamia na kuharibu misitu kwa ajili ya kilimo,malisho ya mifugo,moto,uchimbaji madini,ujenzi na shughuli nyingine.
Licha ya kwamba hakuna takwimu za kuaminika kuhusu kasi ya kutoweka kwa misitu,inakadiriwa kuwa hapa nchini ni kati ya hekta 130,000 hadi 500,000 za misitu zinafyekwa kila mwaka hali inayokatisha tamaa jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanahitaji miti ili kupunguza hewa ukaa .
Sheria ya usimamizi wa mazingira namba 20 ya mwaka 2004 fungu namba 187 kwa makosa yanayohusu uchafuzi wa mazingira ya maji,hewa,ardhi na uchomaji moto ovyo,pia fungu namba 188 kwa makosa yanayohusu uharibifu wa bioanuwai ,adhabu ya jumla fungu namba 191  inasema kuwa mtu yeyote atakayekiuka chochote cha sheria hiyo akitiwa hatiani atatozwa faini isiyopungua sh.50,000 na isiyozidi milioni 50 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au kisichozidi miaka saba jela ama vyote viwili.


No comments:

Post a Comment