Thursday, November 28, 2013

Vita ya maji yaingia Songea


Baadhi ya wakazi wa Mfaranyaki Songea wakigombea maji
Na Albano Midelo
WAKAZI wa manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wapo katika vita kali ya kugombea maji huku wakiwa katika hatari ya kupata magonjwa kutokana na kutumia maji ya mito na visima ambayo sio safi na salama.
Wakazi hao wameamua kutumia maji hayo kutokana na mgawo mkali wa maji unaofanywa na mamlaka ya maji safi na salama Songea SOUWASA tangu mwezi Septemba mwaka huu.
Uchunguzi ambao umefanywa katika maeneo mbalimbali ya pembezoni na katikati ya mji umebaini kuwa tatizo la maji ni kubwa  ambapo wakazi wake wengi wao wakiwemo wanawake na watoto wanazunguka katika maeneo mbalimbali kutafuta maji ya bomba bila mafanikio hali iliyosababisha wananchi kutumia maji ambayo sio salama.

Christina Komba mkazi wa Mfaranyaki alisema sasa miezi miwili hajapata maji ya bomba kutoka SOUWASA hali ambayo imemlazimisha kutumia maji ya visima ambayo pia yanapatikana kwa shida kutokana na idadi kubwa ya watu wanaotumia maji hayo.
Ngohi Nkondola mkazi wa Mjimwema anasema ni miezi miwili na nusu sasa hawajapata maji kutoka SOUWASA  hata hivyo SOUWASA kila mwisho wa mwezi wamekuwa wanasoma mita na kuleta bili yenye VAT na kwamba baadhi ya mamalishe hulazimika kila siku kutumia sh.10,000 kukodi gari la kubebea maji toka Matogoro umbali wa kilometa saba.
Mwandishi ameshuhudi misululu mirefu ya foleni ya akinamama na watoto wakijipanga kuchota maji kwenye visima asubuhi na jioni katika maeneo karibu yote ya mji wa Songea na kwamba maji yanayotoka kwenye visima hivyo yamepungua hali inayosababisha foleni kubwa ya watu wakisubiri kupata walau ndoo moja ya maji na baadhi yao wanadai kuibiwa ndoo na simu.
Baadhi ya maeneo wananchi wameonekana wanachota maji yenye rangi ya tope huku wadudu wakionekana hali ambayo kiafya yanaweza kusababisha magonjwa mbalimbali yakiwemo ya ngozi na matumbo jambo ambalo linaweza kuathiri nguvukazi.
Veronika Ndunguru mkazi wa Ruhuwiko alisema uhaba wa maji katika mji wa Songea unaendelea kuongezeka kwa kasi kila mwaka  na kwamba mwaka huu hali imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa SOUWASA wameshindwa kabisa kusambaza maji hivyo wananchi wengi wanategemea zaidi maji kutoka kwenye visima na mito.
Mhandisi Jones Salema ni meneja uzalishaji wa maji  SOUWASA  amekiri kuwepo upungufu wa uzalishaji na usambazaji wa maji kwa wakazi wa mji wa Songea ambao   mwezi Oktoba mwaka huu umefikia  meta za ujazo 2150 ukilinganisha na  mwezi Oktoba mwaka jana ulikuwa meta za ujazo 2400 .
“SOUWASA hivi sasa tunazalisha maji kwa siku lita za ujazo milioni mbili tu wakati mahitaji ya maji kwa siku katika mji wa Songea ni lita za ujazo milioni 13,hali ni mbaya sana chanzo tunachokitegemea zaidi ni cha Lipasi ambacho kina uwezo wa kuzalisha mita za ujazo 1287 kwa siku’’,alisema Salema.
Mhandisi Salema amekiri kuwa maji yamepungua katika kiwango cha kutisha kwenye vyanzo vya maji  milima ya Matogoro vinavyotegemewa na SOUWASA kwa takribani miaka mitano sasa mfululizo  kutokana na sababu mbalimbali.
Alizitaja sababu hizo kuwa ni mabadiliko ya tabianchi,kuongezeka kwa idadi ya watu katika manispaa ya Songea ,kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ambazo zinachangia kuharibu vyanzo hivyo kwa kulima na kulisha mifugo kwenye vyanzo hivyo.
Ameyataja matarajio ya muda mrefu ya SOUWASA katika kukabiliana na uhaba wa maji katika mji wa Songea kuwa ni kujenga bwawa kubwa katika chanzo cha Mahiro  ambalo litakuwa na uwezo wa kuzalisha maji lita za ujazo milioni tano pamoja na kujenga bwawa la kuhifadhia maji katika chanzo cha maji cha Luhira darajani lenye uwezo wa meta za ujazo milioni moja na kwamba tayari serikali imetoa sh.milioni 400 kwa ajili ya ujenzi huo.
Hata hivyo Contancia Timoth afisa maji Bonde la ziwa Nyasa ofisi ndogo Songea alisema SOUWASA wanatumia vyanzo vitatu vya maji vya bonde hilo kusambazia maji katika mji wa Songea ambavyo alivitaja vyanzo hivyo vilivyopo milima ya Matogoro kuwa ni Luhira A,Luhira B na Mahiro.
Hata hivyo alisema uharibifu mkubwa wa mazingira unaofanywa katika vyanzo hivyo kutokana na shughuli za kibinadamu umechangia upungufu mkubwa wa maji hali inayosababisha SOUWASA kukosa maji ya kutosha kila mwaka kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba.
“Vyanzo vya maji vimevamiwa,miti iliyokuwa rafiki ya maji kama vile minyonyo, matete na mikuyu imeteketezwa, wananchi wanalima hadi kwenye vyanzo vya maji,sisi kama bonde tumekuwa tunatoa elimu ya mazingira na kuunda jumuiya ya watumia maji lakini bado changamoto ni kubwa’’,alisisitiza.
Kutokana na ukubwa wa tatizo la maji mjini Songea afisa huyo wa maji amewashauri SOUWASA kuangalia uwezekana kupata chanzo kingine kilichopo katika bonde hilo ambapo alikitaja chanzo cha maji cha Lumecha kilichopo takriban kilometa 30 kutoka mjini Songea kinaweza kumaliza tatizo hilo kwa kuwa kina maji ya kutosha.
Utafiti umebaini kuwa chanzo cha maji cha Lumecha kinaweza kutumika kwa zaidi ya miaka 50 ijayo hivyo kumaliza kero kubwa ya uhaba wa maji  inayowakabili wakazi wa mji wa Songea hasa kuanzia mwezi Septemba hadi Desemba kila mwaka.
Meneja uzalishaji wa maji wa SOUWASA mhandisi Jones Salema amekiri kuwa chanzo cha Lumecha kinaweza kumaliza tatizo la maji katika mji wa Songea hata hivyo alisema mradi huo unahitaji pesa nyingi kwa ajili ya gharama za  ujenzi wa chanzo, umeme na kutibu maji.
Uchunguzi umebaini kuwa uvunaji wa miti usiokuwa endelevu uliokuwa unafanywa katika msitu wa serikali wa milima ya Matogoro nje kidogo ya mji wa Songea umeleta athari kubwa za kimazingira na kufanya vyanzo vya maji vinavyotegemewa na SOUWASA kuwa hatarini kutoweka .
Uvunaji wa miti hiyo ulipewa kibali na wizara ya maliasili na utalii kupitia idara ya misitu na nyuki kuhakikisha kuwa miti yote ambayo sio rafiki inavunwa katika msitu wa Matogoro ambao una vyanzo vya maji vya mito ya Luhira unaomwaga maji yake ziwa Nyasa,mto Ruvuma unamwaga maji yake bahari ya Hindi na mto Luegu ambao unazaa mto Rufiji.
Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais Mazingira Dk.Terezya Luoga akizungumzia uvunaji wa miti katika msitu wa Matogoro alisema anakubaliana na utafiti ambao umefanywa wa kuhakikisha kuwa miti yote iliyopo hivi sasa inavunwa na kupandwa miti ya asili ambayo ni rafiki wa maji hata hivyo alisema hakubaliani na uvunaji wa miti usiokuwa endelevu unaofanywa katika msitu huo.
“Mimi ni mzaliwa wa Songea, miaka yote tumekaa Songea na misitu hii ya Matogoro, hatujawahi kukosa maji,lakini hivi sasa wakati wa kiangazi mji wa Songea unapata upungufu mkubwa wa maji,kunakuwa na mgawo mkali wa maji hizi ndizo dalili za awali za uharibifu wa mazingira kwenye msitu huu kwa kuwa mnafanya uvunaji usiokuwa endelevu ”,anasisitiza Dk.Huvisa.
Licha ya uharibifu mkubwa wa mazingira katika vyanzo vya maji vilivyopo kwenye milima ya Matogoro,utafiti umebaini kuwa karibu vyanzo vyote vya maji vinavyozunguka mji wa Songea vimevamiwa  kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kilimo,uchimbaji mchanga,uchimbaji visima holela,mabwawa ya samaki na makazi ya watu.
Sheria ya mazingira namba 57 ya mwaka 2004 inataka shughuli za kibinadamu kufanyika umbali wa meta 60 kutoka katika kingo za mto na kwamba yeyote anaharibu mazingira  anafanya makosa akitiwa hatiani atatozwa faini isiyopungua sh.50,000 na isiyozidi milioni 50 au kifungo kisichopungua miezi mitatu au kisichozidi miaka saba jela ama vyote viwili.
Sera maji ya mwaka 2002 inalenga kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji vilivyopo vinatunzwa,kulindwa na kuendelezwa kwa utaratibu unaozingatia uwiano wa mahitaji ya viumbehai wote.






No comments:

Post a Comment