HATIMAYE shirika la
ugavi wa umeme TANESCO limemaliza kero sugu ya mgawo mkali wa umeme katika
manispaa ya Songea baada ya kufungwa vipuri vipya vya mashine za kuzalishia
umeme.
Kaimu meneja wa
TANESCO mkoa wa Ruvuma mhandisi Timoth Ramadhan alisema katika mahojiano maalum
ofisini kwake mjini Songea kuwa mgawo mkali wa umeme umemalizika baada ya
TANESCO kufanikiwa kufunga vipuri vipya
katika mashine zake zote.
“Mashine tano zote
zinafanyakazi na kuweza kuzalisha umeme wa kilowatt 4600,mahitaji katika mji wa
Songea na Peramiho ni kilowatt 4300 hivyo hivi sasa tunazalisha ziada ya umeme
wa kilowatt 300,mgawo wa umeme haupo kabisa tangu wiki iliyopita’’,alisisitiza
Ramadhan.
Alizitaja aina za mashine
zinazozalisha umeme kuwa ni mashine tatu
za zamani aina ya watisira zilizotolewa
kabla ya uhuru,mashine moja aina ya katapila na mashine moja aina ya ABC
iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete mwaka 2011 ambayo ilizimwa mwezi Oktoba
mwaka huu baada ya kupata hitilafu hali iliyosababisha mgawo mkali wa umeme.
Hata hivyo kaimu
meneja huyo wa TANESCO mkoa wa Ruvuma aliongeza kuwa matengenezo bado
yanaendelea katika mashine nyingine ikiwemo aina ya ABC ambayo hivi sasa inazalisha kilowatt 1200
badala ya kilowatt 1700 na kwamba matengenezo hayo yakikamilika mwezi ujao
mashine hizo zitazalisha umeme wa kilowatt 6800 na kufanya mgawo wa umeme
kubakia kuwa historia.
Kulingana na kaimu
meneja huyo kuanzia wiki ijayo TANESCO Ruvuma inatarajia kuanza kuwaunganishia
umeme wateja 574 walioomba kuunganishiwa umeme tangu mwezi Mei mwaka huu kutoka
katika wilaya za Tunduru,Mbinga,Namtumbo na Songea.
Hata hivyo alisema
kuchelewa kuwaunganishia umeme kumetokana na TANESCO kukosa waya mnene
unaoanzia kwenye nguzo hadi kwenye mita ambapo waya huo tayari umepatikana na
kuanzia wiki ijayo wanaanza kazi ya kuwaunganishia kulingana na wateja
waliowahi kuomba.
Baadhi ya wakazi wa
mji wa Songea wamelipongeza shirika la umeme nchini kumaliza mgawo wa muda
mrefu wa umeme katika manispaa ya Songea ambao walidai ulikuwa kero kubwa na
kuchangia kukwamisha shughuli za kiuchumi.
John Haule
ameipongeza serikali kwa kusikiliza kilio cha wananchi wa Songea na kusisitiza
kuwa sasa huduma ya umeme inapatikana kwa uhakika saa 24 bila umeme kukatika ovyo huku na
kuongeza kuwa maendeleo yanaweza kupatikana kwa kuwa umeme ni muhimu katika
shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mwandishi ameshuhudia
karibu kila mahali katika mjini Songea
na Peramiho wananchi wakifurahia huduma bora ya umeme ambao kwa wiki tatu
mfululizo sasa hakuna mgawo wa umeme kama uliokuwepo awali kabla ya kufungwa
vipuri vipya mwezi huu.
Tatizo la mgawo
mkali wa umeme liliongezeka mwaka huu mjini Songea kutokana na kile ambacho
kilielezwa na TANESCO mkoa wa Ruvuma kuwa ni kuharibika kwa vipuri vya mashine
za kuzalishia umeme hali iliyosababisha umeme kuzalishwa kilowatt 3050 tu kati
ya mahitaji ya umeme wa kilowatt 4300 .
Kutokana
na tatizo la umeme kuongezeka katika mji wa Songea kaimu mkurugenzi wa shirika
la umeme nchini Mhandisi Felchesmi
Mramba mwezi Oktoba alilazimika kufanya ziara ya siku moja mjini Songea ili
kujionea hali halisi ya tatizo la umeme katika Manispaa ya Songea ambao alisema
unatokana na kuharibika kwa vipuri vya mashine ya kufua umeme aina ya
ABC.
Serikali
kupitia wizara ya nishati na madini iliagiza vipuri vipya vya mitambo ya kufua
umeme kutoka nchini uholanzi na
kuvifunga katika mashine za kuzalishia umeme hali iliyomaliza tatizo la mgawo
mkali wa umeme katika mji wa Songea kuanzia mwezi Novemba.
Hata hivyo TANESCO kwa kushirikiana na ufadhili wa serikali ya Sweden
chini ya shirika lake la SIDA,inaanza utekelezaji wa mradi wa umeme kutoka
Makambako mpaka Songea.
Taarifa ya wizara ya nishati na madini
inaeleza kuwa ujenzi wa mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa gridi kutoka
Makambako hadi Songea ambao utahusisha pia kujenga mifumo ya kusambaza umeme
vijijini katika Wilaya za Ludewa, Namtumbo na Mbinga ni hatua muhimu ya kuleta
maendeleo endelevu katika mikoa ya Kusini.
Sera
ya Serikali katika umeme ni kuhakikisha wananchi wengi wanapata nishati ya
umeme,ingawa takwimu hivi sasa zinaonesha kuwa wananchi wanaopata nishati ya
umeme haizidi asilimia 10 ya wananchi wote nchini na kati ya asilimia 10, ni
asilimia moja tu ya wananchi wanaoishi vijijini ndio wanaopata nishati ya
umeme.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment