Monday, December 2, 2013

UKIMWI bado tishio

 Serikali imesema kuwa, Ukimwi bado ni tishio kubwa nchini kutokana na kasi kubwa ya maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha ugonjwa huo, (VVU).
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Billal, wakati akihutubia mamia ya wananchi katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi duniani, ambayo kitaifa yaliyofanyika viwanja vya
Mnazi Mmoja, jana jijini Dar es Salaam.
Bilal alisema maambukizi ya mapya kwa dunia nzima kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Ukimwi (UNAIDS), ni watu milioni 2.3 na kwa Tanzania pekee ina zaidi ya watu milioni 1.5, Dk. Billal, alitaja baadhi ya sababu zilizochangia kuongezeka kwa maambukizi hayo mapya kuwa ni pamoja na watu kufanya tendo la ndoa kinyume cha maumbile, kuendesha biashara ya ngono, wanaume wengi kutotahiriwa, uelewa mdogo wa elimu kuhusu Ukimwi hasa kwa vijana wa kike.



Mengine ni  ndoa za utotoni, madereva wanaofanya safari ndefu wanapoendesha magari ya mizigo, kambi za uvuvi, maeneo ya migodini na  kwenye kambi inakojengwa miundombinu ikiwamo ya barabara.

Kwa mujibu wa Dk. Billal, maambukizi hayo yamepunguza nguvu kazi ya taifa kwani watanzaia wengi wamepoteza maisha huku wengine wakiishi na VVU.

Kutokana na hilo, aliwataka wanaume wote ambao bado hawajatahiriwa kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kufanyiwa tohara huku akiziagiza mamlaka na idara husika za serikali ambazo ni pamoja na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids), kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha kiwango hicho cha maambukizi kinapungua nchini  hadi kufikia asilimia sifuri ifikapo mwaka 2015.

Pia aliwataka wazazi na walezi wanaoishi na watoto wenye  maambukizi hayo kuanzia miaka miwili, wawapeleke kwenye vituo vya afya ili waweze kupatiwa dawa za kupunguza makali ya VVU.

MKAKATI WA TATU KUDHIBITI UKIMWI

Dk. Billal pia alizindua mkakati wa tatu wa taifa wa kudhibiti Ukimwi na kukabidhi mashine 37 za kupima kiwango cha makali cha Ukimwi, CD4, zilizogharimu zaidi ya Sh. bilioni moja, kwa wakuu wa mikoa minne ya nyanda za juu Kusini, ikiwa ni moja ya mkakati wa serikali kupiga vita ugonjwa huo.

Mkakati huo unafuatia ule wa kwanza uliozinduliwa na Rais Jakaya Kikwete mwaka jana wa sifuri tatu, ukiwa na maana ya  kupunguza maambukizi mapya, vifo na unyanyapaa vyote kufikia asilimia 0.

Mikoa iliyokabidhiwa mashine hizo ni pamoja na Ruvuma, Rukwa, Mbeya na Katavi.

Hata hivyo, Dk. Billal, alisema, mbali na maambukizi hayo mapya, alisema viwango vya wenye Ukimwi vimeshuka kwa asilimia 0.6 kutoka 5.7 hadi  asilimia 5.1.

Alisema utafiti  unaonyesha kuwa maambukizi hayo nchini yamepungua kwa asilimia 0.6 mwaka 2011/2012, kutoka asilimia 5.7 mwaka 2007/2008, huku kwa wanawake yakiendelea kuwa juu kwa asilimia 6.2 na wanaume asilimia 3.8.

Pia alitaja mikoa inayoongoza kwa maambukizi hayo na kiwango kwa asilimia kwenye mabano kuwa ni Njombe (14.8),  Iringa (9.1), Mbeya (9.0), Sinyanga (7.4) na Ruvuma (7.0).

DK: RASHID AZUNGUMZIA
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif  Rashid, alisema sababu nyingine inayochangia maambukizi ya VVU ni pamoja na kuwapo kwa wanaume wengi wasiotahiriwa.

Alisema Serikali bado inaendelea kutekeleza afua ya tohara katika mikoa 12,  yenye viwango vya juu vya maambukizi.

SHEIN AHADHARISHA Z'BAR

Visiwani Zanzibar, wananchi wamehadharishwa kutojenga dhana kuwa asilimia 1.0 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi Zanzibar ni ndogo ikilinganishwa na nchi nyingine zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako maambukizi katika nchi hizo kwa mujibu wa tafiti za mwaka 2011 yalikuwa ni asilimia 4.9.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alitoa tahadhari hiyo  janaalipokuwa akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika kitaifa kwa Zanzibar katika Kijiji cha Paje Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Aliwataka wananchi wa Zanzibar kuzuia maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

 Akitoa takwimu za hivi karibuni, Dk. Shein alinukuu matokeo ya Utafiti wa Viashiria vya Ukimwi na ugonjwa wa Malaria wa mwaka 2012 ambayo yalionyesha kuwa maambukizi  ya virusi hivyo kwa  Zanzibar yameongezeka kwa asilimia 0.4 kutoka asilimia 0.6 mwaka 2008 hadi asilimia 1.0 mwaka 2012.

Alifafanua kuwa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, yanaonyesha kuwa Zanzibar ina watu milioni 1.3 milioni hivyo, ni watu 30,000 ambao ni asilimia moja ya idadi hiyo wanaishi na virusi vya Ukimwi visiwani hapa.

Awali, akizungumza katika maadhimisho hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Zanzibar, Profesa Saleh Mohamed Idrissa, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, tume hiyo imepanua huduma na tiba kwa mujibu wa Mwongozo wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kwa wenye virusi vya kiwango cha CD4 350 badala ya kile cha zamani cha CD4 200.

MAKUNDI YAVAMIA MORO

Nao Mji wa Morogoro mkoani hapa umevamiwa na makundi maalumu ya vijana yanayojihusisha na biashara ya ngono, usagaji na ushoga katika vilabu  za burudani na kupelekea kuwepo kwa tishio la kuongezeka kwa kasi ya maambukizi ya Ukimwi.

Makundi hayo yametajwa ni ya wanawake wanaouza, wanaume na wanaojidunga sindano za madawa ya kulevya kwa kupokeza.

Akizungumza katika kikao kilichoshirikisha  Madiwani wa Halmashauri hiyo  kuhusu Maadhimisho ya  Ukimwi Duniani,Naibu Meya wake Lyady Mbiaji alisema makundi hayo yanaundwa na wanafunzi wa sekondari, vyuo vikuu na wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Akitoa mada katika maadhimisho hayo kwa makundi hayo maalumu, Meneja wa Shirika la PSI Tanzania Mkoa wa Morogoro, Godwin Msafiri aliitadhalisha Manispaa hiyo isipoyadhibiti makundi hayo kwa kutoa elimu maalumu hali ya ukimwi itakuwa mbaya na hivyo uchumi wa mkoa kushuka. 

 Kwa upande wake Mkuu wa wilaya  ya Tandahimba mkoani Mtwara,  Ponsiano Nyami jana alisusia maadhimisho hayo ambayo kiwilaya yalifanyika Kijiji cha Litehu
Mkuu huyo wa wilaya ambaye alikuwa mgeni rasmi aliwasili katika viwanja hivyo majira ya  saa 4:20 asubuhi na kukuta maandalizi yakiwa bado yanaendelea.

Mara baada ya kuwasili kwenye viwanja hivyo,  alisaini kitabu cha wagen kisha kuondoka licha ya baadhi ya viongozi  kumsihi kuwa na subira.

Nyami alisema hiyo ilikuwa mara yake pili kufika kiwanjani hapo baada ya  saa 3 asubuhi na maandalizi bado yakiendelea.

"Nimefika saa tatu nikakuta hawajaanza nikaondoka badaye nikapiga simu nikaambiwa tayari wameeanza nimefika sikuti wahusika, "alisema Nyami na kuongeza kuwa"Naondoka naenda kuwandikia barua ya uzembe."

Kwa mujibu wa ratiba ya hafla hiyo mgeni rasmi alipaswa kuwasili kati ya saa 3:30 na saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya kufungua maadhimisho hayo.
Akizungumzia tukio hilo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Peter Nambunga alisema ratiba ya shughuli hiyo haikufuatwa kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake.

Alisema baada ya mkuu wa wilaya hiyo kuondoka, mwenyekiti wa halmashauri hiyo,  Ali Ndingo alichukua nafasi ya kuwa mgeni rasmi
Imeandikwa na Isaya Kisimbilu;  Loveness Massero; Elizabeth Zaya, Ashton Balaigwa, Morogoro na Mariam Maregesi Mtwara.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment