Na Albano
Midelo,Nyasa
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi
Tanzania (TAFIRI) Dk.Benjamin Ngatunga
amethibitisha utafiti kubaini kuwa samaki wanaokutwa wamekufa wenyewe
katika ziwa Nyasa hawana madhara kwa walaji.
Akizungumza katika
mahojiano na gazeti hili Dk.Ngatunga alisema utafiti uliofanyika hivi karibuni
katika ziwa Nyasa upande wa Tanzania na Malawi umebaini kuwa tatizo la vifo vya
samaki katika ziwa hilo vimekuwa
vinatokea na kusababishwa na mabadiliko ya mkondo wa maji ambao unatokea
katika ziwa hilo kila baada ya kati ya miaka 15 na 20 .
“Miaka yote maji ya
juu na ya chini ya ziwa huwa
hayachanganyiki, hata hivyo kila baada ya miaka kati ya 15 na 20 maji ya chini yanaweza kuwa mita 600 na kuchanganyika na maji ya juu yaliyopo mita 200 tu kwa hiyo maji ya
chini ambayo hayana oksjeni yanapofika juu husababisha samaki wakose hewa na hatimaye kufa’’,alisema.
Hata hivyo
alibainisha kuwa samaki wanaokufa katika ziwa Nyasa wanaweza kuliwa, amewataka
wananchi kuondoa utumbo katika samaki waliokufa wenyewe kabla ya kula na kwamba
wanapokula samaki bila kutoa utumbo wanakuwa na radha ya chungu sana na kusisitiza ukiachia uchungu hakuna madhara
yanayoweza kutokea kiafya kwa walaji.
Aliongeza kuwa mwaka
huu kati ya mwezi Machi hadi Mei tatizo la samaki kufa ovyo katika ziwa Nyasa
lilitokea na idadi ya samaki waliokufa ilikuwa ni kubwa zaidi ukilinganisha na
miaka 15 iliyopita ndiyo maana wananchi walikuwa na hofu kubwa kwa kuwa waliona ni tukio jipya
kwao.
Kulingana na
Dk.Ngatunga vifo vya samaki katika ziwa Nyasa mwaka huu havikutokea upande wa
Tanzania pekee,bali hata ziwa Nyasa nchini Malawi vifo vya samaki vilikuwa ni vingi zaidi ya
vile vilivyotokea upande wa Tanzania hali
ambayo ilizua hofu kubwa kwa wakazi wa Malawi kuanzia mwezi Februari mwaka huu.
Amewashauri watafiti
na wataalamu kuendelea kutoa elimu sahihi kuhusiana na vifo vya samaki
vinavyotokea katika ziwa Nyasa na kuwaasa wanasiasa kuacha kueneza taarifa ambazo
sio za kisayansi kuhusiana na vifo vya samaki hali ambayo inawatia hofu
wananchi wa pande zote za ziwa Nyasa Tanzania
na Malawi.
Kwa upande wake waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa
Rais (Mazingira), Dk.Teresa Huvisa, akizungumza na wananchi mwambao mwa ziwa
Nyasa alikiri kupata taarifa kuwa samaki wanaokufa katika Ziwa Nyasa wamekuwa
wanaleta hofu kwa wananchi wa nchi zote mbili Tanzania na Malawi, na kwamba
wizara yake imetuma wataalamu kufanya uchunguzi
wa vifo vya samaki ili kubaini kiini cha tatizo hilo iwapo linachangiwa
na uchafuzi wa mazingira katika ziwa Nyasa.
Hata hivyo alisema kuna baadhi ya wavuvi wanatumia
majani yanayoitwa mtunungu kuvulia samaki ambayo ukimwaga ziwani au mtoni
samaki wanakufa, na kuwatahadharisha wavuvi waache kutumia njia haramu za uvuvi
ili kutoharibu mazalia na kuuwa samaki.
Hata hivyo kuanzia mwezi Septemba mwaka huu idadi
ya vifo vya samaki wanaokufa wenyewe katika ziwa Nyasa imepungua na baadhi ya
maeneo hakuna samaki wanaokufa kabisa.Uchunguzi umebaini vifo vya samaki bado
vinatokea katika maeneo ya Ndumbi na Lituhi.
Baadhi ya
wavuvi waliohojiwa katika eneo la Ndumbi mwambao mwa ziwa Nyasa wamedai
kuwa samaki wana tabia ya kula vumbivumbi za makaa ya mawe ambazo zimetapaa
katika bandari ya Ndumbi ambayo inatumika kusafirishia makaa ya mawe.
Fransis Chuwi mvuvi wa Ndumbi akizungumza kwa
niaba ya wenzake alidai kuwa wao kama
wavuvi wamebaini kuwa vifo vya samaki vilianzia
ukanda wa Lituhi na Ndumbi kabla ya kuenea maeneo mengine kama Liuli na
Mbambabay na kudai kuwa sababu kubwa ni vumbi la makaa ya mawe
kuliwa na samaki katika bandari ya Ndumbi.
“Vumbivumbi la makaa ya mawe ndiyo chanzo cha vifo vya samaki katika
bandari ya Ndumbi,sisi kama wavuvi
tumegundua kuwa wanaposimamisha kupitisha makaa ya mawe katika bandari ya
Ndumbi vifo vya samaki vinapungua,miezi mitatu iliyopita walipitisha makaa ya
mawe kwa wingi na samaki wengi
walikufa,hivi sasa wametulia kidogo na samaki wamepumzika kufa hivyo sisi
tumegundua tatizo ni makaa ya mawe’’,alidai mvuvi huyo.
Dk.Ngatunga
mkurugenzi wa TAFIRI nchini amepinga
madai ya wavuvi hao kudai vumbi la makaa ya mawe kusababisha vifo vya samaki na
kusisitiza kuwa wavuvi wanaongea jambo ambalo halijafanyiwa utafiti wa
kisayansi ambao TAFIRI imechunguza katika nchi mbili na kubaini tatizo la vifo
vya samaki ni mabadiliko ya mkondo wa maji katika ziwa na sio vinginevyo.
Mwaka huu kati ya
mwezi Machina Mei idadi kubwa ya samaki
katika ziwa Nyasa walionekana kufa ovyo na
kuelea ndani ya ziwa Nyasa kwenye maeneo ya kata tano za Lituhi,
Kihagara Liuli, Lipingo,Mtipwili hadi vijiji vya mpakani na nchi ya Msumbiji.
Samweli Kaseke na
Isack Kamanga wavuvi wa forodha ya Hongi na Nkali kata ya Liuli waliwataja aina ya samaki ambao walioongoza kufa kwa
wingi kuwa ni pamoja na ligong’wa, njeringu ,likuku, vindongo, vigong’o,
vituhi, hango, ngisi,mbufu,lihenji,magege na batazibi.
Kaimu afisa Uvuvi wa wilaya ya Nyasa Joseph Mwingira alisema utafiti wa awali ulibaini
kuwa samaki wanaokufa na kuelea juu ya
maji walionekana kuwa na majeraha ya kubabuka katika sehemu mbalimbali za mwili
zikiwemo usoni,tumboni,kichwani,mkiani na
mgongoni.
Kulingana na utafiti ambao ulifanywa na jumuiya ya nchi zilizo kusini
mwa Afrika(SADC) kwa kushirikiana na
nchi ya Uingereza kwenye ziwa Nyasa kati ya mwaka 1991 hadi 1994 na
mwaka 1996 hadi 2000,ulionesha kuwa ziwa hilo lina kiasi cha tani 165,000 za
samaki na kati ya kiasi hicho tani 35,000 za samaki ni jamii ya samaki wa maji
ya juu ambao wanaweza kuvuliwa bila kuathiri uvuvi kila mwaka.
Ziwa Nyasa limezungukwa na nchi tatu
ambazo ni Tanzania,Malawi na Msumbuji.Ziwa hilo lipo kwenye usawa wa meta 500
toka usawa wa bahari, kina cha ziwa hilo ni karibu meta 750,urefu wake ni karibu
kilometa 1000,upana mkubwa ni kilometa 80 na upana mdogo ni kilometa 15.
albano.midelo@gmail.com,simu 0766463129

No comments:
Post a Comment