Friday, February 14, 2014

Malaria inauwa watu 290 kila siku


Na Albano Midelo
Kila saa watu 10 wanakufa kwa malaria
UGONJWA wa malaria umeuwa watu  652 katika mkoa wa Ruvuma mwaka 2011 kati ya wagonjwa  zaidi ya 43,000 waliougua ugonjwa huo katika kipindi hicho.

 Mratibu wa malaria mkoani Ruvuma  Kibua Kakolwa anabainisha kuwa  kati ya wagonjwa waliopoteza maisha  watoto chini ya umri wa miaka mitano walikuwa  334 na wenye umri wa zaidi ya miaka mitano walikuwa 318.


Kwa mujibu wa mratibu huyo wa malaria katika mwaka huo pekee mkoa ulilaza wagonjwa wenye umri chini ya miaka mitano wapatao 21,940 na walio zaidi ya umri huo walikuwa 21,819.

“Katika mkoa wa Ruvuma ugonjwa wa malaria bado ni tishio katika wilaya zote tano za Songea,Mbinga,Nyasa,Namtumbo na Tunduru na unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi ukilinganisha na magonjwa mengine kwa mfano katika kipindi cha kuanzia mwaka 2008 hadi 2011 malaria imeuwa watu 3,451’’,alisema.

Takwimu za mwaka jana za mkoa zinaonyesha kuwa  idadi ya wagonjwa wa nje wa malaria wenye umri chini ya miaka mitano  walikuwa 216,311 ambao ni sawa na asilimia 45 ya wagonjwa waliopokelewa na wagonjwa wenye umri zaidi ya miaka mitano walikuwa 207,664  sawa  asilimia 40 ya wagonjwa wote.

Hata hivyo Kakolwa alisema katika miaka mitatu mfululizo takwimu zinaonesha wagonjwa wa malaria wamepungua kwa wastani wa asilimia 6.5 na vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vimeweza kupungua kwa wastani wa asilimia 15.4 na kwamba  vyandarua 706,219 vilivyogawiwa kwa wananchi vimechangia kupunguza ugonjwa wa malaria.

Takwimu za kitaifa zinaonyesha kuwa ugonjwa  wa malaria bado ni  tatizo kubwa hapa nchini  kwa kuwa ugonjwa huo  ndiyo unaoongoza kwa kusababisha idadi kubwa ya vifo ambapo watanzania kati ya 60,000 hadi 80,000 wanakufa kutokana na ugonjwa huo kila mwaka.

 Kwa mujibu wa takwimu hizo kila siku watu 291 wanapoteza maisha  kutokana na ugonjwa wa malaria wengi wao ni watoto chini ya miaka mitano, kwa maneno mengine katika kila saa moja wanakufa watu zaidi ya 10 kwa ugonjwa wa malaria.

Kati ya vifo vinavyotokea kila mwaka kutokana na ugonjwa huo asilimia 90 ni vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano na kwamba ugonjwa huo huleta athari nyingi za kiuchumi na kusababisha kupunguza pato la taifa la ndani kwa asilimia 3.4 kila mwaka.

Asilimia 93 ya watanzania wanaugua malaria
Inakadiriwa kuwa  zaidi ya asilimia 93 ya watanzania wanaokadiriwa kufikia zaidi ya milioni 45 wapo katika hatari ya kuambukizwa malaria na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya tatu duniani kuwa na idadi kubwa ya watu wengi walio katika hali hatarishi ya kuambukizwa malaria.

Takwimu zinaonesha kuwa ugonjwa wa malaria unasababisha zaidi ya asilimia 33 ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano na vifo zaidi ya asilimia 20 vya akinamama wajawazito.


Hata hivyo takwimu hizo zinaonesha kuwa karibu asilimia 80 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilitokana na ugonjwa wa malaria na kwamba inakadiriwa kiwango cha vifo vya watoto 165 kati ya kila vizazi hai 100,000 kila mwaka vinatokana na ugonjwa wa malaria.

Takwimu kutoka wizara ya afya na ustawi wa jamii zinaonesha kuwa kila mwaka watanzania wapatao milioni 18 wanaugua ugonjwa wa malaria hali ambayo inalifanya taifa kupoteza mapato mengi ambapo inakadiriwa kila mwaka zaidi ya sh. milioni 350 zinapotea kwa ajili ya malaria.

 Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ugonjwa wa malaria ndio unaoongoza kwa mahudhurio ya wagonjwa wanaofika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya, na kwamba matukio takriban 12 milioni ya malaria hutolewa taarifa.


 Juhudi zinaendelea kufanywa na serikali kwa zaidi ya miaka 10 sasa kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa kushirikiana na mashirika mengine yasiyokuwa ya kiserikali na juhudi hizo  zimeanza kuzaa matunda kutokana na takwimu kuonyesha  kuwa idadi ya vifo imepungua ambapo takwimu za awali zilizionesha kuwa watu zaidi ya 100,000 walikufa kila mwaka kutokana na malaria.

Serikali inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete  imeanzisha kampeni kubwa ya kuwafahamisha na kuwaelimisha wananchi katika nchi nzima ya kuhakikisha kuwa ugonjwa wa malaria unatokomezwa.

Moja ya fursa kubwa ambayo imefanywa na serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii ni kugawa vyandarua zaidi ya milioni 20 vyenye dawa ambapo ugawaji huo ulianza kwa kuwapatia watoto chini ya miaka mitano.

Serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii inatekeleza mpango  kuanzia mwaka 2008 hadi 2015 ambapo lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kuwa vifo vinavyotokana na ugonjwa wa malaria vinapungua  kwa asilimia 80 katika idadi ya wagonjwa na vifo.

.        
      Sera ya afya ya mwaka 2007 katika ukurasa wa 16 inatamka wazi kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali zikiwemo jumuiya  za kimataifa itaendelea kuandaa na kuboresha sheria, miongozo na mikakati ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza, milipuko pamoja na yale yanayojirudia na mapya kwa wakati muafaka.

Dalili za malaria hizi hapa
 Watalaamu wa malaria wanasema tiba ya mapema na sahihi dhidi ya ugonjwa huo ni jawabu katika kupunguza idadi kubwa ya vifo na wagonjwa hususani kwa watoto.

Kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa kudhibiti malaria dalili za jumla za malaria ni pamoja na ,homa,maumivu ya kichwa, tumbo kuuma, kuharisha, kichefuchefu, kizunguzungu, kutokwa jasho, kutetemeka,kukosa hamu ya kula, uchovu, kupoteza fahamu,degedege,kutapika,kupoteza fahamu, kupumua kwa shida na kukojoa mkojo wenye rangi kahawia au nyeusi.

Rais Jakaya Kikwete akizungumza wakati anazindua kampeni za kupambana na malaria alisema malaria ni vita ambayo ni lazima kupigana nayo na kuishinda kwa sababu serikali ina uwezo wa kuutokomeza ugonjwa huo hivyo kukifanya kizazi  cha sasa kuwa cha mwisho kuugua na kufa na malaria.

Watalaamu wa afya wanasema kuna njia tatu za kupambana na hata kuutokomeza ugonjwa wa malaria ambao ni kuhakikisha kuwa watu wote wanaougua malaria wanapata tiba sahihi  ambayo ni dawa yenye nguvu ya kuuwa wadudu wanaosababisha ugonjwa wa malaria ambao wamejenga tabia ya kubadilika kimaumbile.

Njia ya pili ya kutokomeza malaria ni kuhakikisha kuwa watu wasiumwe na mbu wa malaria kwa kuhakikisha kuwa wanatumia vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuuwa mbu  hali ambayo itamwezesha  mtu asipate malaria.Akinamama wote wajawazito na watoto wanatakiwa kulala katika vyandarua vyenye dawa kwa kuwa malaria ni chanzo kikuu cha vifo vya wajawazito na watoto chini ya miaka mitano nchini.

Tanzania imepatiwa vyandarua zaidi ya milioni tano kutoka serikali ya  marekani na  Global Fund ambapo serikali inasimamia kuhakikisha kuwa kila kaya angalau imepata  vyandarua viwili vilivyotiwa dawa hivyo kufanya idadi ya mbu wanaokufa kuwa wengi na wananchi  angalau watakuwa wamekingwa na malaria.

Njia ya tatu ya kutokomeza malaria ni kuhakikisha kuwa mbu wanaoambukiza malaria hawaendelei kuzaliana kwa kuwauwa kwenye mazalia yao yote pamoja na sehemu zote ambazo wanatua ili kuwatokomeza kabisa mbu wanaoeneza malaria.

 Wizara imeshindwa kufikia malengo
Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ugonjwa wa Malaria wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ulilenga kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo kwa asilimia 50 hadi kufika 2013.  Kwa maneno mengine, Wizara ililenga kuwapunguza wagonjwa wa malaria hadi kufikia milioni sita na idadi ya vifo kufikia kati ya 30,000  hadi 40,000  mpango ambao bado haujafanikiwa kwa kuwa idadi ya wagonjwa na vifo bado ni kubwa.

Mratibu wa asasi binafsi ya ORES-Tanzania ambayo inashiriki katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria Dr.Hermengild Mayunga anasema ili kufanikisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo inatakiwa kuongezwa ushiriki wa wanasiasa,viongozi wa serikali na jumuiya katika masuala mtambuka juu ya malaria.

“Nasisitiza muingiliano wa kisekta na sekta zisizo za afya katika utekelezaji makini wa hatua au njia za kuzuia na kudhibiti malaria kwa mfano miradi ya tathimini ya madhara ya malaria,mafunzo ya kujenga uwezo kwa sekta za afya na zile zisizo za afya”anasisitiza Dr.Mayunga.

Ikumbukwe kuwa ugonjwa wa malaria hauna mipaka hivyo msisitizo  katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ni lazima kasi iongezwe kila mwaka ili siku moja ugonjwa wa malaria utokomezwe,tuanze kuhesabu siku za ugonjwa wa malaria kuwasumbua watanzania zinakwisha mbona wenzetu wameweza sisi tushindwe kuna nini hapa”,anauliza Dr. Mayunga.

Dr.Mayunga anasisitiza kuwa hivi sasa ni kipindi ambacho wanasayansi wanatakiwa kukumbuka kuibua mbinu mpya, mikakati mipya na utalaamu mpya wa kitafiti katika kutokomeza malaria na kujifunza kutoka katika nchi ambazo tayari zimetokomeza malaria.

Matokeo ya maazimio ya Maraisi  mbalimbali duniani walipokutana mjini Abuja nchini Nigeria Aprili 25 mwaka 2000 walikubaliana mikakati maalum ya miaka kumi katika kuutokomeza ugonjwa wa malaria ambapo matokeo yake yalitakiwa yapimwe mwaka 2010.

Matokeo hayo bado yanaonyesha kuwa ugonjwa huo ni tishio katika maisha na kwamba inatakiwa kuongeza juhudi katika mapambano dhidi ya malaria ili kufikia  kiwango cha asilimia 100 hivyo kufikia idadi sifuri  ya vifo kufikia malengo ya milenia 2025.

Watu milioni 500 wanaugua malaria Duniani
Takwimu kutoka shirika la afya ulimwenguni WHO za mwaka 2002 zinaonyesha kuwa kila mwaka  watu kati ya milioni 300 hadi 500 duniani wanapata ugonjwa wa malaria, kati yao watu milioni moja na nusu wanakufa kutokana na ugonjwa huo.

Kulingana na takwimu hizo katika bara la Afrika  watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano ndiyo wanaathirika zaidi na ugonjwa wa malaria ambapo kila mwaka watoto milioni tano wanakufa kwa ugonjwa huo barani Afrika.

Hata hivyo jambo la kutia moyo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria hapa nchini ni utafiti kuhusu chanjo ya malaria ambao unaendelea kufanywa katika mikoa mbalimbali ukiwemo mkoa wa Morogoro.

Utafiti huo hadi sasa unatia matumaini makubwa ya kupatikana kwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa malaria ambayo ikipatikana hapana shaka utakuwa ndiyo mwisho wa ugonjwa huo ambao unaua watu wengi na kudhoofisha uchumi wa taifa.

No comments:

Post a Comment