Saturday, February 1, 2014

Wanachuo St.Joseph wadai kubaguliwa


Na Albano Midelo
Wanachuo katika chuo kikuu cha mtakatifu Joseph tawi la Songea wanadai kubaguliwa na kunyanyaswa na baadhi ya wahadhiri raia wa India katika chuo hicho ni moja ya sababu zilizowafanya kufanya mgomo kushinikiza uongozi wa chuo kupatia ufumbuzi madai yao.  
wametoa madai mbalimbali ya muda mrefu yaliosababisha kufanya mgomo na vurugu kwa kuwa uongozi wa chuo umeshindwa kuyapatia ufumbuzi hadi sasa.
Wakizungumza huku wakikataa majina yao kuandikwa kuhofia kufukuzwa chuo,waliyataja baadhi ya madai hayo kuwa ni kunyanyaswa na uongozi kwa kukatazwa kuingia chuoni hapo na  vifaa muhimu vya mawasiliano ikiwemo simu na kompyuta ndogo yaani latop.


“Dean of student akikukamata na simu au laptop anakunyang’anya na unarudishiwa vifaa vyako baada ya semester kumalizika kwa kweli tunanyanyaswa sana kufanyiwa mambo haya wanachuo wa chuo kikuu,tunaomba Tume ya vyuo vikuu kuingilia kati suala hili sisi sio wanafunzi wa sekondari’’,alidai mmoja wa wanachuo.

 Madai mengine ambayo yalisababisha waandamane na kugoma kuingia madarasani kuwa ni kushinikiza Rais wa serikali ya wanachuo Aristides Mujwahuzi pamoja na waziri wake mkuu Deogratias Sanga ambao walivuliwa nyazifa zao na kusimamishwa masomo kwa muda wa miezi sita,warudishwe na waendelea madaraka yao.
Kulingana na wanachuo hao madai mengine ni chuo hakina mazingira bora ya kusomea na vyoo vilivyopo ndani ya eneo hilo ni vichache ambavyo havina hadhi ,pia kuna uhaba mkubwa wa maji jambo ambalo limekuwa liwasababishia kwenda kujisaidia porini.

“ Vyoo ni vichache na vichafu,ubaguzi na udhalilishaji kutoka kwa baadhi ya wahadhiri wenye asili ya kihindi,tunapinga kuitwa majina ya mahudhurio darasani kila siku kama inavyofanyika katika shule za msingi na sekondari sisi ni wanachuo wa chuo kikuu,pia tunapinga kitendo cha chuo hiki kubadilisha  masomo tuliopangiwa na Tume ya vyuo vikuu’’,alisema mmoja wa wanachuo.
Walidai kuwa chuo hicho kina vyoo vyenye matundu 14 kati ya matundu hayo saba ya wanawake na saba ni wanaume ukilinganisha na idadi halisi ya wanachuo ambayo ni zaidi  ya 1,200 na kusababisha tundu moja kutumiwa na wanachuo 64 badala ya 20 .
 Walidai kuwa madai hayo  ndiyo yaliyosababisha uongozi wa chuo kuwaondoa madarakani Rais na serikali yote ya chuo bila taarifa kwa wanachuo ambao wameiweka madarakani  hali iliyosababisha mgomo na vurugu zilizosababisha chuo kufungwa kwa muda usiofahamika.

Mkurugenzi  na makamu St.Joseph wanena
Januari 20,mwaka huu uongozi wa juu wa chuo kikuu cha mtakatifu Joseph  ukiongozwa na Dk.Txa Ananth ambaye ni Rais wa Baraza la vyuo vikuu vya mtakatifu Joseph Afrika vinavyomilikiwa na watawa wa DMI ulitembelea chuo hicho na kubaini hakuna mawasiliano mazuri baina ya uongozi wa chuo na wanachuo.
Kutokana na hali hiyo viongozi hao wa juu wa St.Joseph walikubali kufungwa kwa chuo hicho ili kutoa fursa ya kupatia ufumbuzi uliosababisha mgomo chuoni hapo na kuahidi kuundoa uongozi wote wa chuo na kuboresha miundombinu yake.
Kwa upande wake makamu mkuu wa chuo cha mtakatifu Joseph Sr.Antonia DMI amekiri kufungwa kwa chuo hicho kwa muda usiojulikana kwa wanafunzi wanaosoma ngazi ya shahada huku wanachuo wanasoma ngazi ya stashahada wakiendelea na masomo yao.
“Chuo kimefungwa kutokana na vurugu na mgomo wa wanachuo ambao wamegoma kuingia drasani na kufanya vurugu  ikiwemo kuweka gundi aina ya superglue kwenye kufuli za milango ya madarasa’’ ,alisema na kuongeza kuwa mgomo huo pia umesababishwa na kuondolewa kwa serikali ya wanachuo akiwemo Rais na katibu wake kwa kosa la kufanya mkutano bila taarifa kwa uongozi wa chuo.
Hata hivyo Sr.Antonia amepinga madai ya wanachuo kubaguliwa,kudhalilishwa na kunyanyaswa na kusisitiza kuwa kila kinachofanyika katika chuo hicho ni kwa mujibu wa sheria za chuo ambazo pamoja na mambo mengine zinazuia mwanachuo kufika chuoni akiwa na  vifaa vya mawasiliano kama vile simu na kompyuta.
Wanachuo 40 washikiliwa na polisi
WANANCHUO 40  wa chuo kikuu cha mtakatifu Joseph tawi la Songea walishikiliwa na jeshi la polisi mkoani Ruvuma kwa kosa la kwa siku mbili kwa kosa la kukusanyika katika eneo la chuo wakati chuo kimefungwa kwa muda usiojulikana.
Chuo cha mtakatifu Joseph tawi la Songea kilifungwa  tangu Januari 15,mwaka huu kutokana na vurugu na mgomo wa kuingia darasani wa wanachuo wakidai madai mbalimbali.
Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma Deusdedith Nsimek alisema  siku ya Jumanne asubuhi majira ya saa mbili asubuhi wanachuo  zaidi ya 300 walikusanyika katika chuo cha mtakatifu Joseph  kwa madhumuni ya kufanya vurugu kwa madai kuwa hawatambui kama chuo kimefungwa wakitaka kuingia chuoni.
Kamanda Nsimek alisema wanachuo hao walipohojiwa na polisi kwanini wamekusanyika katika eneo hilo,walianza kuporomosha matusi kwa askari na kuwarushia mawe ndipo ikawalazimu askari kutumia nguvu ikiwemo kupiga mabomu ili kuwatawanya wanachuo hao ambao idadi yao iliendelea kuongezeka.
Kamanda huyo wa polisi mkoa wa Ruvuma alisema wanachuo walikataa kutii agizo la serikali badala yake waliendelea  kukusanyika eneo la chuo kila siku licha ya ulinzi wa jeshi la polisi ulioimarishwa chuoni hapo tangu kufungwa kwa chuo hicho.
Kulingana na Nsimek siku ya tukio wanachuo walikusanyika na kuanza kurusha mawe kwa askari huku wakiungwa mkono na makundi ya wanachuo waliokuwa wanatoka maeneo ya jirani pamoja na waendesha pikipiki na kwamba licha ya kutangaziwa zaidi ya mara tatu na polisi watawanyike kwa kuwa mkusanyiko wao haukuwa na kibali lakini walikataa ndipo askari waliwatanya na kufanikiwa kuwakamata wanachuo 40.
“ Miongoni mwa waliokamatwa ni Rais wa chuo hicho Aristides Munjwahuzi,Rais wa chuo aliyeondolewa madarakani na uongozi wa chuo, ameonekana kuwa ndiyo anawaongoza wenzake kukusanyika na kutotambua amri ya kufungwa kwa chuo hicho’’,alisema.
Kauli ya serikali ya mkoa kuhusu mgomo
 Mnamo Januari 16 mwaka huu mkuu wa wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti  akitoa tamko la serikali kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu aliwaasa wanachuo waache vurugu na kutawanyika ili kuheshimu maamuzi ya chuo kufungwa hadi hapo madai yao yatakapopatiwa ufumbuzi kupitia Taasisi zinazohusika na elimu ya juu
 Kufuatia mgogoro huo kuendelea serikali ya mkoa wa Ruvuma imeingilia kati kwa kuita bodi ya chuo hicho na kukaa nayo na imewataka wazimalize tofauti zao ili masomo yaweze kuendelea.
Akiongea na waandishi wa habari  ofisini kwake mkuu  wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu  alisema kuwa serikali ya mkoa imeamua kuiita bodi ya chuo hicho na kuitaka ikamalize tofauti hizo ambazo uongozi wa chuo hicho umekuwa ukilalamikiwa mara kwa mara na wanachuo hao ambao wamedai kuwepo kwa kero nyingi ambazo zimeshindwa kutekelezeka.

 Mwambungu alisema kuwa chuo cha st.Joseph tawi la Songea kinahitaji kifanyiwe marekebisho makubwa ili kiende sanjari na vyuo vikuu vingine vya hapa nchini hivyo bodi ya wakurugenzi wa chuo hicho ni vyema iangalie uwezekano wa kukutana na Baraza la vyuo vikuu hapa nchini kwa lengo kuboresha mazingira ya chuo hicho ili kiendane na hadhi ya vyuo vikuu vingine.
Katika hatua nyingine chuo hicho kimefikia hatua ya kulitia aibu kanisa katoliki nchini baada ya baadhi ya wahadhiri kuanza kupigana wenyewe kwa wenyewe huku wakiumana meno sehemu mbalimbali za mwili baada ya  dean wa wanachuo raia wa India aliyefahamika kwa jina moja la Nicholus kukataa kusaini wanachuo 25 kufukuzwa chuo ambao wanadaiwa kuwa vinara wa mgomo.

 Chuo kikuu cha mtakatifu Joseph Songea kilianza mwaka 2004 kikiwa na wanachuo wachache ambapo hivi sasa chuo hicho kina idadi kubwa ya wanachuo ambao ni 685 kati yao wanaume ni 558 na wanawake 127 ambao wanasoma stashahada na shahada katika Sayansi ya kompyuta.
Hata hivyo kuanzia mwaka wa masomo uliopita chuo kimeanza kutoa  masomo ya shahada ya Sayansi ya elimu ambapo tayari kuna wanachuo 205 wanaosoma kozi hiyo na kwamba katika chuo hicho kampasi ya Songea tangu mwaka 2010  kinatoa masomo ya shahada ya kilimo  ambapo tayari kuna wanachuo 173 kati yao wanaume ni 119 na wanawake 54.

No comments:

Post a Comment